Saturday, March 2, 2013

POLISI AUA MWALIMU KWA RISASI

MWALIMU wa Shule ya Sekondari Kitulo, wilayani Makete, Kastory Sote ameuawa baada ya kupigwa risasi begani na askari wa jeshi la polisi, wakati akitoa fedha kwenye mashine ya ATM katika benki ya NMB tawi la Makete.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Fulgensi Ngonyani alisema tukio hilo lilitokea katika eneo la benki na kumtaja askari aliyehusika kuwa ni PC Joseph Gelvas, mwenye namba G9790.

Alisema askari huyo, amekamatwa na anashikiliwa na jeshi hilo kwa tuhuma za mauaji na anatarajiwa kufikishwa mahakamani, wakati wowote kujibu tuhuma hizo.

Akisimulia tukio hilo, alisema askari huyo akiwa kazini alimuuliza mwalimu huyo kwanini anaendesha pikipiki eneo la benki, bila kuvaa kofia ngumu kichwani na kumwamuru aiweke pikipiki yake karibu na kibanda ambacho kinatumiwa na polisi, kwa ajili ya ulinzi ili atoe maelezo.
Alisema baada ya kuamuliwa kufanya hivyo, mwalimu huyo alitii agizo la kuweka pikipiki yake pembeni ili aweze kutoa maelezo kwa kosa alilokuwa akituhumiwa.

Alisema kwenye harakati za kuweka pikipiki, askari huyo alionekana akitaka kuondoka eneo la tukio, kitendo ambacho kilimfanya mwalimu naye aamue kuondoka na kuendelea na safari zake.
Akiwa umbali mfupi kutoka ilipo benki, askari huyo anadaiwa kumfyatulia risasi  ambayo ilimjeruhi bega la kulia na kuanguka chini, ambapo alifariki papo hapo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wakazi wa Makete walisema kifo cha mwalimu huyo, kinatokana na tabia ya baadhi ya askari ambao wamekuwa wakilinda benki hiyo, kuomba fedha kwa kutafuta makosa ya watu wanaoingia kuchukua fedha kwenye mashine.

Mmoja wa wakazi hao, Michael Sanga alisema kutokana na tabia ya askari hao kuendekeza kuomba fedha kwa wananchi, ni wazi  marehemu hakuwa tayari kutoa fedha hiyo.

Mwili wa marehemu, umesafirishwa kwenda  Mbalizi mkoani Mbeya kwa ajili ya mazishi.

CHANZO: TUMAINI MSOWOYA, NJOMBE

Friday, March 1, 2013

DC WA WILAYA YA MOSHI

MKUU  WA WILAYA YA MOSHI DK. IBRAHIM MSENGI, KILIMANJARO MWEZI FEBRUARI 2013 KATIKA MAENEO TOFAUTI MKOANI HUMO.
 KATIKA KIKAO NA NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI NA MAWASILIANO CHARLES TIZEBA
 AKIWA KATIKA RCC YA MKOA WA KILIMANJARO CHINI YA MWENYEKITI LEONIDAS GAMA
 MACHAME GATE AKIWASILI KUWAUNGA MKONO TOURISTS WA WFP
 DK MSENGI AKUTANA NA MWAKILISHI WFP NCHINI TANZANIA RICHARD RAGAN
 DC MSENGI AKITETA JAMBO NA MWIGIZAJI MAARUFU WA TAMTHILIA NA BALOZI WA WFP NCHINI AFRIKA KUSINI HLUBI MBOYA "NANDIPHA"
 DC MSENGI AKIZUNGUMZA JAMBO KATIKA ENEO LA MACHAME GETINI
 KIBAO CHA OFISINI KWAKE MJINI MOSHI

MWAKALEBELA APIGILIA MSUMARI UAMUZI WA SERIKALI KWA TENGA


Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini TFF FREDERICK MWAKALEBELA amezidi kuushindilia msumari wa motomchakato wa uchaguzi Mkuu wa TFF ambao umesitishwa na serikali na kudai kwamba haukufuata taratibu husika kama katiba ya chama hicho inavyotaka.

MWAKALEBELA ambaye amewahi kukiongoza kwa mafanikio chama hicho amesema, kufuatia kukiukwa kwa taratibu husika wakati wa upitishwaji na usajili wa marekebisho yaliyofanywa na TFF kwa njia ya waraka hivi karibuni ndio maana Serikali imeingilia kati na kutaka katiba ya mwaka 2006 itumike ili kutenda haki kwa wagombea wote.

