WANAWAKE watatu raia wa Rwanda wanaosadikiwa kuendesha biashara ya ukahaba mjini Dodoma wamekamatwa na kupewa siku tatu kuondoka nchini, huku wawili kati yao wakikutwa na vidonge vya kupunguza makali ya virusi ya Ukimwi (ARVs).
Kukamatwa kwa wanawake hao ambao ni Esperance Hagenimana (28), Vestina Zaninika (27) na Ziada Mukamurera (25), kunafuatia mmoja wao Esperance kwenda kutoa taarifa kituo cha polisi kuwa alikuwa ameibiwa fedha taslimu Sh 800,000 na hati ya kusafiria.
Lakini, Polisi walipofika nyumba ya kulala wageni waliyofikia iliyopo eneo la Area D walikuta wanawake wengine wawili ambao walikuwa wakikaa chumba kimoja na Esperance.
Uchunguzi wa Polisi ulibaini kuwa mwanamke huyo hakuibiwa na kubaini wote si raia wa Tanzania. Hata hivyo kilikosekana kifungu cha kuwashitaki ndipo waliamua kupeleka sakata hilo Uhamiaji ili liweze kushughulikiwa.
Kulingana na maelezo yao, Esperance alitangulia kuja nchini kisha kuwaita wenzake ambao ilikuwa ni mara ya kwanza kuja nchini, lakini hata hivyo alisema kuwa, kumekuwa na makundi ya wanawake kutoka Rwanda wanaokuja nchini kipindi cha Bunge na hata mwaka jana kuna kundi lilikuja wakati wa mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Kulingana na uchunguzi uliofanywa na Uhamiaji, wanawake hao waliingia nchini na kujitambulisha kuwa walikuja Dodoma kufanya biashara ya vitenge, lakini hawakuwa hata na kitenge kimoja ambacho kingeweza kuwaonesha kuwa walikuwa wakifanya biashara hiyo.
Juhudi hizo za Uhamiaji zinadaiwa kuwafikisha hadi klabu moja maarufu ya usiku iliyopo eneo la Area D ambapo walinzi wa Kimasai walikiri kuwafahamu wanawake hao na walikuwa wakiwafuata nyumba ya wageni waliyofikia kama mtu alikuwa akiwahitaji na walikuwa na ni wateja wa klabu hiyo ya usiku.
Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Naibu Kamishna wa Uhamiaji, Ofisa Uhamiaji Mkoa wa Dodoma, Norah Massawe alikiri kukamatwa kwa wanawake hao na polisi na kukabidhiwa Uhamiaji.
CHANZO: HABARILEO.