Saturday, January 5, 2013

MONJA LISEKI ASAJILIWA MIEMBENI AKITOKEA MTIBWA SUGAR



Monja Privas Liseki 
MSHAMBULIAJI wa Mtibwa Sugar ya Morogoro, Monja Privas Liseki amejiunga na Miembeni ya Daraja la Kwanza Zanzibar kwa mkataba wa miaka miwili.
                                                
Monja yupo kwenye kikosi cha Miembeni FC kinachoshiriki Kombe la Mapinduzi visiwani hapa, ambayo leo usiku itamenyana na Azam FC, ikitoka kuifunga 4-1 Mtibwa Sugar katika mchezo wake wa kwanza wa Kundi B.

“Nipo hapa Miembeni, nadhani nitastaafu nikiwa na timu hii. Huku nimekuja kumalizia soka yangu nafikiri,”alisema

Monja alizaliwa Agosti 8, mwaka 1975, Kinondoni Muslim mjini Dar es Salaam na alipata elimu yake pekee, ya Msingi katika shule ya Muhimbili, Upanga mjini Dar es Salaam.

“Mimi nilikuwa napenda sana soka, nilipomaliza shule ya Msingi tu, nikaachana na shule kabisa nikaanza mitikasi ya soka hadi nikasajiliwa Sigara mwaka 1991 nikiwa bado mdogo sana nina miaka 16 tu,”alisema Monja.

Alicheza Sigara hadi mwaka 1996 iliposhushwa daraja, akahamia Simba SC ambako alidumu hadi mwaka 1998 alipotolewa kwa mkopo Yanga ili aichezee kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.

COASTAL UNION SARE NA MTIBWA SUGAR




COASTAL Union ya Tanga imelazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na Mtibwa Sugar ya Morogoro, katika mchezo wa Kundi B Kombe la Mapinduzi, jioni hii kwenye Uwanja wa Amaan visiwani Zanzibar.
 
Hadi mapumziko, hakuna timu iliyofanikiwa kuona lango la mwenzake na Coastal Union ndio walitakiwa kujilaumu kwa kushindwa kutumia mwanya wa Mtibwa Sugar kucheza pungufu kutokana na beki wake, Salum Swedi kutolewa nje kwa kadi nyekundu dakika ya 43.

Timu zilishambuliana kwa zamu katika kipindi hicho, upande wa Coastal ukiongozwa na Danny Lyanga na Mtibwa Hussein Javu.

Baada ya Swedi kutolewa nje kwa kadi nyekundu, kocha Mecky Mexime alimuinua beki Rajab Mohamed kwenda kuchukua nafasi ya mshambuliaji, Hassan Seif.

Kipindi cha pili, Mtibwa walirudi kwa kasi na kufanikiwa kupata bao la kuongoza dakika ya 58, mfungaji Ally Mohamed ‘Gaucho’ aliyepiga shuti la umbali wa mita 19 na kumtungua Juma Mpongo.

Coastal Union ilisawazisha bao hilo dakika ya 81, mfungaji Jerry Santo aliyefumua shuti la chini la umbali wa mita 24 na kumtungua kipa Hussein Sharrif.

Katika mchezo huo, kikosi cha Mtibwa Sugar kilikuwa; Hussein Sharrif, Hamisi Issa, Yussuf Nguya, Salvatory Ntebe, Salum Swedi, Babu Ally Seif, Ally Mohamed ‘Gaucho’, Rashid Gumbo, Hussein Javu, Hassan Seif/Rajab Mohamed dk43 na Vincent Barnabas.

Coastal Union; Juma Mpongo, Ismail Khamis, Othman Tamim, Philip Metusela, Mbwana Khamis ‘Kibacha’, Hamisi Shengo, Suleiman Kassim ‘Selembe’, Jerry Santo, Mohamed Miraj, Mohamed Soud Othman na Danny Lyanga. 

YANGA YATOKA SARE NA ARMINIA BIELEFELD YA UJERUMANI


Mchezo wa kirafiki kati ya timu ya Arminia Bielefeld kutoka Ujerumani, huko Uturuki, umemalizika kwa sare ya 1-1.

Taarifa ya Yanga katika ukurasa wa facebook wa klabu hiyo, Bao la Yanga lilifungwa katika dakika ya 60 na Tegete, akiunganisha pasi safi aliypewa na Saimon Msuva aliyewatoka walinzi wa Arminia Bielefeld.

