Tuesday, September 24, 2013

AL-SHABAAB WATISHIA KUIVAMIA TANZANIA NA UGANDA

Wakati Jeshi la Polisi la Tanzania likisema linafuatilia taarifa za vitisho za kundi la Al-Shabaab la Somalia za kushambulia, Mtanzania mmoja, Vedasto Nsanzugwanko ambaye alijeruhiwa kwenye shambulio la Kenya ameelezea yaliyomkuta. 


Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba alisema jana kuwa wameanza kufuatilia kwa undani taarifa zilizozagaa katika mitandao ya kijamii kwamba kundi la Al-Shabaab linajipanga kuishambulia Tanzania na Uganda.


DCI Manumba alikiri kusikia taarifa hizo na kusema kuwa Jeshi la Polisi limeanza kufanya uchunguzi wa kina: “Siwezi kukueleza ni uchunguzi wa aina gani tutakaofanya, hiyo ni siri yetu.”


Hata hivyo, Msemaji wa Jeshi la Wananchi (JWTZ), Meja Eric Komba alisema kuwa kuna uwezekano taarifa hizo zikapikwa na wajanja wachache kwa ajili ya kuwajengea hofu wananchi.


“Taarifa za kwenye mitandao wakati mwingine ni uzushi mtupu… kuna kipindi ziliwekwa taarifa za uongo zinazohusu jeshi hili,” alisema.


Alipotakiwa kutoa msimamo wa jeshi hilo iwapo taarifa hizo zitakuwa na ukweli alisema, “Jeshi tuko tayari kwa jambo lolote.”