SERIKALI ya Tanzania imeomba Malawi iache kutapatapa kuhusu mgogoro wa mipaka wa ziwa Nyasa kufuatia Rais wa nchi hiyo, Joyce Banda kutangaza katika baadhi ya vyombo vya habari kuwa atapeleka suala hilo kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Haki(ICJ), badala yake isubiri uamuzi wa jopo la usuluhishi lifanye kazi na litoe maamuzi.
Aidha serikali imesema kuwa hata siku moja haijapelekewa taarifa wala nyaraka za siri kutoka kwa Katibu wa jopo hilo, ambalo linahusisha marais wastaafu wa zamani wa Afrika na wanasheria kama ilivyodaiwa na Rais Banda katika vyombo hivyo , kuwa kuna Mtanzania anayeitwa Dk. John Tesha ambaye wanaamini ametoa habari na kuiba nyaraka za siri.
Akizungumza na Waandishi Habari leo Waziri Membe amesema kuwa Tanzania na jopo hilo limestushwa juu ya madai hayo na hatua ya Rais Banda kupoteza imani.
Membe amesema Serikali ya Tanzania ina imani na jopo linaloongozwa na Rais mstaafu wa Msumbiji , Joachim Chissano na marais wengine ambao ni Festus Mogae na Thabo Mbeki , kwa kuwa lina watu wenye uzoefu, wataalamu na wachapakazi. Pia kuna jopo la wanasheria na wataalamu wa masuala ya migogoro limeundwa na ni la watu saba,” alisisitiza Waziri Membe.
Akirejea mazungumzo ya makubaliano yaliyofanyika Novemba 17, mwaka jana(2012) kuwa walikubaliana hapo walipo katika jopo hilo ndipo sehemu ya mwisho. Hivyo wataenda ICJ iwapo watashauriwa na jopo la mzee Chissano.
Hivyo ameiomba serikali ya Malawi iache kutapatapa mara Uingereza, Marekani ,Jumuia ya Madola na Umoja wa Afrika(AU) na kuona viongozi mbalimbali wa dunia, bali iamini jopo la Mzee Chissano. Matokeo ya utafiti wao upo uwezekano wa kuyakubali au kuyakataa.
Akizungumzia kuhusu utoaji wa ripoti ya jopo hilo utakuwa ni lini,Waziri Membe amesema Tanzania haina haraka juu ya jambo hilo.
No comments:
Post a Comment