Thursday, September 12, 2013

ALIYEIBA 'BODABODA' AKUTWA AMEJIFICHA KWENYE PAA LA NYUMBA

Mtu anayedaiwa kuwa mwizi wa pikipiki za biashara maarufu kama Bodaboda, hivi karibuni alichomolewa kutoka ndani ya paa la nyumba alikokimbilia kujificha baada ya kuoneshwa bastola ya polisi huko Temeke, karibu na kituo cha mabasi cha daladala cha Bandari jijini Dar.

  Mwizi huyo akitolewa kwenye paa la nyumba.
Tukio hilo lililojaza umati lilitokea baada ya mtuhumiwa huyo kukimbizwa na askari waliokuwa na silaha kufuatia jaribio lake la kupora pikipiki hiyo kushtukiwa.
Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo ambaye jina linahifadhiwa, alisema kuwa mtuhumiwa alipofika nyumbani hapo kwa nia ya kujificha, mikononi mwake alikuwa ameshika visu viwili huku akidai kuwa mwenzake aliyekimbia, ndiye aliyekuwa na  bunduki iliyotumika kumtishia dereva wa bodaboda ili kumnyang’anya pikipiki.
Baada ya kuingia katika nyumba moja iliyo pembeni mwa kituo hicho cha daladala, mtuhumiwa huyo alipanda juu ya dari na kuanza kutambaa akitokomea chumba kimoja baada ya kingine.
Kuona hivyo, wananchi walisaidiana na polisi kumdhibiti.
Mmoja wa askari asiye na sare alipanda juu ya paa hilo na kumwelekezea bastola, akitishia kumlipua kama hatashuka kwa hiyari, kitendo kilichomlazimisha jamaa huyo kutii amri na kuteremka.
Shuhuda huyo alisema kuwa matukio hayo ya uporaji wa pikipiki yamekuwa mengi wilayani Temeke ambapo yamekuwa kero kubwa kwa wananchi, kiasi kilichosababisha mtuhumiwa huyo kupata wakati mgumu kuponyoka.
“Unajua ujambazi umezidi sana hapa Temeke na kuna baa moja kubwa (jina linahifadhiwa) ndiyo wamekuwa wakikaa kwa ajili ya kupanga mipango yao, sisi hivi karibuni tuliibiwa gari lakini tunashukuru Mungu tulilikamata baada ya Fuso moja kuligonga wakati majambazi walipokuwa wakikimbia nalo,” alisema.

Baada ya kukamatwa mtuhumiwa huyo alipelekwa kwenye Kituo cha Polisi cha Chang’ombe lakini Kamanda wa Polisi mkoa wa Temeke, Englibert Kiondo alipoulizwa na gazeti hili hatma ya tukio hilo, alisema bado halijafika mezani kwake na kuwa atafuatilia kwa mkuu wa kituo na kutoa ufafanuzi baadaye.

KESI YA SHEIKH PONDA YAAHIRISWA

Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Morogoro jana iliitaja na kuahirisha kesi inayomkabili Katibu wa Jumuiya na Taasisi ya Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda bila ya kiongozi huyo kuwapo mahakamani.
 
Kesi hiyo ilitajwa jana na Mwanasheria wa Serikali, Gloria Rwakibalila mbele ya Hakimu wa Mahakama hiyo, Agnes Ringo na kuahirishwa hadi Septemba 17 mwaka huu, wakati Mahakama itakapotoa uamuzi kuhusu maombi ya kiongozi huyo kupatiwa dhamana.
Hii ni mara ya kwanza kwa kesi hiyo kutajwa bila Ponda kuwapo, huku kukiwa na utulivu tofauti na siku zilizopita.
Mara ya mwisho Agosti 29, Ponda alifikishwa mahakamani hapo na kusababisha kusimama kwa shughuli za Serikali wilayani Morogoro baada ya ofisi kadhaa ikiwamo ya Mkuu wa Wilaya na baadhi ya mitaa kufungwa ili kupisha kusikilizwa kwa kesi hiyo.
Kadhalika Agosti 19, mwaka huu Ponda alisafirishwa kwa helikopta akiwa chini ya ulinzi mkali, na kesi yake ilivuta umati mkubwa watu.
Jana kesi hiyo ikitajwa kwenye mahakama ya ndani (chamber court) na baadhi ya wafuasi wa Ponda walionekana nje ya uzio wa mahakama hiyo huku wakiwa hawajui nini kinachoendelea.
Ilimlazimu Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Richard Kabate kutoka nje ya ofisi yake na kuwaeleza wafuasi hao sababu za kutofikishwa kwa kiongozi wao mahakamani hapo.
“Kesi hiyo imeshindikana kutajwa kwenye mahakama ya wazi kwa sababu mahakama hiyo inatumiwa kuendeshea kesi nyingine chini ya majaji wa Mahakama Kuu, hatutaki kuleta mwingiliano.
“Ninataka kuwaeleza kuwa mwondoke kwa kuwa Sheikh Ponda hakufikishwa mahakamani hapa leo hadi Septemba 17 atakapoletwa kwa ajili ya kutolewa kwa uamuzi wa dhamana,” alisema Hakimu Kabate.
Baada ya Hakimu Kabate kutoa ufafanuzi huo, wafuasi hao walionekana kutoridhishwa na kauli hiyo na kuanza kujikusanya vikundi vikundi, lakini baadaye walianza kutawanyika.
Mashtaka yaliyotajwa mahakamani hapo na kumkabili Sheikh Ponda ni matatu ambayo ni uchochezi, kuharibu imani ya watu wengine na kushawishi kutendeka kwa kosa, mashtaka ambayo anadaiwa kuyatenda Agosti 10 mwaka huu eneo la Kiwanja cha Ndege Manispaa ya Morogoro.
Sheikh Ponda anatetewa na mawakili watatu wakiongozwa na wakili Msomi Juma Nassor ambaye tayari amewasilisha ombi la dhamana.

WANANCHIA WATUMIA VYANDARUA KUTENGENEZEA VYOO


Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mkoani Singida Edward Ole Lenga akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kinampundu mara baada ya kukabidhiwa Zahanati na nyumba mbili za mganga na shirika moja lisilo la kiserikali la HAPA,hafla hiyo ilifanyikajuzi kijijini hapo.

Ni Mwakilishi wa shirika la SIMAVI kutoka nchini Uholanzi Lieke Ongering akizungumza katika hafla ya kukabidhi mradi wake kwa ushirikiano na shirika la HAPA Singida kukamilisha mradi wa ujenzi wa Zahanati na nyumba mbili za mganga kijiji cha Kinampundu takribani umbali wa kilomita 70 kutoka mjini Singida.
 
