Saturday, October 5, 2013

MAMA'KE LULU ASEMA KUHUSU KANUMBA

Mama lulu atoboa siri za kanumba, aelezea mengine mengi zaidi!
Lucresia Karugila
Mama wa staa wa filamu za Kibongo, Elizabeth Michael ‘Lulu’, Lucresia Karugila kwa mara ya kwanza amemfungukia marehemu Steven Kanumba aliyefariki dunia Aprili 7, 2012. Mahojiano hayo yamefanywa hivi karibuni na gazeti la Risasi linalotolewa na kampuni ya GPL.
Ifuatayo ni habari hii kama ilivyoripotiwa na mwandishi wa gazeti hilo:-
Katika mahojiano rasmi na Risasi Jumamosi, juzi jijini Dar, Mama Lulu aliweka wazi kila kitu kuhusu madai mbalimbali ya yeye na mama Kanumba, Lulu na marehemu Kanumba.
Mambo yaliyoelekezwa ayajibu mwanamama huyo ni pamoja na madai kwamba alishapokea barua ya posa ya Kanumba kutaka kumuoa Lulu, yeye na mama Kanumba kugombana hivi karibuni na Lulu kumjali zaidi mama Kanumba kuliko yeye.
Awali, mwanamke huyo alisema miongoni mwa watu waliofiwa na Kanumba yeye yupo mstari wa mbele kwani uchungu alioupata siku ya tukio mpaka leo haujamtoka.
Mahojiano kamili yalikuwa kama ifuatavyo:
Risasi: Mama kuna madai kadhaa ambayo ni vyema uyajibu.
Mama Lulu: (Kwa ukali kidogo) maswali gani? Mimi sitaki waandishi, nilishasema! Kama ni kuhusu Lulu muulizeni mwenyewe.
Ilibidi waandishi watumie kazi ya ziada ili mama huyo aweze kuzungumza.
Risasi: Ni mambo ya kawaida tu mama, wewe ndiyo unafaa kujibu, tafadhali tusikilize.
Mama Lulu: Haya, ulizeni.

ALIUJUA UHUSIANO WA KANUMBA NA LULU?
Risasi: Kuna madai kwamba uliujua uhusiano wa kimapenzi kati ya Lulu na Kanumba,  lakini mama Kanumba alikuwa hajui kinachoendelea, ni kweli?
Mama Lulu: Kwanza katika maisha yangu hakuna siku niliyowahi kupata mshtuko kama niliposikia Kanumba amefariki dunia na mwanangu Lulu kahusishwa na kifo kile, nilishtuka sana.
“Ilikuwa mara yangu ya kwanza kujua kumbe Kanumba alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanangu Lulu, lakini kabla ya hapo sikuwa najua lolote.
ALIMKABIDHI LULU KWA KANUMBA?
“Ninachoweza kukiweka wazi ni kwamba, nilikutana na Kanumba nikamkabidhi mwanangu kwa moyo mweupe amlee kisanii kwa sababu nilijua anaweza, kumbe na wao wakaanzisha uhusiano huo kwa siri.
KWA NINI ALIMKABIDHI LULU KWA KANUMBA?
 “Mimi na Kanumba tulikuwa tumezoeana sana. Alinipa heshima zote kama mama yake na alikuwa kijana mwenye aibu kwangu kutokana na heshima, haikuwa rahisi kuangaliana machoni na ndiyo maana niliamua kumpa Lulu amkuze kisanii.
ALIPOKEA BARUA YA POSA YA KANUMBA?
“Si kweli, sijawahi kuona wala kupokea barua ya posa ya Kanumba kumchumbia Lulu.
KAMA KANUMBA ANGETAKA KUMUOA LULU?
“Lakini nataka kusema kwamba kama Kanumba angekuwa hai na angetaka kumuoa Lulu ningefurahi sana kwani naamini mpaka sasa wangekuwa wamepata mtoto mzuri na sisi wazazi tukaitwa bibi.”
MADAI YA KUGOMBANA NA MAMA KANUMBA?
Risasi: Kuna madai kwamba wewe na mama Kanumba kwa sasa ni paka na panya, na sababu kubwa ni Lulu kumjali zaidi mwanamke huyo kuliko wewe, ni kweli habari hizi?
Mama Lulu: Mimi na mama Kanumba hatuwezi kugombana hata siku moja. Kwanza Lulu nimempa jukumu kwamba kwa sababu wote ni mama zake, akinunua nyama kilo tano kwa ajili yangu na kwa mama Kanumba apeleke tano.
“Akinunua vocha ya elfu tano kwangu na mama Kanumba amtumie kama hiyohiyo. Kwa hiyo hakuna ugomvi.”
Risasi: Je, Lulu akimzidishia mama Kanumba wewe hutajisikia vibaya?
Mama Lulu: Siwezi kujisikia vibaya ingawa mimi kwa sababu naishi naye ni lazima nitapata zaidi, lakini akimsaidia naona ni sawa tu.