Katika mchezo huo Athumani Iddi na Hamis Kiiza hawakuhusishwa katika mchezo huo baada yakutokuwa fiti kwa mchezo.

Kocha Mkuu wa Young Africans Ernest Brandts amesema amefurahishwa na kiwango walichokionyesha wachezaji wake na anaamini kadri siku zinavyokwenda wanazidi kuimarika na kuwa bora, hivyo katika michezo mingine wataendelea kuonyesha mabadiliko makubwa.

1.Ally Mustafa ‘Barthez’
2.Mbuyu Twite
3.Oscar Joshua
4.Nadir Haroub ‘Cannavaro’
5.Kelvin Yondani
6.Kabange Twite
7.Haruna Niyonzima
8.Frank Domayo
9.Said Bahanuzi
10.Didier Kavumbagu
11.David Luhende

Subs:
1.Said Mohamed
2.Shadrack Nsajigwa
3.Stephano Mwasika
4.Juma Abdul
5.Nurdin Bakari
6.Nizar Khalfani
7.Simon Msuva
8.George Banda
9.Jerson Tegete 

JAJI WARIOBA ATOA UFAFANUZI HOTUBA YA RAIS JK MWAKA MPYA




Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji Joseph Warioba ametoa ufafanuzi kuhusu hotuba ya Rais Jakaya Kikwete aliyoitoa usiku wa mwaka mpya na kuzungumzia mchakato wa Katiba unaoendelea na kusema Rais hapaswi kulalamikiwa kwani yote aliyosema yamo ndani ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.

Jaji Warioba Akitoa Ufafanuzi

Jaji Warioba alitoa ufafanuzi huo leo (Jumamosi, Januari 5, 2013) katika mkutano wake na Waandishi wa Habari wakati akizungumzia tathmini ya kazi ya kukusanya maoni binafsi ya wananchi kupitia mikutano iliyomalizika tarehe 19 Disemba mwaka jana (2012).

“Kuna kitu gani kipya alichosema Rais? Yote aliyosema yapo kwenye Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na mimi katika mikutano yangu yote nanyi nimeyaeleza na hakuna asiyejua,” alisema Jaji Warioba ambaye ameshawahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Waziri Mkuu na Makamu wa Rais.

“Rais alielezea mchakato wote kuanzia kukusanya maoni, kuandaa rasimu, kufanyika kwa Mabaraza ya Katiba, Bunge Maalum la Katiba na kura ya maoni…haya yote yapo kwenye sheria ambayo Wabunge waliipitisha,” alisema Jaji Warioba wakati akijibu swali la Mwandishi wa Habari Jabir Idrissa aliyetaka kujua kauli ya Tume kuhusu maoni ya baadhi ya wanasiasa kuwa Rais aliingilia kazi za Tume.

“Hivi ingekuwaje kama Rais angetoa salam za Mwaka Mpya bila kuzungumzia mchakato muhimu kwa nchi kama huu wa Katiba,” alihoji Jaji Warioba.

Akizungumzia mikutano ya kukusanya maoni iliyomalizika mwezi uliopita, Jaji Warioba alisema kazi ya kukusanya maoni ilianza tarehe 2 Julai mwaka jana na Tume yake imetembelea na kufanya mikutano 1,776 katika mikoa yote 30 ya Tanzania Bara na Zanzibar.

Kwa mujibu wa Jaji Warioba, jumla ya wananchi 1,365,337 walihudhuria mikutano hiyo na kati yao, wananchi 64,737 walitoa maoni kwa kuzungumza katika mikutano na wengine 253,486 walitoa maoni yao kwa maandishi katika mikutano hiyo.

Kwa mujibu wa maelezo ya Jaji Warioba, takwimu hizi hazijumuishi maoni yanayoendelea kukusanywa na Tume yake kupitia posta, totuvi ya Tume, mitandao ya kijamii na ujumbe mfupi wa simu za mkononi ambao hadi kufikia jana (Ijumaa, Januari 4, 2013) jumla ya ‘sms’ 16,261.

Kuhusu idadi ya wananchi waliojitokeza mikutanoni na kutoa maoni yao, Mwenyekiti huyo alisema Tume imeridhika na idadi hiyo na kufafanua kuwa kilichokuwa kinatafutwa na Tume ni hoja na kwamba haukuwa wakati wa kupiga kura.