Kwa maana hiyo MWAKALEBELA anapingana na taarifa zilizotolewa na Katibu Mkuu wa TFF ANGETILE OSIAH na baadhi yak viongozi wa Shirikisho hilo kwa kwa kuusimamisha uchaguzi huo Serikali inaingia maamuzi ya TFF jambo ambalo linapingwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani FIFA.

Akizungumza na Sports Extra ya CLODS FM MWAKALEBELA ameelezea kuwa Serikali haijaingilia maamuzi yak TFF katika mchakato wa uchaguzi na ilichofanya kuangalia sheria na kanuni za serikali ambazo zilikiukwa jambo ambalo lilikuwa likiiindolea TFF sifa za kuendesha shughuli zake nchini.

“Unaposema kuingia ni pale ambapo TFF imetoa maamuzi yake kwa mfano Mtibwa Sugar imepewa point baada ya kukata rufaa dhidi ya Yanga, hapa ikiwa Serikali itaingia na kutaka ushindi huo ubaki kwa Yanga itakuwa imeingia maamuzi ya chama cha soka na hilo ndilo jambo linakatazwa,” alisema MWAKALEBELA.

Mbali na hayo amesema kama chama cha mpira wa soka katika nchi yoyote ile hakijasajiliwa kwa kufuata sheria za nchi husika FIFA haiwezi kutoa kibali kwa chama hicho kushiriki na kuendesha mashindani yoyote jambo ambalo hapa nchini linafanywa na Baraza la Michezo la Taifa BMT na Msajili ya Michezo nchini.

Akizungumzia juu ya utaratibu uliotumiwa na Msajili wa Michezo nchini kupitisha waraka bila kufuatwa kwa taratibu MWAKALEBELA amesema, tayari Serikali imeyaona mapungufu hayo na kuchukua hatua stahiki huku akiikingia kifua TFF kwamba iliamua kuendesha uchaguzi baada ya msajili kuusajili waraka wao.

Kwa upande wake Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF kutoka Mkoa wa Dodoma MULAMU NGHAMBI amesema mgogoro wote ulioikumba mchakato wa uchaguzi mkuu wa TFF umetokana na Shirikisho hilo kukiuka katiba yake iliyojiwekea.

Akifafanua amesema licha ya baadhi ya Wajumbe kutoka mikoa mbalimbali kupinga utaratibu wa kupitisha katiba ya shirikisho hilo kwa njia ya waraka, TFF haikuchukua hatua hali ambayo imepelekea kuzuka kwa mgogoro huo.

MULAMU amesema katiba ya TFF inaeleza kinagaubaga kila jambo namna linavyotakiwa kuendeshwa ikiwemo jinsi ya kufanya marekebisho ya katiba lakini kilichofanyika hivi karibuni ni wazi TFF ilikiuka katiba yake mwenyewe.

Akifafanua Mjumbe huyo amewataka wadau wa Soka nchini kuachana na upotoshaji unaoendelea kwamba Serikali imeyakataa mabadiliko yote ya Katiba yaliyofanywa tangu mwaka 2006 na kwamba kilichofanyika ni kupingwa kwa mabadiliko ya sheria yaliyopitishwa mwaka 2012 kwa njia ya waraka.

Kufuatia hatua hiyo MULAMU ameiomba TFF na wadau wengine wa soka kufuata taratibu za soka walizojiwekea na kupitishwa kwenye Katiba ya TFF inayokubalika na Serikali ili hatimaye shirikisho hilo liweze kupata viongozi bora watakaoinua kiwango cha soka nchini.

KAMPUNI YA TANZANIA MWANDI YAANZISHA MICHUANO YA AFRICAN YOUTH FOOTBALL TOURNAMENT


Kampuni ya Tanzania Mwandi kwa kutambua kuwa Tanzania na Afrika nzima kuna vijana wengi ambao wana vipaji vya mpira wa miguu na hivyo wanachohitaji ni kuonyeshwa tu jinsi ya kuufikia 'Ulimwengu Halisi' wa Mpira duniani Tanzania Mwandi imeamua kuanzisha michuano ya African Youth Football Tournament ambayo itawashirikisha vijana wenye umri kati ya miaka 18 hadi 21.

http://us.123rf.com/400wm/400/400/ohmega1982/ohmega19821211/ohmega1982121100369/16394494-soccer-football-in-goal-net-with-sky-field.jpg
Michuano hiyo itaambatana na mafunzo kwa siku tano ambapo vijana hao watapata mafunzo ya mpira wa Miguu (elimu, ujuzi na hata mbinu za uwanjani) kutoka kwa makocha wawili wa hapa nchini na watatu wa kimataifa kutoka nje ya nchi, kuanzia tarehe 10/06/2013 hadi tarehe 14/06/2013 katika Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume.