ALIKUWA AKIMUOGOPA MAMA KANUMBA?
Mwandishi: Ilikuwaje ukakutana na mama Kanumba kwa mara ya kwanza?
Mama Lulu: Lulu ndiye aliyekuwa akinishawishi kila mara niende nikaonane na mama Kanumba ingawa wakati mwanangu yuko jela kiukweli nilikuwa namuogopa sana.
“Unajua yule aliyepotea (Kanumba) ni mtoto kama wangu, lakini alipotoka tulikwenda nyumbani kwake na tunamshukuru alitupokea vizuri. Awali kabla ya kifo cha Kanumba sikuwahi kufahamiana naye.
Risasi: Ukiambiwa uongee na Watanzania utataka kuwaambia nini?
Mama Lulu: Cha kuwaambia ni kwamba, mimi na mama Kanumba si marafiki bali ni mtu na dada yake. Nawaomba wawaombee mama Kanumba na Lulu mwenyewe ili waendelee kupatana na kufanya kazi za sanaa pamoja kama walivyoanza.
Risasi: Tunashukuru sana mama.
Mama Lulu: Karibuni sana, mimi huwa naogopa sana magazeti, sipendi sana kuongea na waandishi wa habari.
KUMBUKUMBU YA LULU
Katika mahojiano na kipindi cha Take One kinachorushwa na Clouds TV, Lulu alisema: “Katika maisha yangu sitakaa nimsahau Kanumba kwa sababu alikuwa ni zaidi ya mpenzi. Kamwe sitamsahau.”

MKUU WA UPELELEZI KUTOA USHAHIDI KUHUSU MADAWA YA KULEVYA

Aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi  wa Polisi mkoani Mbeya, Anaclet Malindisa ambaye sasa hafanyi kazi hiyo, Jumatatu ijayo anatarajiwa kutoa ushahidi wa kesi  ya kusafirisha kilo 34 za  dawa za kulevya  zenye thamani ya Sh1 bilioni  inayowakabili  raia wawili wa Afrika Kusini, Vuyo Jack na Anastazia Cloet.
Washtakiwa hao wanadaiwa kukamatwa Novemba 18, 2010 eneo la Tunduma wakisafirisha dawa hizo kwa kutumia gari  namba   CA 508650, ambapo walifunguliwa kesi  ya makosa ya kusafirisha dawa za kulevya kinyume na sheria za nchi.
Kesi yao ilianza kusikilizwa tangu mwishoni mwa mwezi uliopita na inaendelea mfululizo jijini hapa.
Tayari mashahidi wanne kati ya wanane, wameshatoa ushahidi wao, na kwa mujibu wa Msajili wa Mahakama Mbeya, Aaron Lyamuya, shahidi Malindisa anatarajiwa kutoa ushahidi wake Jumatatu akiongozwa na mawakili wa upande wa mashtaka..
Upande wa mashtaka unasimamiwa na mawakili wa Serikali, Edwin Kakolaki na Basilius Namkambe, wakati washtakiwa wanatetewa na  mawakili Ladslaus Rwekaza na Mary Gatuna.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Mbeya, Noel Choja aliahirisha kesi hiyo, Alhamisi iliyopita  hadi Jumatatu akisisitiza umuhimu wa kuzingatia muda wakati wote wa kesi hiyo, ambayo ni kubwa kuliko kesi nyingi zilizowahi kufanyika mkoani hapa kuhusu dawa za kulevya.