Ni mmoja wa kinamama wajawazito akipimwa uzito na mkuu wa Wilaya ya Mkalama Ole Lenga mara baada ya kukabidhiwa vifaa vya zahanati hiyo, anayeshuhudia kipimo hicho ni mhasibu mkuu wa shirika hilo Noel Makyao.

Mkurugenzi wa HAPA Davd Mkanje  (Kulia) kimkabidhi DC wa Mkalama Ole Lenga baadhi ya vifaa vya kutolea huduma kwenye Zahanati hiyo wakati wa hafla fupi ya makabidhiano ya mradi huo.

Ni baadhi ya wageni kutoka Mataifa mbalimbali nje ya nchi wakicheza muziki na wananchi wa kijiji cha Kinampundu mara baada ya kukabidhiwa mradi huo wa afya ya uzazi wa mama na mtoto.
Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Ole Lenga, kushoto mwenye suti, mwakilishi wa SIMAVI, Lieke, MMkurugenzi wa shirika la HAPA, Davd Mkanje na mhasibu mkuu wa shirika hilo Noel Makyao wakifurahia pamoja na wananchi mara baada ya kukabidhi mradi huo.


Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mkoani Singida ameonya tabia ya baadhi wananchi kuezekea kwenye vyoo vyandarua vya kujikinga na mbu wa malaria.

Onyo hilo limetolewa mwishoni mwa wiki iliyopita na Mkuu huyo wa Wilaya, Edward ole Lenga wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kinampundu muda mfupi baada ya kukabidhiwa Zahanti ya kijiji na shirika la HAPA.

Alisema imezuka tabia ya wananchi kutumia vyandarua hivyo kwa matumizi yasiyo rasmi ikiwa na pamoja na wengine kuvifanya kama mabanda ya kuhifadhi vifaranga vya kuku.

“Hii ni aibu, wenzetu wanatupatia vyandarua  ili tusipate malaria, nyie mnatumia kuezeka vyoo kwa kweli hii ni aibu kubwa sana na mimi nimetembea vijijini na kujionea hili, na kwa kweli atakayekamatwa atakiona cha moto.” Alisema Dc Lenga kwa masikitiko.

Aidha alisema serikali inatumia fedha nyingi kwa ajili ya kuagizi
vyandarua hivyo kwa ajili kujikinga na mbu wa malaria huku wananchi wakiziona kana kwamba hazina msaada na kuzitumia kama kinga kwenye vyoo.

“Hivi chandarua kukiezekwa kwenye choo si mtu unaonekana tu , acheni hii tabia chafu, nimeunda kikosi kila kijiji atakayebainika kufanya hivyo akamatwe na kuletwa kwangu mimi nitamshughulikia ipasavyo.” Alisisitza Ole Lenga.

Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Wilaya aliwataka wananchi wa Wilaya hiyo wanaoishi maeneo ya mijini kuja nyumbani na kujenga nyumba na vyoo bora.

Wednesday, September 11, 2013

BABY MADAH ASAINI MKATABA WA MAMILIONI YA PESA KENYA

Baby Madah
Msanii maarufu wa kike Tanzania anayefanya vizuri sana kwenye muziki na filamu,baby Madaha amelamba bingo ya uhakika na kampuni ya Candy n’ Candy Records Label ya jijini Nairobi iliyomsainisha mkataba msanii mwingine wa Tanzania Mr.Nice hivi karibuni.
Meneja wa msanii huyo  Joe Kariuki amesema kuwa  pamoja na msanii huyo kupewa mkataba huo wa million hamsini (50) pia wamempa mwanadada huyo gari ya kutembelea ya kisasa aina ya AUDI TT  na nyumba  kali mitaa kijitonyama jijini  Dar es salaam.
Pamoja na hayo pedeshee huyo wa Mr.Nice ambaye ndio mmiliki wa studio hiyo amesema wanataka kumuhamishia msanii huyo jijini Nairobi nchini Kenya kwa kipindi cha mwaka mmoja ili afanye nao kazi huko kwani wamegundua kuwa anakubalika sana nchini humo na wapenzi wa muziki.
Baby madaha ambaye  anatarajia kutua nchini leo akitoka Nairobi pamoja na meneja wake kwa ajili ya kuachia video ya  wimbo wake wa kwanza aliofanya na Label hiyo uitwao (Summer Holiday) ambao umefanywa huko huko jijini Nairobi

FRAT YAPINGA UAMUZI WA LIGI YA SHIRIKISHO TZ

Chama cha Waamuzi Tanzania (FRAT), kimepinga uamuzi wa Kamati ya Ligi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kuwafungia kwa mwaka mmoja waamuzi  Martin Saanya na Jesse Erasmo.
Ofisa Habari wa TFF, Bonifance Wambura alisema jana kuwa Saanya amefungiwa kwa kuchezesha chini ya kiwango na alitoa adhabu tata iliyoipa Union bao la kusawazisha wakati Erasmos alishindwa kumshauri mwamuzi wa kati katika tukio hilo.
Hata hivyo, Katibu Mkuu wa FRAT, Charles Ndagala alisema uamuzi huo wa Kamati ya Ligi kuwafungia Saanya na Erasmo si sahihi na hatari kwa maendeleo ya soka la Tanzania.
“Bado sijapata taarifa rasmi za kiofisi kwa vile nipo safarini, lakini kama uamuzi wao ndiyo huo wanafanya makosa makubwa ambayo matokeo yake ni kulizamisha soka letu,” alisema Ndagala na kuongeza:
“Jamani, makosa hata Ulaya yanafanywa, lakini si kosa mwamuzi anasimamishwa wakati mwingine tuwaonye na kuwapa nafasi nyingine ya kuwatazama vinginevyo tutawamaliza.”
Alisema, endapo adhabu ya aina hiyo itaendekezwa kuna hatari ligi kuchezeshwa na waamuzi wasiokuwa na uzoefu.
“Waamuzi wazuri wote wataondoka watakuja wasio na uzoefu na hapo hali ndiyo itakuwa mbaya zaidi, ebu fikiri tayari wamemfungia Akrama (Mathew) na Abbas Mahagi kama utaratibu huu utaendelea hai itakuwaje?”.
Naye mwamuzi wa zamani wa soka, Othman Kazi alisema: “Kamati ya Ligi haina tofauti na ile ya TFF  kwa sababu imefanya uamuzi uleule wa kukurupuka.

JE, KANUNI ZA BUNGE ZIMEWASHINDA NAIB SPIKA NA MBOWE?