Aidha, mafunzo yatafanyika nyakati za asubuhi na jioni wachezaji hao watashiriki Mashindano ya kucheza wao kwa wao ili kupata vijana 11 bora miongoni mwa wachezaji watakaoshiriki.

Wachezaji Bora 11 watakaopatikana watakuwa mabalozi wa Mdhamini Mkuu wa Michuano ya African Youth Football Tournament na watapata fursa ya kutangazwa zaidi kimataifa na kutafutiwa vilabu vya kucheza soka Barani Ulaya katika nchi nane (Ufaransa, Ureno, Uswis, Ubelgiji, Uholanzi, Norway, Sweden na Denmark pamoja na barani Afrika na Asia.

Ili kupanua wigo wa kuwatangaza kimataifa wachezaji wengi zaidi, Michuano hii pia itaalika skauti na mawakala wa soka wa kimataifa ili kufuatilia uwezo wa wachezaji hao asubuhi katika mazoezi na jioni kwenye michuano, kuwapata vijana bora ambao watapendelea kuwatafutia timu nje ya nchi kukipiga huko kwa makubaliano ambayo pande hizo mbili (mchezaji na wakala) zitaafikiana.

Miongoni mwa Mawakala ambao watakuwepo ni wakala wa Kimataifa wa Tanzania, Dk. Damas Ndumbaro, Phillip Mwakikosa (Sweden) na wengine wengi.

Hata hivyo kutokana na gharama kubwa za uandaaji wa Michuano hii, na ndio kwanza ikiwa inaanzishwa, Kampuni ya Tanzania Mwandi kwa kujali mahitaji ya Kitanzania tumeweka kiingilio kwa mchezaji wa Tanzania kuwa shilingi laki tatu (Tsh. 300, 000) na mchezaji wa nje ya Tanzania Dola 500 za Kimarekani (USD 500).

Fedha hizo zitagharamia malazi, chakula na mahitaji mengine yote kwa mchezaji pindi atakapokuwa kambini.

Hii ni fursa adimu kwa vijana wa Kitanzania kuonyesha uwezo wao ili kutimiza ndoto za kucheza soka barani Ulaya, Asia na barani Afrika katika vilabu vikubwa huku ikikumbukwa kuwa mnamo Mwaka 2012 ni wachezaji wachache sana wa Kitanzania waliopata fursa ya kufanya majaribio ya kucheza soka la kulipwa kutokana na uchache wa mawakala na gharama hivyo kuletwa mawakala hao nyumbani Tanzania ni fursa pekee ya kufikia malengo.

Mpaka sasa tayari Kampuni ina majina takribani ya vijana 10 wa Nje ya nchi (Uganda, Nigeria na Ghana) ambao wameomba kushiriki hivyo tunatoa wito kwa Watanzania kutoipoteza fursa ya kuletewa njia ya kuelekea kusakata soka Barani Ulaya mlangoni mwao.

Lakini tunafahamu hali halisi ya maisha yetu kwahiyo nitoe wito kwa Wadhamini mbalimbali ambao tumewaomba kutusaidia kufanikisha Mashindano haya ambayo naamini yatalitangaza taifa letu na kulitangaza zaidi soka letu kimataifa. Pia udhamini wao utatuwezesha kupunguza hizi gharama kwa washiriki kutoka Tanzania na hivyo kuwachukua vijana wengi zaidi.

Kampuni ya Tanzania Mwandi ni Kampuni binafsi ambayo imejikita katika kuendeleza sekta za utalii, michezo na burudani ndani na nje ya nchi na hivyo kuiongezea kipato nchi moja kwa moja ama kupitia kuwawezesha wananchi kama vile kuwatengenezea fursa za ajira vijana kupitia michezo.

Fomu za ushiriki Michuano hii zinapatikana kupitia www.tanzaniamwandi.co.tz nawww.blog.tanzaniamwandi.co.tz
“African Youth Football Tournament; Live your Drea

Monday, February 25, 2013

POLISI YAWASHIKILIA WATU 13 WAKIWEMO JWTZ NA POLISI KWA UNYANG'ANYI


JESHI la Polisi Mkoa wa Mbeya, linawashikilia watu 13, wakiwemo askari wawili wa Jeshi la wananchi (JWTZ) na polisi mmoja  kwa matukio ya mauaji na unyang'anyi wa kutumia silaha.