“Ilikuwa ni muhimu kufikia watu wengi iwezekanavyo na ndiyo maana tumefika kila sehemu. Lakini tangu awali, tulishasema hatutaweza kumfikia kila mtu,” alisema na kuongeza kuwa Tume yake imeridhika na idadi na maoni yaliyotolewa na wananchi na kutoa mfano wa Tume ya Nyalali ambayo alisema ilipokea maoni ya wananchi 21,000 lakini Ripoti ya Tume hiyo ilisheheni mambo muhimu kwa taifa.

Jaji Warioba alifafanua kuwa katika awamu zote nne za mikutano ya kukusanya maoni, wananchi wametoa maoni kuhusu maeneo yote muhimu kama utawala, haki, maadili na mamlaka yao na mengineyo.

Aliongeza kuwa mikutano ya Tume ya kukusanya maoni ililelenga kupata hoja za msingi ili Tume iweze kuandaa Rasimu ya Katiba ambayo itawasilishwa katika mikutano ya Mabaraza ya katiba itakayofanyika kila wilaya.

Akizungumzia hatua inayofuata, Jaji Warioba alisema kuwa kuanzia keshokutwa (Jumatatu, tarehe 7 Januari, 2013), Tume hiyo itaanza kukutana na makundi mbalimbali kwa lengo la kukusanya maoni yao kuhusu Katiba Mpya. Makundi hayo ni Vyama vya Siasa; Vyama vya Kitaaluma; Asasi za Kiraia; Taasisi za Kidini, Vyama vya Wafanyakazi, Wakulima na Wafanyabiashara na makundi mengine mbalimbali.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo, Tume yake imeshawasiliana na makundi hayo na imeandaa utaratibu wa kukutana na wawakilishi wao katika ofisi za Tume na baadhi ya kumbi jijini Dar es Salaam na Zanzibar.

Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilianza kazi rasmi Mei 2 mwaka jana (2012) na kazi ya kukusanya maoni kupitia mikutano imefanyakika kwa awamu nne. Awamu ya kwanza ilifanyika kati ya Julai 2 – 30, 2012 wakati awamu ya pili ilifanyika kuanzia tarehe 27 Agosti – 28 Septemba, 2012. Awamu ya tatu iliyofanyika kati ya terehe 8 Oktoba, 2012 na tarehe 6 Novemba, 2012 na awamu ya nne na ya mwisho ilifanyika kati ya tarehe 19 Novemba – 19 Disemba mwaka jana (2012).

Friday, January 4, 2013

WATATU WAFA AJALINI ARUSHA

ARUSHA

Watu watatu wamefariki hapo hapo baada ya gari walimokuwa wanasafiria aina ya Fuso lenye namba T 526 AVZ kupinduka eneo la kilimatembo wilayani Karatu na dereva kujeruhiwa vibaya wakati wakitokea Serengeti Moa wa Mara kwenda Arusha.

Akizungumza na wanahabari ofisini kwake Kamanda wa jeshi la polisi mkoani hapa Liberatus Sabas aliwataja waliokufa kuwa ni Peter Herman 40 ,Ramadhani Hamza 45 na Peter Kimaro 40 ,wote ni wakazi wa mkoa wa Arusha. Kamanda Sabas alimtaja pia Dereva wa gari hilo Ombeni Urassa kuwa alipata majeruhi kwenye ajali hiyo na anaendelea kupatiwa matibabu kwenye hospitali ya Selian iliyopo jijini hapa.
 
Kamanda wa polisi Liberatus Sabas
Sabas alisema kuwa chanzo cha ajali hakijajulikana na ajali hiyo ilitokea kwenye mteremko wa kilimatembo na lilikuwa likitokea wilyani Serengeti kuja wilaya ya Meru mkoani hapa huku akisema kuwa jeshi la polisi mkoani hapa linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo.

Wakati huo huo jeshi la polisi mkoani hapa limetoa pongezi kwa wananchi mkoani hapa kwa kutoa ushirikiano kwenye ulinzi shirikishi wakati wote wa kipindi cha sikukuu na kuwataka kuendelea kutoa ushirikiano katika kupambana na vitendo vya uhalifu kwenye maeneo ya yao.