Kumekuwa na mjadala mkali kuhusu iwapo Naibu Spika, Job Ndugai alikiuka Kanuni za Bunge katika kushughulikia vurugu zilizotokea Bungeni Alhamisi iliyopita kwa kuamuru kutolewa nje kwa Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe.
Ndugai ambaye alikuwa kiongozi wa shughuli za Bunge siku hiyo, aliwaamuru askari kumtoa nje Mbowe baada ya kukaidi amri yake ya kutaka kuketi chini aliposimama kutaka kupewa nafasi ya kuzungumza, hali iliyozua tafrani bungeni.
Pamoja na mambo mengine Ndugai amekuwa akituhumiwa kwamba anaminya uhuru wa wabunge wa upinzani kutokana na mapenzi aliyonayo kwa chama chake, CCM.
Kwa upande mwingine, kumekuwa na lawama kwamba Mbowe alikosea kukaidi amri ya Naibu Spika kwa kuwa kanuni zinamtaka mbunge yeyote (hata akiwa waziri), kuketi pale kiongozi wa Bunge (Spika, Naibu au Mwenyekiti) anaposimama, hivyo kusababisha mtafaruku.
Mwenyekiti wa Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar, Profesa Chris Peter Maina alisema tatizo lililojitokeza bungeni linaweza kumalizwa na kuwapo kwa sheria inayokataza Spika wa Bunge kuwa mwanachama wa chama chochote cha siasa.
“Unajua kwa Katiba ya sasa Spika wa Bunge anaweza kuwa mwadilifu lakini akapata shinikizo kutoka upande wa chama chake, Ibara ya 128 ya Rasimu ya Katiba Mpya inaeleza kiundani kuhusu spika kutokutoka miongoni mwa wabunge jambo ambalo ni zuri,” alisema Profesa Maina na kuongeza:
“Mwenendo wa Bunge siyo mzuri. Wabunge hawaheshimiani hata kidogo, nadhani wanahitaji kukubaliana kwa hoja, wao ndiyo wanatunga sheria, hivyo wanatakiwa kulumbana kwa kufuata utaratibu uliowekwa.”
Spika wa zamani, Pius Msekwa alisema wakati akiongoza Bunge hakuwahi kuona vurugu, fujo na malumbano ya wabunge kama ilivyotokea Alhamisi iliyopita.
“Wakati nikiwa Spika sikumbuki kama kuna siku ziliwahi kutokea vurugu za aina hii, kilichotokea ni sawa na uhalifu kwa sababu taratibu hazikufuatwa,” alisema Msekwa.
Matakwa ya Kanuni
Ibara ya 76 (1) na (2) ya Kanuni za Bunge Toleo la Aprili 2013, zinaeleza jinsi ya kudhibiti fujo bungeni, lakini Ndugai anakosolewa kwamba hakuzingatia taratibu hizo kushughulikia vurugu za Alhamisi.
Kanuni ya 76 (1) inasema: “Kwa madhumuni ya kudhibiti fujo endapo itatokea ndani ya Ukumbi wa Bunge na Spika ataona kuwa kuna haja ya kutumia nguvu, basi anaweza kuahirisha shughuli za Bunge bila ya hoja yoyote kutolewa au kusitisha kikao kwa muda atakaoutaja ili fujo hiyo iweze kudhibitiwa na Mpambe wa Bunge”.
Kadhalika, fasili ya pili ya Kanuni hiyo inasema: “Baada ya utulivu kurudia, Spika atalipeleka kwenye Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge suala ambalo lilisababisha kutokea kwa fujo ikiwa ni pamoja na jina la mbunge au majina ya wabunge waliohusika na fujo hiyo ili kamati hiyo iweze kulishauri Bunge kuhusu adhabu inayostahili kutolewa”.
Wakati vurugu zilipozuka bungeni, Ndugai aliwaita askari badala ya mpambe, kumtoa nje Mbowe na hakuwa amesitisha wala kuahirisha shughuli za Bunge kama kanuni zinavyotaka.
Pia Naibu Spika alitangaza kumsamehe Mbowe na Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ kwa maana ya kuwaruhusu kuendelea na vikao vya Bunge siku hiyo jioni, badala ya suala hilo kupelekwa kwenye kamati husika kama kanuni ya 76 (2) inavyoelekeza.
Utetezi wa Ndugai
Ndugai alisema hakuzingatia kanuni hizo kwani mazingira ya vurugu hizo hayaendani na kanuni husika, hivyo alitumia nafasi yake ambayo pia inatambuliwa na kanuni za Bunge.
“Vurugu zilikuwa zimepangwa na zilifanywa kwa makusudi ili kuhakikisha kwamba shughuli za Bunge zinakwama maana hiyo kanuni wanafahamu kwamba ipo, sasa hatuwezi kuwa na Bunge ambalo mtu akiamua tu anafanya fujo ili liahirishwe,” alisema Ndugai na kuongeza:
“Mimi kama kiongozi wa shughuli za siku hiyo, kazi yangu ni kuhakikisha kwamba shughuli zilizopangwa zinafanyika, kwa hiyo nisingeweza kuruhusu watu wachache watukwamishe kutokana na masilahi yao.”
Alipoulizwa kwamba alifahamu vipi kuwapo kwa njama hizo, alisema kauli na matendo ya wabunge wa upinzani vilionekana tangu mwanzo wa mjadala kutaka kukwamisha shughuli za Bunge siku hiyo.
Kuhusu kuwatangazia wabunge hao msamaha badala ya kupeleka suala hilo kwenye kamati husika, Ndugai alisema: “Hakukuwa na adhabu kubwa ya kuwapa zaidi ya kuwatangazia msamaha.”
“Niliwasamehe kwa mujibu wa kanuni maana zinaruhusu kuzingatia uamuzi ambao uliwahi kutolewa na maspika waliopita, kwa hiyo kama unakumbuka kesi ya Mengi (Regnald) na Malima (Adam), Spika Samuel Sitta baada ya kumwita Malima akakataa kwenda alisema anamsamehe,” alisema na kuongeza:
“Yeye (Sitta) alitumia neno kwamba nimeamua kumpuuza lakini mimi sikusema hivyo, nilisema kwamba namsamehe kwa sababu tu namheshimu na ni kiongozi mkubwa tu katika jamii”.
Mbowe hakupatikana juzi na jana kuzungumzia suala hilo, lakini Mnadhimu Mkuu wa Upinzani Bungeni, Tundu Lissu alisema kiongozi wake huyo hakufanya makosa kwani alisimama wakati Mbunge wa Vunjo (TLP), Augustine Mrema alipokuwa akizungumza na kwamba hilo siyo kosa kikanuni.
Alisema Ndugai alipaswa kumheshimu Mbowe kwa kuzingatia wadhifa wake bungeni na kwamba kitendo cha kumwambia “kaa chini” hakikubaliki.
“Hatuwezi kuruhusu na hatutaruhusu Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kudhalilishwa, ikiwa tutaruhusu hilo litokee, basi miongoni mwetu sisi wapinzani hakuna atakayepona,” alisema Lissu na kuongeza:
“Naibu Spika amelidhalilisha Bunge kwa sababu kwa kumdharau Mbowe ni kwamba amemdharau mmoja wa viongozi wakuu wa Bunge”.
Wabunge wa Kambi ya Upinzani Bungeni wakizuia Kiongozi wa kambi hiyo, Freeman Mbowe (aliyevaa tai ya njano) asitolewe nje ya Ukumbi wa Bunge na Askari wa Bunge baada ya Naibu Spika, Job Ndugai kuamuru atolewe, kwenye kikao kilichofanyia Alhamisi ya wiki iliyopoita, mjini Dodoma. (Picha na Fidelis Felix)