Akizungumza na waandishi habari jijini Mbeya Kamanda wa polisi mkoa wa Mbeya  Diwani Athuman amesema watuhumiwa hao wamewagawanya katika makundi mawili, ambapo kundi la kwanza ni la watuhumiwa 9 wakiwemo askari hao wawili wakidaiwa kuhusika na tukio la kuwaua kikatili na kisha kuwazika dereva na utingo wake.

Kundi la pili ni la watuhumiwa wanne wanaotuhumiwa kuhusika na mauaji ya dereva wa polisi lililotokea Wilayani Chunya mkoani hapa baada ya kufanyika uporaji wa shilingi milioni 2,200,000 katika kituo cha mafuta eneo la Matundasi wilayani chunya.

Akitoa ufafanuzi zaidi Kamanda Diwani amesema, katika tukio la kwanza ni lile lililotokea Februari 2 katika eneo la Mafinga,Mkoani Mbeya, ambapo watuhumiwa wa kundi la kwanza waliwateka dereva na utingo wake, Festo Kyando (45) na Jafari lililotokea na kuwaua kisha kwenda kuwazika porini.

Amesema dereva huyo alikuwa ametoka Jijini Dar es salaam kubeba mzigo wa wafanyabiashara kwa lengo la kuleta mkoani Mbeya, lakini kumbe walikuwa wakiwindwa na walipofika mkoani Iringa walitekwa na kufanyiwa mauaji hayo ya kinyama.

Kamanda Diwani amesema kufuatia tukio hilo jeshi la polisi lilianza uchunguzi mkali na hatimaye kunasa mtandao huo wa watu 9 wakiwemo askari hao wawili wa jeshi la polisi na JWTZ,ambao uchunguzi umebaini kuwa hutoa mavazi ya majeshi hayo na silaha.

Kamanda Diwani amewataja watuhumiwa hao kuwa MT.85393 Samwel Charles  Balumwina(31) wajiriwa wa jeshi la wananchi kikosi 844 kikosi cha Itende Mbeya na G.1901PC Samwel Kigunye (27) askari wa jeshi la polisi Jijini Mbeya.

Wengine ni mfanyabiashara maarufu wa eneo la Mwanjelwa, Gath Mbilinyi (32), Rajabu Mbilinyi(25), Gregory Mtega(25,Francis Sanga(30) pamoja na ndugu ambao ni wafanyabiashara maarufu katika mji wa Makambako mkoani Njombe ambao ni Japhet Ng'ang'ana(24), Claud Ng'ang'ana(36), Hilally Ng'ang'ana(30)

Hata hivyo amesema walifanikiwa kukamata bidhaa hizo katika eneo la Tunduma ambako tayari zilikuwa zimekamatwa na kwamba miongoni mwa watuhumiwa ndiye aliyeuziwa mzigo huo.

Amesema mali zilizookolewa katika matukio hayo kuwa ni Nondo 397 za aina tofauti pamoja na bando 18 za mifuko ya sandarusi(Sulphate) ambavyo vinashikiliwa na jeshi la Polisi Tunduma Wilani Mbozi Mkoani hapa.

Katika tukio la pili ni lile linalohusisha vifo vya watu wawili wilayani Chunya, ambao ni dereva wa polisi na dereva wa gari la majambazi baada ya kutokea kurushiana risasi.

Amesema tukio hilo lilitokea Februari 6 baada ya watuhumiwa wanne ambao wanashikiliwa na jeshi hilo kufanya uporaji wa shilingi milioni 2,200,000 katika kituo cha matundasi wilayani humo.
Amewataja madereva hao waliouwawa katika tukio hilo kuwa ni dereva wa polisi aliyefahamika kwa jina moja la Jafari, ambapo yule wa majambazi akitajwa kwa jina la  Shabani John.

Diwani amewataja watuhumiwa wanashikiliwa kwa tukio hilo kuwa ni Manase Kibona (37).Emmanuel Mndendemi na Masai Hongole, Mashaka George, John Mahenge, Narasco Mabiki.

Kamanda huyo amezitaja mali zilizookolewa katika matukio hayo kuwa ni Nondo 397 za aina tofauti pamoja na bando 18 za mifuko ya sandarusi(Sulphate) ambavyo vinashikiliwa na jeshi la Polisi Tunduma Wilani Momba  Mkoani Mbeya.