Kamanda Sabas alisema kuwa wananchi walisherekea sikukuu za mwisho wa mwaka bila ya matukio ya kutisha na kuwa hakukuwa na wimbi la uhalifu wa kutishia amani ya wananchi na usalama wa mali zao.

RAIS KIKWETE AKUTANA NA MSHAURI WA KIJESHI WA UN



Rais Jakaya Mrisho Kikwete akipeana mikono na Mshauri Mkuu wa Kijeshi wa Umoja wa Mataifa Luteni Generali Babacar Gaye baada ya kuonana naye Ikulu jijini Dar es salaam leo Januari 4, 2013.Kushoto Mbele ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mhe Mahadhi Mahadhi Juma Maalim, akifuatiwa na Mkuu wa Majeshi Tanzania  Jenerali Davis Mwamunyange, na wa pili kulia ni Balozi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa Balozi Tuvako Manongi na wengine ni maafisa waandamizi katika JWTZ na Umoja wa mataifa.


Rais Jakaya Mrisho Kikwete katika picha ya pamoja  na Mshauri Mkuu wa Kijeshi wa Umoja wa Mataifa Luteni Generali Babacar Gaye baada ya kuonana naye Ikulu jijini Dar es salaam leo Januari 4, 2013.Kushoto Mbele ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mhe Mahadhi Juma Maalim, akifuatiwa na Mkuu wa Majeshi Tanzania Jenerali Davis Mwamunyange, na wa pili kulia ni Balozi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa Balozi Tuvako Manongi na wengine ni maafisa waandamizi katika JWTZ na Umoja wa mataifa.


Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiwa  na Mshauri Mkuu wa Kijeshi wa Umoja wa Mataifa Luteni Generali Babacar Gaye baada ya kuonana naye Ikulu jijini Dar es salaam leo Januari 4, 2013.Kushoto ni  Mkuu wa Majeshi Tanzania Jenerali Davis Mwamunyange.

PICHA NA IKULU YA TANZANIA

BOKO HARAM WAFANYA MAUAJI NIGERIA


MAIDUGURI

Watu 13 wameuawa Kaskazini Mashariki mwa Nigeria wakati wa makabiliano ya siku mbili na Waasi wa Kundi la Kiislamu lenye Msimamo Mkali la Boko Haram

Polisi nchini Nigeria imesema mapema leo kuwa Askari aliyekuwa na Bunduki aliingia siku ya Jumatano aliingia katika Mji wa Marte ulio jangwani usiofikika kirahisi karibu na mipaka ya Cameroon na Chad akiwa na miripuko na kuzua hofu kubwa. Jeshi la Serikali limekabiliana  kwa siku mbili mfululizo katika mji huo ulio umbali wa kilometa 100 kutoka Maiduguri na kwamba miripuko hiyo ilikuwa rasmi kwa ajili ya maafisa wa Serikali na Ofisi za Polisi za Adamawa. Itakumbukwa kwamba watu akali ya 50 wameuawa katika eneo hilo lenye utajiri wa mafuta nchini Nigeria na wanamgambo wa Boko Haram wenye mafungamano na Al Qaeda.Jamā'atu Ahlis Sunnah Lādda'awatih wal-Jihad  hujulikana zaidi kama Boko Haram kwa lugha ya Kihausa ambapo watu 3000 wameuawa miaka 3 iliyopita na kundi hilo.

Wednesday, January 2, 2013

QUEEN DARLEEN AFUNGUKA

Queen Darlin

MSANII na STAA anayefanya poa na ngoma ‘Kokoro’, Queen Darleen, ameuambia mtandao huu kuwa anajisikia raha kuwa na marafiki wengi wa kiume kuliko wanawake, huku akiamini kuwa tabia za baadhi ya wanawake ndizo zinazomfanya awe hivyo. 

Msanii huyo ni mmoja ya wanawake wenye staili za kipekee kabisa kwenye game ingawa ndani ya mwaka huu amekuja kivingine kabisa baada ya kuwa kimya kwa muda na kuteka mashabiki kupitia kibao cha ‘Maneno Maneno’. 

Kauli ya msanii huyo imekuja baada ya kuzungumza na mwandishi wetu alietaka kujua ni kundi gani la watu ambao hupenda kuwa nao karibu sana na kubandilishana mawazo ndipo yenye maana, ndipo alipofunguka kuwa mara nyingi huwa karibu na wanaume na si wanawake. 