MFANYA BIASHARA AMWAGIWA TINDIKALI



Matukio ya wananchi kumwagiwa tindikali yameendelea kushika kasi nchini baada ya Mfanyabiashara wa vifaa vya ujenzi, Christian Msema wa Mburahati Dar es Salaam, kumwagiwa kemikali hiyo mwishoni mwa wiki na watu wasiojulikana.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camilus Wambura alisema hana taarifa hizo licha ya tukio hilo kutokea mbele ya Kituo cha Polisi Mburahati.
“Kwa sasa sina hizo taarifa, labda mpaka niulize,” alisema Kamanda Wambura.
Msema maarufu kama ‘Mnyalu’ amelihusisha tukio hilo lilitokea jioni ya Jumamosi Septemba 8 na mgogoro wa eneo la wazi ambapo yeye alikuwa akipinga mfanyabiashara mmoja (jina linahifadhiwa) kulitumia kuegesha magari yake.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Mburahati, Dickson Tungaraza amekanusha kuwepo kwa mgogoro huo“Mimi ninachojua hakuna mgogoro… wewe uko wapi? njoo ofisini ndiyo utajua yote,” alisema.
Akizungumza katika Hospitali ya Taifa Muhimbili alikolazwa, alisema baada ya kufunga duka lake, watu waliokuwa kwenye pikipiki ya matairi matatu (Bajaj) walimwagia kemikali hiyo na kutoweka.
“Ilikuwa saa mbili usiku baada ya kufunga duka langu nikawa naelekea nyumbani, mara ikaja Bajaj ikasimama mbele yangu. Mmoja wa abiria akaniuliza, vipi bosi, ndiyo unakwenda kuangalia kiwanja chako? Nilipomwangalia ndiyo wakanimwagia tindikali,” alisema Msema na kuongeza:
“Nilipiga mayowe wezi hao wezi hao! Lakini walikimbia bila kukamatwa. Walikuja watu wakanimwagia maji na maziwa na kuniwahisha hospitali.”

Tuesday, September 10, 2013

RACHLE AKIFANYA YAKE KWENYE SERENGETI FIESTA

MSANII kutoka kundi la Tanzania House of Talent (THT), Winfrida Josephat 'Rachel' akifanya vituko  vyake stejini wakati wa Tamasha la Serengeti Fiesta 2013.

ZANZIBAR KUIFUNGULIA MASHTAKA MELI ILIYOKAMATWA NA MIHADRATI ITALY

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imesema itafungua mashtaka dhidi ya kampuni ya Gold Star, baada ya meli yake kukamatwa na tani 30 Za mihadarati aina ya bangi Kisiwa cha Malta Vessel, nchini Italia.

Mkurugenzi wa Mamalaka ya usafiri Zanzibar (ZMA) Abdi Omar Maalim akionyesha fomu za mashariti ya usajili wa meli kufuatia kukamatwa kwa meli ya MV Gold Star ikiwa na tani 30 za bangi meli hiyo imesajiliwa Zanzibar mwaka 2011.
Hatua hiyo ilitangazwa na Mkurugenzi wa Mamalaka ya Usafiri Baharini (ZMA), Abdi Omar Maalim, alipozungumza ofisini kwake Mlandege Zanzibar, jana.
Maalim alisema kwa mujbu wa sheria namba 5 ya mwaka 2006 ya usafiri baharini, kampuni hiyo imekiuka masharti ya usajili, ambayo yanazuia meli kubeba silaha, dawa za kulevya, wakimbizi au mzigo wowote wenye biashara haramu.
Alisema wanasheria wa ZMA wataipitia sheria hiyo kabla ya kuamua kuishtaki kampuni hiyo mabaharia tisa wanaodaiwa kula njma za kusafirisha bangi, kabla ya kukamatwa huko Italia.
“Tunategemea kufungua mashtaka dhidi ya Kampuni ya Gold Star kwa kukiuka masharti ya fomu ya usajili, ambayo yanazuia meli kubeba mihadarati, silaha, wakimbizi au mzigo wowote haramu,” alisema Maalim.
Alisema meli hiyo ilisajiliwa Oktoba 5, 2011 na Kampuni ya Uwakala wa Kusajili Meli ya Philtex Corparation yenye kituo chake kikubwa cha biashara nchini Dubai, inamilikiwa na raia wa Marekani na Phillipines.
Maalim alisema Kampuni ya Philtex ina mkataba wa miaka 10 wa kusajili meli na SMZ, ikiwa na hisa asilimia 35 na SMZ 65.
Alisema mkataba huo ulitiwa saini mwaka 2007 na umeweka sharti kuwa, hakuna kampuni yoyote yenye mamlaka ya kusajili meli kwa niaba ya SMZ zaidi ya kampuni hiyo hadi miaka 10 itakapoisha.
Alisema kulingana na mkataba huo, upande wowote utakaovunja masharti kabla ya muda kumalizika utalazimika kulipa fidia ya dola 500,000 za Marekani na kusisitiza kuwa, Philtex
haina makosa kufuatia meli hiyo kukamatwa na bangi kwa vile ni uhalifu wa kawaida kama inavyotokea kwa meli nyingine.
Hata hivyo, Maalim alisema shehena hiyo ya bangi haieleweki hadi sasa kama ilikuwa ikisafirishwa kutoka Morocco au Uturuki na kwamba, mzigo huo haukutoka Tanzania kama ilivyoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari.
Kuhusu Philtex kukumbwa na misukosuko ya usajili tangu kuanza kufanya usajili kwa niaba ya SMZ, Maalim alikiri mwaka jana meli 36 za Iran zilifutiwa usajili baada ya kubainika kusajiliwa kinyume na sheria za kidiplomasia.
“Iran imewekewa vikwazo na Baraza la Usalama wa UN, zilifutiwa usajili wake baada ya kujitokeza malalamiko ya Zanzibar kusajili meli za mafuta za Iran,” alisema.