Aidha,kamanda Diwani  amevitaja baadhi ya vielelezo vilivyokamatwa  kuwa ni Bunduki aina ya Shot Gun moja ambayo namba zake zilifutika, Gobore moja ambalo pia namba zake zilifutika, Bastora tatu zilizotengenezwa kienyeji zisizo na namba na zinazotumia risasi za s/Gun.

Vingine ni Risasi 31 za Silaha ya SMG/SAR, Sare za Jeshi (JWTZ), suruali 4, mashati 4 kofia 3 na Viatu jozi mbili , Risasi 99 za S/GUN, Risasi 25 za Bastola na magari yenye namba T 464BLX TOYOTA COROLA,T381 BDR VITZ, T 251 AKU Toyota Pick Up ,T 193 BDY  Toyota Premio na T 214 ASV  Toyot Mark II.

Hata hivyo Kamanda wa Polisi anawashukuru wananchi wa Mkoa wa Mbeya waliojitokeza katika kutoa ushirikiano wa kuwasaka majambazi hayo ambapo pia anaendelea kutoa wito kwa watu wenye taarifa za watu ambao haeajakamatwa.
Ameongeza kuwa taratibu za upelelezi zimekamilika ambapo taratibu za kuwafikisha mahamakamani zinaendelea.

CHANZO: JOSEPH MWAISANGO, MBEYA YETU NA JESHI LA POLISI MKOANI MBEYA    

MDAHALO WA UCHAGUZI MKUU KENYA USIKU HUU UNAENDELEA


Wagombea urais nchini Kenya, usiku huu  wanashiriki katika mdahalo wa pili na wa mwisho, ikiwa ni wiki moja kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu Machi 4. 
 
http://s1.ibtimes.com/sites/www.ibtimes.com/files/styles/article_slideshow_slide/public/2013/02/12/kenya-debate.jpgMgombea urais wa muungano wa Jubilee, Uhuru Muigai Kenyatta, aliashiria awali kuwa hatashiriki kwenye mdahalo huo, lakini sasa yupo katika mdahalo huo. Mdahalo huo utazingatia zaidi masuala ya ardhi na maendeleo ya kiuchumi. Mdahalo wa unahudhuriwa na kiongozi wa ujumbe wa waangalizi wa Umoja wa Afrika kwenye uchaguzi mkuu wa Kenya, rais wa zamani wa Msumbiji Joachim Chisano na rais wa zamani wa Botswana, Festus Mogae. Mdahalo wa kwanza ulifanyika tarehe 11 ya mwezi huu wa Februari, ambapo uligusia masuala ya ukabila, rushwa, usalama, elimu na huduma ya afya. Katika mdahalo wa kwanza, wagombea wote wanane wanaowania kiti cha urais walishiriki.

BABA BENEDICT XVI ABADILISHA SHERIA YA ROMA


Baba Mtakatifu Benedikto wa Kumi na Sita amebadilisha sheria ya Kanisa Katoliki ambayo inaruhusu mrithi wake kuchaguliwa mapema zaidi. 

http://www.biography.com/imported/images/Biography/Images/Profiles/B/Pope-Benedict-XVI-15045109-1-402.jpg
Baba Mtakatifu Benedikto wa xvi
Msemaji wa Vatican, Padri Federico Lombardi, amesema Makardinali hawatasubiri kwa wiki mbili kabla ya kuanza kikao cha siri cha kumchagua Baba Mtakatifu mpya. Sheria za awali zilikuwa zinawataka Makardinali kusubiri siku 15 zipite baada ya Baba Mtakatifu kufariki au kujiuzulu na ndipo wamchague Baba Mtakatifu mwingine. Mwanzoni mwa mwezi ujao wa Machi, Makardinali wote wa Kanisa Katoliki wataamua tarehe ya kuanza kikao chao cha siri cha kumchagua Baba Mtakatifu mpya, kufutia kujiuzulu kwa Baba Mtakatifu Benedikto wa Kumi na Sita tarehe 28 ya mwezi huu. Zikiwa zimebakia siku nne tu kwa Baba Mtakatifu kujiuzulu, kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki duniani amekubali ombi la kujiuzulu kwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Edinburgh, Mwadhama Keith Kardinali O'Brien, kutokana na tuhuma kwamba alionyesha tabia zisizofaa kwa mapadri. Hata hivyo, Kardinali O'Brien, ambaye ni Kardinali pekee wa Uingereza aliyekuwa na uwezo wa kumchagua Baba Mtakatifu, amekanusha tuhuma hizo.