AJALI MBAYA MLIMA KITONGA - IRINGA


Ajali mbaya  nyingine  imetokea  usiku  huu katika mlima kwa Kitonga wilaya ya Kilolo mkoani Iringa katika barabara  kuu ya Dar es Salaam -Iringa . 
Katika  ajali  hiyo  watu  wawili wamekufa papo hapo huku wa wawili  wakijeruhiwa  vibaya baada ya malori mawili kugongana  uso kwa uso . 
Ajali  hiyo imetokea  mida ya saa 12.50 jioni ya  leo  ikiwa ni dakika takribani 30  baada ya ajali ya basi la JM kupinduka eneo  la Mazome  wilaya ya Kilolo. 
waliopoteza maisha katika ajali  hiyo ambayo chanzo ni dereva  wa lori la IT lililokuwa  likisafirishwa kwenda nchi  za  kusini mwa Tanzania aliyekuwa akitaka  kulipita gari la mbele mlimani na katika kona kali . 
Hata  hivyo  dereva  wa  lori  hilo IT aliyetambuliwa kwa jina la Gody  amevunjika mguu  wake ambao umetoka katika na  dereva  na utingo la fuso wamekupa papo hapo  huku mwanamke  aliyekuwa katika lori IT akisalimika . 

VYOMBO VYA HABARI KUBANIWA ZAIDI

Siku sita baada ya Serikali kuyafungia magazeti ya Mwananchi na Mtanzania kwa madai ya kuandika habari za uchochezi, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeibuka na kueleza jinsi Serikali ilivyowasilisha bungeni Muswada wa Marekebisho ya Sheria mbalimbali wa 2013, ikiwemo sheria ya magazeti ya mwaka 1976 na kuongeza faini kutoka Sh150,000 hadi Sh5 milioni.
Kimesema muswada huo mbali na kulenga kuviminya zaidi vyombo vya habari, pia unalenga kuwabana wananchi katika haki yao ya kutoa maoni, kwamba hata katika kifungu cha kanuni za adhabu imependekezwa faini ya Sh5 milioni kwa watakaoandika  maneno ya chuki na uchochezi.
Kutokana na hali hiyo, chama hicho kimeitaka Serikali kuwasilisha jedwali la mabadiliko ya muswada huo kabla ya kuanza kwa vikao vya kamati za Bunge Octoba 16 mwaka huu, kutishia kuwasilisha hati ya dharura marekebisho ya sheria hiyo bungeni kama mabadiliko hayatafanyika.
Kimeeleza kuwa uamuzi huo wa Serikali unalenga kuvifunga mdomo vyombo vya habari, katika kipindi hiki cha mchakato wa kuandika Katiba Mpya na maandalizi ya Uchaguzi Mkuu 2015.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Mkurugenzi wa habari na uenezi wa Chadema, John Mnyika alisema katika muswada huo, hakuna sehemu iliyopendekeza kufanyiwa marekebisho kifungu cha 25 cha sheria hiyo ya magazeti, ambacho kinaipa mamlaka Serikali kuyafungia magazeti, bila kuhitaji utetezi wowote, huku yenyewe ikiwa ndio mshtaki na mtoa adhabu.
Mnyika alisema muswada huo ulisomwa kwa mara ya kwanza katika mkutano wa bunge uliopita na utajadiliwa katika mkutano ujao wa bunge, utakaoanza mwishoni mwa mwezi huu.
“Katika sheria ya magazeti kifungu cha 25 hawajakigusa kabisa, badala yake wamegusa kifungu cha 36 na 37 tena kwa kuongeza faini” alisema na kuongeza;
“Vifungu hivi vinasema kuwa ukiandikwa uchochezi au uongo faini ni Sh150,000, lakini katika mapendekezo wanataka faini iwe Sh 5milioni, wakati huo huo kifungu cha adhabu ya kuyafungia magazeti hakijaguswa kabisa wakati ndio kinachopigiwa kelele na wadau wa habari kuwa hakifai.”
Mnyika alisema kinachofanywa na serikali ni kujaribu kuvibana vyombo vya habari na wananchi kutojadili au kutoa maoni ya jambo fulani, “Vyombo vya habari vinajiendesha katika mazingira magumu, hizi faini zinaongezwa ili iweje.”
Alisema tayari muswada huo umeshachapishwa katika gazeti la serikali tangu Agosti 23 mwaka huu, huku akiwataka wadau wa habari kupaza sauti na kupinga mapendekezo hayo, kushinikiza yachukuliwe mapendekezo ambayo waliwahi kuyatoa miaka ya nyuma juu ya kubadilishwa kwa sheria hiyo.
“Hata katika kanuni za adhabu kifungu cha 55,63 na 63(b), wamependekeza kuongezwa adhabu kwa watu watakaozungumza jambo lolote litakalotafsiriwa kuwa ni uchochezi na chuki, ingawa wamelenga katika masuala ya dini, ukabila na mengineyo, lakini lengo lao kuwabana wasema kweli” alisema Mnyika.
Alisema mapendekezo hayo yanalenga kuwanyima wananchi haki ya kutoa maoni, kwamba kifungu hicho kitawanyima uhuru na haki hata wale watakaokuwa wakitoa hotuba mbalimbali.