Alisema kuwa karibu na wanaume haimanishi kwamba ni mabwana zake hapana bali anaona ni watu ambao anaendana nao ingawa tabia zake si za kiume kama baadhi ya watu wanavyopenda kudhani kutoka na staili zake au aina ya kazi anazofanya. 

“Kuna watu wanajua mimi nina tabia za kiume hiyo inawezekana kwa sababu wao ndo wanaosema, napenda sana kuwa na watu ambao tutafanya mambo ya maendeleo na si kuzungumza mapenzi na upuuzi muda wote hiyo ndo sababu kubwa inayonifanya nijiweke sana kwa wanaume,” alisema. 

Hata hivyo aliongeza kuwa anahisi akijiweka karibu sana na wanawake hakuna kitu kikubwa watakachokuwa wanazungumza zaidi ya majungu na mapenzi, ingawa hata wanaume baadhi yao wako hivyo ila si kama wanawake ambao hupoteza mda mwingi kujadili ujinga.

Rais Jakaya Kikwete amtolea Sajuki Rambirambi

Rais wa jamuhuri ya muungano wa tanzania Dr.Jakaya Mrisho Kikwete

Rais Dk. Jakaya Kikwete amemtumia Salamu za Rambirambi Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara kufuatia kifo cha msanii maarufu wa kujitegemea hapa nchini, Juma Kilowoko maarufu kwa jina la kisanii la Sajuki, kilichotokea usiku wa kuamkia tarehe 2 Januari, 2013 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili alikokuwa amelazwa kwa matibabu.


Enzi za uhai wake, Marehemu Juma Kilowoko alianza kujishughulisha na Tasnia ya Sanaa kwa kujiunga na kundi maarufu la sanaa la Kaole kabla ya kufanya uamuzi wa kuwa msanii wa kujitegemea ambapo aliendelea kupata umaarufu katika tasnia ya michezo ya kuigiza na filamu na kufanikiwa kutengeneza filamu nyingi.

Baada ya kuanza kuugua mwaka 2010, Marehemu Kilowoko aliwahi kupatiwa matibabu nchini India mwaka 2011 na kurejea akiwa amepata nafuu kubwa kiasi cha kumwezesha kutengeneza filamu nyingine, lakini alianza kuugua tena hadi mauti yalipomkuta.

Taarifa iliyotolewa na Ikulu jijini Dar es salaam, leo, imemkariri Rais Kikwete akisema kuwa amesikitishwa na kuhuzunishwa mno na kifo cha Msanii Juma Kilowoko ambaye ametoa mchango mkubwa katika kuinua kiwango cha sanaa hususan michezo ya kuigiza na filamu hapa nchini.

"Kwa hakika kifo cha msanii huyu ni pigo kubwa kwa Tasnia ya Michezo ya Kuigiza na Filamu ambayo inaendelea kujizolea umaarufu mkubwa miongoni mwa Watanzania”, amesema Rais Kikwete katika Salamu hizo za Rambirambi.

“Kutokana na msiba huu mkubwa, nakuomba wewe Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara unifikishie salamu zangu za rambirambi na pole nyingi kwa Familia ya Marehemu Juma Kilowoko kwa kuondokewa na Kiongozi na Baba wa Familia.

“Natambua uchungu ilio nao Familia ya Marehemu Kilowoko, lakini nawahakikishia kwamba binafsi niko pamoja nao katika kuomboleza kifo cha mpendwa wao. Nawaomba wawe na moyo wa uvumilivu, ujasiri na subira katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo.  Namuomba  Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema aipokee na kuilaza mahala pema peponi roho ya marehemu Juma Kilowoko, Amina”.

Aidha Rais Kikwete ametoa pole kwa wasanii wote nchini hususan wanaojishughulisha na masuala ya michezo ya kuigiza na filamu kwa kumpoteza mwenzao na hivyo kuleta simanzi na huzuni kubwa miongoni mwao.  Hata hivyo amewataka kuwa wavumilivu na kuchukulia kifo hiki kama changamoto kwao katika kuendeleza tasnia ya michezo ya kuigiza na filamu hapa nchini.