RAY NA LULU WACHAGULIWA KUWA MABALOZI WA WASANII DFF 2013

Ray na lulu wachaguliwa kuwa mabalozi wa wasanii Tamasha la Filamu 2013 (DFF 2013)Waigizaji Elizabeth Michael (LULU) na Vicenti Kigosi (Ray) wamechaguliwa kuwa mabalozi wa wasanii wenzao katika tamasha la filamu la Dar filamu Festival litakalofanyika kuanzia tarehe 24 – 26. Katika press Release iliyotolewa na kampuni inayoandaa tamasha hilo imesema kuwa pamoja na mambo mengi, tamasha hilolitatoa mafunzo kwa wadau mbalimbali wa Filamu Tanzania.

Soma press Release hiyo HAPA.

Kampuni ya Haak Neel Production kwa kushirikiana na mtandao wa habari za filamu wa filamucentral inapenda kutambulisha kwenu Tamasha la filamu linaloitwa Dar Filamu Festival (DFF) 2013 litalofanyika katika uwanja wa CoICT- UDSM- Posta Kijitonyama, kuanzia tarehe 24- hadi 26, September,2013 Tamasha litaambatana utoaji wa Semina kwa wadau wa filamu, kuonesha filamu za kitanzania kwa watu wote bure kwa siku tatu.Kutakua na filamu nne kwa siku kuanzia saa kumi na mbili jioni mpaka saa tano usiku.

Tamasha hilo limelenga kutoa hamasa kwa watanzania kuziona filamu za kitanzania na zile zinazotumia Lugha ya Kiswahili pekee ili kutoa fursa ya ajili kwa vijana na jamii husika kwa ujumla, filamu zitakazoonyeshwa ni zile zinazotengenezwa na hapa nchini katika kutangaza Lugha yetu nzuri ya Kiswahili kupitia kazi zao ikiwa kampeni ya filamucentral kuitangaza lugha hiyo na kuwa ni bidhaa muhimu Ulimwenguni.
Kwa tamasha hili la awali tutaonyesha filamu za hapa Tanzania pekee ikiwa ni utambulisho wa Dar Filamu Festival kwa mara ya kwanza kwenu wanahabari, miaka ijayo Tamasha litahakikisha linashirikisha filamu kutoka sehemu mbalimbali zinazotumia Lugha ya Kiswahili kutoka popote Ulimwenguni.
Akiongea na Waandishi wa Habari mratibu wa Tamasha hilo Staford Kihore pia amesema kuwa katika kuzingatia maendeleo ya tasnia ya filamu siku tatu hizo kila siku imepewa jina kwa filamu zitakazoonyeshwa Tarehe 24th September, 2013 siku ya Jumanne ambayo ndio siku ya ufunguzi utakuwa ni usiku wa Bongo Movie Classics, 25th September, 2013 ni usiku wa Quality Nights.
Na ile siku ya mwisho tarehe 26th September, 2013 itakuwa ni Stars Nights siku ambayo kutakuwa na wasanii wetu mbalimbali ambao wanajenga soko hilo la Bongo movie filamu, Tamasha hili linapambwa na wasanii wote wakiwakilishwa na wasanii wenzao wawili ambao ni Vincent Kigosi ‘Ray’ kama Official Producer and Director for DFF 2013 na Elizabeth Michael ‘Lulu’ kama Official Actress for DFF 2013.
Pia tamasha litaambatana na utoaji wa semina kwa wadau wa filamu kwa asubuhi ambapo madarasa yataendeshwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Idara ya Sanaa tarehe 24 September, 2013 masomo ya Uandishi wa Muswada, Uigizaji na Uongozaji wa filamu yatafundishwa kwa washiriki, 25th September 2013 Siku nzima Makapuni ya Utengenezaji filamu yataonyesha na kutangaza kazi zao kwa wadau mbaliambali.
Tarehe 26th September 2013 ni siku muhimu sana kwani Taasisi kama vile TRA, Bodi ya Ukaguzi wa filamu na michezo ya kuigiza, Wasambazaji wa filamu na taasisi nyingine watakutana katika jukwaa la majadiliano kuhusu mustakabali wa tasnia ya filamu, pia filamu kadhaa zitaonyeshwa na kujadiliwa na wadau watakaokuwepo matukio yote ya asubuhi yatafanyika Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam Idara ya Sanaa.
Pia tunatoa shukrani kwa taasisi za Serikali kutuunga mkono katika ufanikishaji wa tamasha hilli la Dar Filamu Festival (DFF) 2013, taasisi kama Bodi ya Filamu na ukaguzi wa michezo ya kuigiza Tanzania, Fine Perfoming Art – Udsm, Tanzania Film Federation (TAFF), MFDI, Swahiliwood na makapuni ya usambazaji wa filamu Steps Entertainment Ltd, Leo Media na kampuni mpya ya usambazaji ya Proin Promotion ambayo imeanza hivi karibuni na kuonyesha dhamira ya kusaidia tasnia ya filamu, pia leo tunazindua mtandao wa www.dff.or.tz
Kwa kutambua mchango wako kama mwanahabari tunaamini utaungana nasi katika kuhakikisha DFF inakuwa ni chachu ya maendeleo ya tasnia ya filamu Tanzania, huku tukisema kuwa Dar Filamu Festival2013 kwa kauli mbiuya ‘Ubora wa Filamu Zetu’ ikiwa ni njia ya kuwakutanisha wadau wote kwa pamoja na kuwa jukwaa linalojenga tasnia ya filamu inayokua kila siku. Pia tunaomba ushiriki wako katika kufanikisha hili.
Imetolewa na Mratibu wa Tamasha la DFF 2013 Staford Kihore.

RUTO NA SANG WAKANA MASHTAKA ICC

Kesi dhidi ya naibu rais wa Kenya William Ruto, imeanza kusikilizwa katika mahakama ya kimataifa ya ICC huko Hague.
Naibu rais wa Kenya William Ruto.
Bwana Ruto anayetuhumiwa kwa kuchochea ghasia za baada ya uchaguzi mkuu mwaka 2007, alikana mashtaka yote dhidi yake. Vile vile mshtakiwa mwenza mtangazaji wa redio Joshua Arap Sang pia alikana mashtaka.
Rais Uhuru Kenyatta ambaye pia anatuhumiwa kuhusika na ghasia hizo anatarajiwa kufika mbele ya mahakama hiyo mwezi Novemba.