“Wanafanya hivi ili watu wasihoji kuhusu Katiba, wasihoji kuhusu uchaguzi mkuu, wasipofanya mabadiliko katika muswada huu tutajua wazi kuwa suala hilo linahitaji hati ya dharura ili kujadiliwa na kupatiwa ufumbuzi bungeni” alisema.

Monday, September 30, 2013

MKUU WA WILAYA YA MBULU AWAPIGIA MAGOTI WANANCHI

Mkuu wa Wilaya ya Mbulu, mkoani Manyara, Anatory Choya, amesema kuwa aliwapigia magoti wananchi wa Kijiji cha Hydom, ili kuonyesha unyenyekevu kwa wananchi hao aliodai walionekana kujazwa maneno ya uchochezi na wanasiasa ili wavuruge amani .
https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEi1RQQjJpo54_cA8AHS4i5uVreyJ931Y7TpIpXMDFMBNkVqQFSZe340fWxX9TnmZxAerhirCMtldZ5ZpLQOtwZKBHeYQAbf4A7ITiBH0KG8JckzIncmrMCnkAdipbnFV2xmRQHG_R_5PGLW/s1600/dc.jpg
Mkuu wa Wilaya ya Mbulu, mkoani Manyara, Anatory Choya akiwa amewapigia wananchi magoti kwa maana ya kuonyesha unyenyekevu
 

Alisema kutokana fujo zilizofanywa na baadhi ya wananchi hao katika mkutano wa hadhara uliofanyika majuzi, kwa nafasi yake angeweza kuagiza hata Jeshi la Polisi kuwadhibiti watu, lakini misingi ya dini yake haimruhusu kumdhuru mtu zaidi ya kumwonyesha unyenyekevu.
 Alisema hali hiyo ndiyo iliyomfanya kuamua kupiga magoti na kumshtakia Mungu.
 “Mimi ni mkristo, unyenyekevu ndiyo nguzo pekee ya kuonyesha upendo na kudumisha amani. Ningeweza kuagiza polisi wawadhibiti, lakini sioni sababu kwa kuwa hiyo siyo misingi ya utawala. Ndiyo maana nikaona bora nitumie njia nyingine ya kumshirikisha Mungu mbele yao,”alisema Choya na kuongeza:
 
“Wanasiasa wamekuwa wakipandikiza chuki kwa wananchi kwa makusudi kwa lengo la kuvuruga amani lakini kwa kumweka Mungu mbele nina imani tutafanikiwa ili siku moja tusije tukaingia kwenye mkumbo wa Syria na Misri”
 
Choya alitoa kauli hiyo jana alipokuwa akizungumza na Mwananchi Jumapili, siku chache baada ya kitendo chake cha kupiga magoti mbeye ya wananchi kwenye mkutano wake wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Haydom.
 
Mkuu huyo wa wilaya alidaiwa pia kuwalaani baadhi ya wakazi wa Kijiji cha Haydom kwa kile kinachodaiwa kuwa ni kumdharau na kutofuata maagizo yake, wakati yeye amewasaidia katika kutatua migogoro mbalimbali waliyokuwa nayo.
 
Tukio hilo la kusikitisha lilijitokeza baada ya wananchi wa kijiji hicho kupinga agizo la Choya, lililowataka kufanya uchaguzi wa kaimu mwenyekiti wa kijiji hicho, kabla ya kufanya uchaguzi mdogo, ambapo walipinga kwa kudai kuwa hakuna sheria hiyo.
 
Mmoja wa wananchi hao alilumbana na mkuu huyo wa wilaya mbapo Choya alijibu; “Nami nitarudi kwetu." Naye Tikin akasema tena: “Unasema utarudi kwenu Biharamulo wakati hawakutaki kwani ulifukuzwa ubunge?”
Maneno hayo yalionyesha kumkwaza Choya ambapo alipiga magoti huku machozi yakimlenga na kumwomba Mungu afanye jambo kwa watu wa Haydom kwani wanamdharau kabla ya kujitokeza wazee watatu wa Haydom na kumwomba msamaha mkuu huyo wa wilaya

MAGAZETI YAFUNGIWA

Ni Magazeti mawili ambayo ni Mtanzania na Mwananchi.
Ambapo Mtanzania limefungiwa kwa siku 90 na Mwananchi kwa siku 14.