Dr. Fenella Mukangara atuma salamu za rambirambi kwa ndugu, jamaa na marafiki wa Sajiki


Waziri wa Habari, Vijana , Utamaduni na Michezo Dkt. Fenella Mukangara amewatumia salamu za rambirambi, ndugu, jamaa na wasanii wote nchini kufuatia kifo cha msanii Juma Kilowoko (SAJUKI)kilichotokea usiku wa kuamkia tarehe 02/01/2013 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Taarifa iliyotolewa leo, jijini Dar es salaam ,Wizara ya Habari, Vijana na Utamauni na Michezo imepokea kwa masikitiko na huzuni kubwa taarifa za kifo cha msanii huyo na kuongeza kuwa kifo hicho ni pigo katika tasnia ya filamu hapa nchini.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo Kifo chake ni pengo kubwa kwa Serikali, wadau wa tasnia ya filamu na michezo ya kuigiza nchini kwa ujumla.
Juma Kilowoko (Sajuki)

Dkt. Mukungara amewataka ndugu, jamii na wasanii wote kuwa wavumilivu na watumilivu wakati wote wa msiba na kumuombea marehemu makao mema kwa Mwenyezi Mungu.

Juma Kilowoko (SAJUKI)ni mzaliwa wa mkoa wa Ruvuma. Sajuki alianza kujihusisha na masuala ya maigizo alipojiunga na kikundi cha Kaole na baadaye filamu. Filamu alizocheza ni pamoja na Revenge ya Kampuni ya RJ. Mwaka 2008 aliamua kuanza kutengeneza kazi zake mwenyewe ambapo filamu yake ya kwanza iitwayo Two Brothers kwa kushirikiana na Shija Deogratious ilitoka. Sajuki baadaye aliamua kuanzisha kampuni yake iitwayo WAJEY Production Company ambapo alitengeneza filamu nyingi zikiwemo Mboni Yangu, Round, Briefcase , Kijacho, Kozopata, Mchanga na Keni, 077( Zero Seven Seven).nk. Sajuki alifanikiwa kucheza michezo ya kuigiza na filamu na wasanii wengi wenye majina hapa nchini. Sajuki amebobea katika Uigizaji, Utayarishaji na Uongozaji wa filamu.

Sajuki alianza kuugua mwaka 2010 na hali ilizidi kudhoofu mwaka 2011,ambapo alikwenda kutibiwa nchini India. Wadau wengi wa tasnia ya filamu walifanikiwa kutoa michango mbalimbali iliyomwezesha Sajuki kupata matibabu yake. Alirudi na kuonekana kapata nafuu kidogo jambo ambalo lilileta matumaini na furaha kwa watanzania; aliporejea tu aliweza kutoa filamu iitwayo Kivuli huku filamu nyingine ikiwa katika hatua ya utengenezaji.

Aidha hali yake ilibadilika jambo lililolazimu alazwe katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili hadi umauti ulipomkuta usiku wa kuamkia tarehe 02/01/2013.

Mungu ailaze roho ya Marehemu mahali pema peponi Amen.
Imetolewa na:
Mkurugenzi 

Idara ya Habari(MAELEZO). 
Dar es Salaam. 
Sajuki na Mkewe (Wastara)     [Picha Na Global publishers]
2 Januari 2013

SERIKALI YATOA UFAFANUZI JUU YA MAANDAMANO YA WANACHI WA MTWARA


 Serikali imelitolea ufafanuzi sakata la wananchi wa mkoa wa Mtwara walioandamana mwishoni mwa mwaka jana wakitaka kupewa kipaumbele katika uchimbaji wa gesi iliyogundulika katika kina kirefu cha Bahari, ikiwajulisha kuwa gesi hiyo ni mali ya watanzania wote.


Waziri mwenye dhamana ya Nishati na madini Prof. Sospeter Muhongo amelazimika kujitokeza mbele ya waandishi wa habari na kufafanua juu ya gas iliyopo pamoja na matumizi yake katika maendeleo ya kiuchumi ya nchi.

Katika sheria za nchi mipaka ya kiutawala katika kila mkoa haipaswi kuvuka umbali wa kilomita 22. ambapo Gas asilia imeonekana kwenda umbali zaidi ya huo na kugundulika kuwapo kwa asilimia 78 ukilinganisha na iliyopo mkoa wa Mtwara asilimia 14, Lindi 7% pamoja na Pwani 1%.