SHEHENA YA MADAWA YA KULEVYA ILIYOKAMATWA KUMBE NI YA MHSHMIWA MBUNGE

Ilikuwa ni siri Imetawala kuhusu mmiliki wa meli ya Kitanzania iliyonaswa juzi nchini Italia, ikiwa na tani 30 za madawa ya kulevya aina ya bangi lakini sasa kila kitu kinaweza kuwekwa nje bin hadharani kutokana na taarifa mpya.
Mv Gold Star ikiungua.
tunazo ‘data’ kuwa mmoja wa wamiliki wa meli hiyo ni mfanyabiashara wa Kitanzania mwenye asili ya Bara la Asia ambaye alipata kuwa memba wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika awamu zilizopita.

Jina la mfanyabiashara huyo linabaki kwenye kapu letu mpaka baadaye tutakapokuwa kwenye mazingira sahihi ya kumtaja, kwani kufanya hivyo kwa sasa ni kuingilia mamlaka za kisheria ambazo zipo kwenye uchunguzi makini.
Habari zinafafanua kuwa mbunge huyo, hamiliki meli hiyo peke yake, bali kuna watu wengine ambao ni raia wa Visiwa vya Marshall, barani Australia.


Inaelezwa zaidi kwamba watu hao kutoka Marshall ni mabilionea wakubwa ambao wanamiliki visiwa vitatu kwenye Bahari ya Pacific ambavyo ni Ujae Atoll, Ujelang Atoll na Lib.

Mabilionea hao ndiyo wenye Kampuni ya Gold Star Shipping ambayo inajihusisha na utoaji wa huduma za usafiri wa majini hususan kwa njia ya meli.
Magunia ya bangi japo siyo yaliyokuwa katika MV Gold Star.

Gold Star Shipping ni kampuni iliyosajiliwa Visiwa vya Marshall lakini kwa ushirikiano na mbunge huyo wa zamani, waliileta nchini meli yao ya mizigo ya MV Gold Star, ikasajiliwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ).

MV Gold Star ilisajiliwa Zanzibar ili tu ipate kibali cha kutumia Bendera ya Taifa la Tanzania, kwani baada ya hapo, imekuwa ikipuyanga kwenye mataifa mengine, ikitoa huduma za usafiri pasipo kurudi kwenye nchi iliyosajiliwa.
Taarifa za hivi karibuni, zinaonesha kuwa imeshakwenda na kurudi Misri mara mbili, Algeria mara mbili na Uturuki, huku Bandari ya Zanzibar ambayo inaitambulisha kama ndiyo nyumbani kwao, haijapata kutia nanga hata mara moja.

Julai 29, 2013, saa 2:04 asubuhi, ilitia nanga Bandari ya Said, Misri. Juni 18, 2013, saa 1:05 jioni, iliwasili Bandari ya Mostaganem, Algeria. Mei 31, 2013, saa 9:04 usiku, ilifika Bandari ya Iskenderun, Uturuki. Mei 24, 2013, saa 1:04 asubuhi, iliingia Bandari ya Said, Misri na Aprili 14, 2013, saa 2:02 asubuhi, ilipiga king’ora Bandari ya Mostaganem, Algeria.

Bandari ya nyumbani ni Zanzibar, imetengenezwa mwaka 1975, watengenezaji ni Kampuni ya Astilleros De Mallorca, iliyopo Palma De Mallorca, Hispania, mmiliki ni Gold Star Shipping kutoka Visiwa vya Marshall, meneja ni Gold Star Shipping, ipo katika jamii ya Hellenic Shipping Register.

Ilimilikiwa na Ibrahim Junior mpaka Februari 2011, Breogan I (aliiuza Novemba 2006), Breogan (Machi 2002), Estela De Mar (Desemba 1996), Inezgane (1996), Puerto Suances (1988) na Suecia (1985).

Kwa mujibu wa ripoti za mitandao ya Waitaliano na Waingereza, MV Gold Star, ilipakia mzigo wa madawa ya kulevya nchini Uturuki na walikuwa wanafanya jaribio la kuingiza mzigo huo wenye tani 30 nchini Italia.

Walinzi wa ufukweni kwenye Bahari ya Mediterranean, waliishtukia meli hiyo na kuizingira, watu waliokuwemo baada ya kuona hali ni mbaya, waliwasha moto kuiteketeza MV Gold Star kisha kufanya jaribio la kutaka kutoroka kupitia boti ndogo.

Askari hao wa ufukweni, walishirikiana na maofisa uhamiaji wa Italia kuwakamata watu tisa ambao walikuwemo kwenye meli hiyo na baada ya kuwahoji, ilibainika wote wanatokea nchi za Misri na Syria.
Taarifa kutoka kwa maofisa uhamiaji wa Italia zinasema kwamba baada ya kuwahoji watuhumiwa, ilibainika waliamua kuiteketeza meli hiyo kwa moto ili kuondoa ushahidi wa tani 30 za madawa ya kulevya zilizokuwemo.
Ilibainishwa pia kuwa thamani ya madawa hayo ya kulevya yaliyokamatwa ni pauni milioni 50 ambazo kwa chenji ya Tanzania ni shilingi bilioni 126.5.
 
Kama mzigo huo ungevuka salama na kuuzwa, fedha hizo zinatosha kuendesha wizara tatu katika Serikali ya JK, hii ni kwa mujibu wa makadirio na mapato ya matumizi (bajeti), mwaka wa fedha 2013-2014.

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto bajeti yake ni shilingi bilioni 23, Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo shilingi bilioni 30 na Wizara ya Maendeleo ya Uvuvi na Mifugo shilingi bilioni 67, jumla shilingi bilioni 120.

Hii inamaanisha kuwa fedha hizo za wauza unga, zinaweza kuendesha wizara hizo na chenji itabaki shilingi bilioni 6.5 ambazo zinaweza kujenga shule na mabweni mengi tu. Uchambuzi huo ni kuonesha namna ambavyo wauza unga walivyo watu hatari, kwani wana pesa nyingi.
 
Baada ya kuwakamata watuhumiwa hao, vikosi vya uokoaji nchini humo, kuanzia vya majini, anga na nchi kavu, viliizingira meli hiyo kuzima moto uliokuwa unaiteketeza.

Mpaka tunakwenda mitamboni, taarifa zilieleza kwamba bado shughuli ya kuzima moto ilikuwa inaendelea.
 