Prof. Muhongo anasema kuwa wananchi wa mkoa wa Mtwara mjini walioandamana hawana uwelewa kuwa gesi hiyo sio ya Mtwara na bila kuuma maneno akabainisha kuwa maandamano yao yalishinikizwa na vyama vya upinzani.

Desemba 27 mwaka jana wananchii wa Mtwara mjini waliandamana kwa madai ya kile walichodai kutokupewa kipaumbele kutokana na upatikanaji wa gas hiyo kupelekwa Jijini Dar Es Salaam kwa ajili ya kusambazwa.

Prf.Muhongo Ameongeza kuwa suala la kujenga mabomba ya Gas na kuyaleta Jijini Dar es salaam ni la msingi kutokana na asilimia 80 ya uzalisha na ongezeko la pato la nchi unatoka Jijini humo, hivyo wananchi wanapaswa kulifaham hilo.

Mpaka kufikia sasa, viwanda 34 vya Jijini Dar es Salaam tayari vimeanza kutumia nishati ya gas asilia ya songosongo kwa ajili ya uzalishaji ambavyo kwa kiasi kikubwa vimefungua milango ya ajira pamoja na kuongeza pato la nchi.

Monday, December 31, 2012

KUZIMWA KWA MITAMBO YA ANALOJIA NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO JANUARY MAKAMBA ATOA TAARIFA KWA UMMA.


Ndugu Wananchi,
 Mtakumbuka kuwa hapo tarehe 23 Februari 2012 tuliwatangazia kupitia vyombo vya habari juu ya usitishwaji wa matangazo ya televisheni kwa kutumia teknolojia ya analojia kwenda katika mfumo mpya unaotumia teknolojia ya dijitali.
Napenda kuwaleleza kuwa, maandalizi ya kuzima mitambo ya analojia kuanzia tarehe 31 Desemba 2012 yamekamilika kwa mujibu wa makubaliano ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Hata hivyo, napenda sasa kutoa taarifa kuwa uzimaji wa mitambo ya analojia utafanyika kwa awamu kama ifuatavyo:-
    (1) Dar Es Salaam-31 Desemba, 2012;
    (2) Dodoma & Tanga- 31 Januari, 2013;
    (3) Mwanza-28 Februari, 2013;
    (4) Moshi & Arusha-31 Machi, 2013;
    (5) Mbeya-30 Aprili, 2013.
 Tumeamua kuanza kuzima mitambo hiyo kwa Jiji la Dar es Salaam kwanza ili kutoa fursa kwa makampuni yenye leseni kusimika mitambo ya utangazaji wa dijitali katika mikoa mingine. Makampuni haya yamejipanga kukamilisha usimikaji wa mitambo hiyo katika mikoa minane katika miezi minane ijayo.
Mitambo ya analojia itakayozimwa kesho ni ile iliyopo Kisarawe na Makongo. Vituo ambavyo siku ya tarehe 1 Januari 2013, vitapaswa kuanza kutangaza matangazo kwa mfumo wa dijitali ni TBC1, ITV, EATV, Channel 10, StarTV, DTV, CapitalTV, TumainiTV, ATN, MlimaniTV, C2C, CTN, CloudsTV na Efatha.
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inafanya jitihada za kutosha kuhakikisha kwamba makampuni yenye leseni za kusambaza ving’amuzi yanakuwa na ving’amuzi vya kutosha na vingine vimeagizwa ili kukidhi mahitaji ya baadaye na vile vilivyopo sokoni vina ubora unaokubalika.
Vilevile, Serikali kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania itahakikisha kwamba zoezi la uhamaji linafanyika bila usumbufu na kero kwa wananchi. Makampuni yanayouza ving’amuzi yameagizwa yaimarishe huduma kwa wateja wakati wa kuuza ving’amuzi na hata baada ya ununuzi iwapo wananchi watakuwa na matatizo na ving’amuzi.
  
Zoezi hili la uhamaji ni muhimu sana kwa maendeleo ya nchi yetu. Tutakapokuwa tumekamilisha uhamaji, huduma za mawasiliano na utangazaji zitapanuka na kuwa bora zaidi. Kwa mfano, itawezekana sasa kuangalia televisheni kupitia simu zetu za mikononi. Vilevile, itawezekana, kwa bei nafuu kabisa, kwa mtu mwenye uwezo wa kutengeneza vipindi kukodisha chaneli yake na kutangaza vipindi vyake. Vilevile, bei za mawasiliano na utangazaji zitashuka, na tutakuwa tumepiga hatua kubwa kwenye mapinduzi ya teknolojia duniani, ambayo nchi yetu haiwezi kubaki nyuma.
Ndugu Wananchi,
Serikali kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania itaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu uhamaji huu. Serikali inatarajia kupata ushirikiano wa karibu kutoka kwa wadau wa sekta ya utangazaji na wananchi kwa ujumla katika kipindi cha uzimaji wa mitambo ya utangazaji wa televisheni ili kufanikisha zoezi la uzimaji wa mitambo ya utangazaji ya teknolojia ya analojia.
Uhamaji huu hautahusu televisheni za wananchi zinazopata matangazo kupitia madishi (nyungo) (satellite) au nyaya (cables). Hivyo, wananchi wanaopata matangazo kupitia DStv, Zuku, na nyinginezo wataendelea kupata matangazo yao kama kawaida.
Ndugu Wananchi
Naibu waziri wa nishati na nadini
Kama kuna mwananchi yoyote ana kero, malalamiko, swali au anahitaji maelekezo kuhusu uhamaji, awasiliane na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kupitia namba 0784-558270; 0784558271 au barua pepe: malalamiko@tcra.go.tz
  
Ndugu Wananchi,
Nawashukuru kwa kunisikiliza.

MPAMBANO WA MASUMBWI KUPIGWA Janual 27 katika ukumbi wa CCM Tandare

SUPER D BOXING COACH AKIMWELEKEZA KING CLASS MAWE

Mabondia Hassan Mandulla na Jems Martin wanatarajia kupanda ulingoni Janual 27 katika ukumbi wa wa CCM Tandare Dar es salaam akizungumza mpambano huo mwandaaji Waziri Rosta 
amesema kutakuwa na mapambano mengine ya utangulizi yakiwemo ya mabondia maarufu na chipkizi alisema mapambano ya utangulizi ni Fadhiri Majia na Anton Matiasi mpambano mwingine

Utawakutanisha Shabani Kilumbelumbe na Mwaite Juma na Chaeles Mashali atavaana na Adam Ngange, Julias Noro atapambana na Abdallah Luwaje mpambano mwingine utawakutanisha Rajabu Tumaini na Daudi Anton na Rashid Mohamed Atavaana na Eliman Richard wakati Rashid Hamisi atamvaa Omary Shabani

Super D, alisema katika mpambano huo atasambaza DVD zake mpya tofauti na kanda yake ya awali iliyokwenda kwa SUPER D BOXING COACH, DVD za sasa zimeandaliwa kisasa na zikiwa na mchanganyiko wa ‘clips’ za michezo ya nyota wa Dunia katika kuwafunza watu namna ya kupigana ngumi.Super D, alisema mbali na michezo ya nyota hao wa Dunia akiwemo Manny Pacquio,Juan Emanuel Marquez, Floyd Maywether, Roy Jones na wakali wengine DVD hizo zina.

 michezo
ya tamasha lao la ngumi wanaloendesha kwa kushirikiana na kocha mkongwe Habibi Kinyogoli.”katika muendelezo wa kuwafunza watu ngumi kwa njia rahisi, nimetoa dvd pamoja na CD nyingine tofauti zilizokusanya michezo ya mabingwa wa dunia na mafunzo ya ngumi tunayoendesha kupitia tamasha letu na Kinyogoli Foundition ” alisema.

 Super D ambae ni kocha wa timu ya ngumi ya Ashanti pamoja na timu ya mkoa wa Ilala kimichezo alisema anamini kupitia njia  hii watu wengi wenye kupenda kujifunza mchezo wa ngumi kwa kuangalia mbinu na ufundi katika mchezo huo kupitia michezo ya mabondia waliopo kwenye dvd hizo. 

 
Aliongeza kuwa, mbali na dvd hizo bado wanaitajika vijana wenye vipaji kujitokeza kuja kushiriki katika mazoezi ya ngumi ili wajiunge na wenzao wa
timu ya Ashanti na Amana kujifunza ‘live’ chini ya makocha Habibu Kinyogoli, Kondo Nassoro, na yeye mwenyewe Super D na wengine wanaowanoa vijana.