Tuilifanya jitihada za kuwatafuta watu mbalimbali wanaohusika na udhibiti wa madawa ya kulevya nchini lakini hakuna hata mmoja aliyekuwa na taarifa.
Hata Kamanda wa Kikosi cha Kudhibiti na Kupambana na Madawa ya Kulevya, Godfrey Nzowa, aliliambia  akiwa nchini Ethiopia kuwa hajui chochote kuhusu meli hiyo kukamatwa lakini aliahidi kufuatilia.

Kukamatwa kwa meli hiyo kunazidi kuipaka matope Tanzania, kwani hivi karibuni raia wake wamekuwa wakikamatwa katika mataifa mengine, wakiwa wanasafirisha madawa ya kulevya. Vilevile, kuna ile skendo ya meli ya Wairan yenye Bendera ya Tanzania ambayo iliibua gumzo mwaka huu lakini suluhisho halijapatikana. 

WABUNGE WAVUTANA MBELE YA MH. RAIS

 Wabunge wa majimbo mawili ya wilaya ya Kwimba Mkoani Mwanza, Mh. Richard Ndassa wa sumve na Mh. Shanifu Manssor wa jimbo la Kwimba wamevutana mbele ya rais Dk. Jakaya Mrisho Kikwete kuhusu utekelezaji wa mradi wa kupeleka maji mjini Ngudu na kumlazimu rais kumtaka waziri wa maji Prof. Jumanne Maghembe kutoa ufafanuzi kuhusu utekelezaji wa mradi huo.

Mvutano huo umekuja kufuatia taarifa ya wilaya ya Kwimba iliyosomwa kwa rais Jakaya Kikwete na mkuu wa wilaya hiyo Bw. Selemani Mzee, ambaye amesema hali ya huduma ya maji mjini Ngudu kwa sasa ni mbaya kupindukia ambapo idadi ya wananchi wanaopata majisafi na salama ni 11,310 tu kati ya watu 25,370, idadi ambayo ni sawa na asilimia 44.6 kutokana na mji huo kutegemea visima virefu vitano, ambavyo vilichimbwa miaka kati ya 27 na 57 iliyopita, huku pia uwezo wa chanzo cha maji kilichopo kikiwa ni mita za ujazo 265 kwa siku, ambapo maji hayo hutolewa kwa mgao kila baada ya siku tatu.

Huku kila mbunge akionekana kuvutia upande, mbunge wa Sumve Mh. Richard Ndasa ameshauri mradi huo wa kupeleka maji katika mji wa Ngudu utokee Magu kupitia jimboni kwake ili kuvinufaisha vijiji zaidi ya 40, huku mbunge wa jimbo la Kwimba Mh. Shanifu Mansoor akisema kuwa ni vizuri serikali iendelee na mpango wake wa kutumia maji ya ziwa victoria yanayotolewa kwenye mradi wa Kahama- Shinyanga ( kashwasa ) na kuyapeleka ngudu kutokea kijiji cha mhalo, hatua ambayo itanufaisha vijiji zaidi ya 60 vya tarafa ya mwamashimba na Ngudu.

Katika kuweka sawa hali ya mambo, waziri wa maji Mh. Prof. Jumanne Maghembe amesema kwamba serikali itatekeleza miradi yote miwili, ambayo ni ya kutoa maji kijiji cha Mhalo kwenda Runere na hatimaye kufika mjini Ngudu pamoja na ule wa kutoka wilayani Magu ambao uko kwenye mchakato wa kumpata mhandisi mshauri wa kusanifu mradi huo, na kuongeza kuwa mradi wa maji wa mwamashimba kwa mwaka huu umetengewa shilingi milioni 500.

Mapema akizungumza na wananchi wa wilaya ya Kwimba wakati akifungua uwanja wa ndani wa michezo katika chuo cha maendeleo ya michezo Malya, rais  Kikwete amesema atahakikisha miradi yote miwili inatekelezwa kama alivyohaidi wananchi wakati wa kampeni ili kuondoa kero ya maji katika wilaya ya kwimba yenye wakazi zaidi ya laki mbili.

MABASI YA ABIRIA YAFUNGIWA NA SUMATRA

Mabasi 17 yatokayo Dar es Salaam kuelekea mikoa mbalimbali nchini yamefungiwa kusafirisha abiria baada ya kukutwa na makosa mbalimbali kuanzia Januari mpaka Agosti mwaka huu.
Ofisa Mfawidhi wa Sumatra, Kanda ya Mashariki,Conrad Shio alisema jana kuwa sababu za kufungiwa mabasi hayo ni pamoja na ubovu wake unaosababisha ajali.
“Mabasi hayo yalibainika kuwa na matatizo mengi, tuliwaonya sana,wamiliki wamekuwa na uzembe wa kutofanyia kazi maagizo tunayowaambia,” alisema Shio.
Akisita kutaja baadhi ya majina ya vigogo wanaomiliki mabasi hayo, Shio alisema si sahihi kutaja majina hayo kutokana na utaratibu waliowekewa.
“Wanajulikana lakini kwa sababu utaratibu tulionao ni kuhakikisha wanafanyia ukarabati mabasi hayo,” alisema.

WATAFITI AGUNDUA KAZI NYINGINE NYINGI BAADA YA KIFO CHA SHABAN ROBERT

Shaban Robert
Hakuna apingaye kuwa Shaban Robert alikuwa  manju wa fasihi ya Kiswahili, ambaye  hata baada ya miaka 50 tangu  kifo chake mwaka 1962, hakuna aliyejitokeza kumpiku kwa kiwango alichofikia katika fani ya fasihi.
Mpaka sasa kazi  zake nyingi bado zinaishi, huku zikiwa  zimetafsiriwa katika lugha mbalimbali na kusambazwa kote duniani.
Bila shaka, mtu huyu anabaki kuwa miongoni mwa watu  muhimu waliowahi kutokea nchini. Lakini inashangaza kuwa familia yake na hata historia yake vimetelekezwa!
Hata  mahala lilipo  kaburi lake katika kijiji cha Machui, Kusini mwa Jiji la Tanga, pameshindwa kuendelezwa japo kwa kuwa na makumbusho madogo ya mwanafasihi huyo aliyetamba ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.
Kimsingi, eneo hili mbali ya kuwa sehemu muhimu katika historia ya nchi, pia lingeweza kutumika kama  darasa la kuwakusanya watu, hasa watafiti na wanahistoria  kutoka  pembe zote za dunia. Ukitoa simulizi isiyovutia ya kusahauliwa kwa Shaban Robert, baada ya utafiti wa miaka mingi kuna habari mpya za kugunduliwa kwa kazi nyingine za gwiji huyo.
Kwa mujibu wa mwanafasihi bobezi nchini,  Profesa Mugyabuso Mulokozi,  aliyeshiriki katika utafiti huo, kazi hizi hazikuwahi kufahamika awali.
 Anasema katika  utafiti wao mpya wamegundua mafungu ya barua ambayo Shaabani Robert aliyaweka katika makundi ya nyaraka za kifamilia, kazi na ajira, pamoja na kiofisi.
 ‘’Baadhi ya barua zinahusu uhusiano kati ya mtu na kaka yake. Shaaban Robert alijipa jukumu la kulea, anazungumzia umuhimu wa mtu kutenda mema na umuhimu wa elimu katika dunia hii’’anabainisha.
 Pia anasema katika utafiti huo wamebaini makala za mashairi alizopeleka kwenye mashindano, na kuwa mashairi hayo bado  ni muswada yakisubiri kuchapishwa.
Miongoni mwa mambo yanayoibua maswali kwa wanafasihi wa sasa ni namna Shaaban Robert alivyoweza kuepuka misukosuko ya kisiasa, hasa enzi za ukoloni kwani baadhi ya  kazi  zake zipo zilizokuwa zikipinga unyanyasaji wa Waafrika.
Jambo hili pia limebainika katika utafiti huo mpya. Inadaiwa kuwa katika vita Kuu ya Pili ya Dunia(1939-1945), aliandika utenzi wa vita hiyo akiisifia Uingereza kuwa ilikuwa na haki dhidi ya dola ya Wajerumani.
 Utenzi huo haukuifurahisha Ujerumani na gwiji huyo wa fasihi ya lugha ya Kiswahili aliwekwa katika orodha ya watu watakaonyongwa endapo Wajerumani wangeshinda vita.
 Aidha,  kwa mujibu wa Profesa Mulokozi miongoni mwa kazi zilizogunduliwa, ni sehemu ya utenzi alioandika akilalamikia kuhamishwa vituo vya kazi  mara kwa mara.
Sehemu ya utenzi huo inanukuliwa ikisema:
’Nimezaliwa Tanga 1909, tangu utoto   sina kituo hasa, naona sina siasa ila kuandama njia’’
Mashairi mengine yanatajwa kuwa yanaelezea mila za watu wa Tanga.
 Katika kazi mpya zilizogunduliwa pia anazungumzia jinsi watu walivyoweza kupata tiba. Kwa mfano, anasema mtu alipougua alikwenda kwenye tambiko, msikitini kuombewa au hospitali.
 Akimzungumzia Shaaban Robert,  mwanafunzi wa Shahada ya Uzamili katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,  Felix Sosoo anasema kuwa alikuwa ni mtunzi aliyeheshimika na ametoa mchango mkubwa kuendeleza lugha ya Kiswahili.
 Mwanafunzi huyo kutoka Ghana anasema amefika nchini kujifunza zaidi lugha ya Kiswahili na baada ya masomo atarudi Chuo Kikuu cha Ghana kama mtaalamu wa lugha hiyo.
 Anasema anajivunia kusomea katika nchi anayosema ndiyo chimbuko la lugha ya Kiswahili na kuwa lugha hiyo ni utambulisho wa utamaduni wa Afrika. Matarajio yake ni kubobea na kuwa mtalaamu zaidi wa lugha hiyo.
 ‘’Nimetoka Ghana kujifunza Kiswahili ambayo ni kama lugha ya Afrika, hapa najifunza Kiswahili fasaha. Lugha hii itanirahisishia kujifunza lugha nyingine pia’’ anasema Sosoo
 Akitoa maoni yake kuhusu umahiri wa Shaaban Robert, msanii wa Kimataifa John Mugango, anasema mtunzi huyo ameacha somo kwa  Taifa kuendeleza    watu wake kulingana na vipaji walivyonavyo.
Anasema vipaji vingi vinapotea kwa kutoendelezwa na kuwa badala yake wanapatikana wataalamu wanaofanya kazi kwa shinikizo la kukosa ajira na siyo kwa sababu ya kupenda kazi husika.
 ‘’Tusomee vipaji vyetu, ukiona daktari anakukaripia baada ya kumfikisha mgonjwa hospitali, ujue huyo ana damu ya ajira katika kazi yake na siyo udaktari wa kujitambua’’anabainisha Mugango
 Naye Mwalimu Domician Domonick kutoka Shule ya Sekondari Bukoba, anashangaa gwiji huyo kutopewa shahada ya heshima na taifa, kama sehemu ya kutambua mchango wake katika kukuza lugha ya Kiswahili.
 Anasema Shaabani Robert ana mchango mkubwa katika kuifanya lugha hiyo iheshimike duniani. Analalamika kuwa hivi sasa Serikali inapitisha vitabu vya kufundishia lugha hiyo ambavyo maudhui yake ni dhaifu.
 Anasema vitabu vinavyotumika hivi sasa vingi havina mantiki ya fasihi na kwa vyovyote haviwezi kulinganishwa na vile vilivyotungwa na Shaaban Robert. Anarejea baadhi ya vitabu vyake kama vile  Mapenzi Bora kinachoonyesha  umuhimu wa elimu.
Ikbal Shaaban ambaye ni mtoto wa Shaaban Robert anasema kazi za baba yake hazijasaidia kuboresha maisha ya familia aliyoiacha.
 Anaeleza kuwa  wapo wajanja wanaofaidika na jasho la baba yao na kuwa hakuna pato linaloingia katika familia yao kutokana na mauzo ya kazi hizo.
 ‘’Bado hatujaona faida ya kazi zake zaidi ya kuitwa kwenye semina, kuna wajanja wanaonufaika na jasho lake,tuko mbioni kuanzisha vita mpya dhidi ya kazi za marehemu’’ analalamika.
 Ikbal anadai kuwa gwiji huyo wa lugha ya Kiswahili  hajapewa heshima ya kutosha na Taifa, licha ya kuwa kazi zake zinaendelea kutumika kuendeleza na kuitangaza lugha hiyo.
Kwa hali yoyote ile, huu  ni wakati wa kumuenzi Shaaban Robert kwa kutambua mchango wake kwa taifa, huku tukiendelea kuwaandaa wanafasihi wengine  wa baadaye. 
Mtoto  wa marehemu Shaaban Robert Ikbal Shaaban akiwa  katika moja ya makongamano ya kujadili mchango wa kazi za baba yake katika fasihi ya Kiswahili. (Picha na Phinias Bashaya)