Shaban Robert |
Hakuna apingaye kuwa Shaban Robert alikuwa manju wa fasihi ya Kiswahili, ambaye hata baada ya miaka 50 tangu kifo chake mwaka 1962, hakuna aliyejitokeza kumpiku kwa kiwango alichofikia katika fani ya fasihi.
Mpaka sasa kazi zake nyingi bado zinaishi, huku zikiwa zimetafsiriwa katika lugha mbalimbali na kusambazwa kote duniani.
Bila shaka, mtu huyu anabaki kuwa miongoni mwa watu muhimu waliowahi kutokea nchini. Lakini inashangaza kuwa familia yake na hata historia yake vimetelekezwa!
Hata mahala lilipo kaburi lake katika kijiji cha Machui, Kusini mwa Jiji la Tanga, pameshindwa kuendelezwa japo kwa kuwa na makumbusho madogo ya mwanafasihi huyo aliyetamba ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.
Kimsingi, eneo hili mbali ya kuwa sehemu muhimu katika historia ya nchi, pia lingeweza kutumika kama darasa la kuwakusanya watu, hasa watafiti na wanahistoria kutoka pembe zote za dunia. Ukitoa simulizi isiyovutia ya kusahauliwa kwa Shaban Robert, baada ya utafiti wa miaka mingi kuna habari mpya za kugunduliwa kwa kazi nyingine za gwiji huyo.
Kwa mujibu wa mwanafasihi bobezi nchini, Profesa Mugyabuso Mulokozi, aliyeshiriki katika utafiti huo, kazi hizi hazikuwahi kufahamika awali.
Anasema katika utafiti wao mpya wamegundua mafungu ya barua ambayo Shaabani Robert aliyaweka katika makundi ya nyaraka za kifamilia, kazi na ajira, pamoja na kiofisi.
‘’Baadhi ya barua zinahusu uhusiano kati ya mtu na kaka yake. Shaaban Robert alijipa jukumu la kulea, anazungumzia umuhimu wa mtu kutenda mema na umuhimu wa elimu katika dunia hii’’anabainisha.
Pia anasema katika utafiti huo wamebaini makala za mashairi alizopeleka kwenye mashindano, na kuwa mashairi hayo bado ni muswada yakisubiri kuchapishwa.
Miongoni mwa mambo yanayoibua maswali kwa wanafasihi wa sasa ni namna Shaaban Robert alivyoweza kuepuka misukosuko ya kisiasa, hasa enzi za ukoloni kwani baadhi ya kazi zake zipo zilizokuwa zikipinga unyanyasaji wa Waafrika.
Jambo hili pia limebainika katika utafiti huo mpya. Inadaiwa kuwa katika vita Kuu ya Pili ya Dunia(1939-1945), aliandika utenzi wa vita hiyo akiisifia Uingereza kuwa ilikuwa na haki dhidi ya dola ya Wajerumani.
Utenzi huo haukuifurahisha Ujerumani na gwiji huyo wa fasihi ya lugha ya Kiswahili aliwekwa katika orodha ya watu watakaonyongwa endapo Wajerumani wangeshinda vita.
Aidha, kwa mujibu wa Profesa Mulokozi miongoni mwa kazi zilizogunduliwa, ni sehemu ya utenzi alioandika akilalamikia kuhamishwa vituo vya kazi mara kwa mara.
Sehemu ya utenzi huo inanukuliwa ikisema:
’Nimezaliwa Tanga 1909, tangu utoto sina kituo hasa, naona sina siasa ila kuandama njia’’
Mashairi mengine yanatajwa kuwa yanaelezea mila za watu wa Tanga.
Katika kazi mpya zilizogunduliwa pia anazungumzia jinsi watu walivyoweza kupata tiba. Kwa mfano, anasema mtu alipougua alikwenda kwenye tambiko, msikitini kuombewa au hospitali.
Akimzungumzia Shaaban Robert, mwanafunzi wa Shahada ya Uzamili katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Felix Sosoo anasema kuwa alikuwa ni mtunzi aliyeheshimika na ametoa mchango mkubwa kuendeleza lugha ya Kiswahili.
Mwanafunzi huyo kutoka Ghana anasema amefika nchini kujifunza zaidi lugha ya Kiswahili na baada ya masomo atarudi Chuo Kikuu cha Ghana kama mtaalamu wa lugha hiyo.
Anasema anajivunia kusomea katika nchi anayosema ndiyo chimbuko la lugha ya Kiswahili na kuwa lugha hiyo ni utambulisho wa utamaduni wa Afrika. Matarajio yake ni kubobea na kuwa mtalaamu zaidi wa lugha hiyo.
‘’Nimetoka Ghana kujifunza Kiswahili ambayo ni kama lugha ya Afrika, hapa najifunza Kiswahili fasaha. Lugha hii itanirahisishia kujifunza lugha nyingine pia’’ anasema Sosoo
Akitoa maoni yake kuhusu umahiri wa Shaaban Robert, msanii wa Kimataifa John Mugango, anasema mtunzi huyo ameacha somo kwa Taifa kuendeleza watu wake kulingana na vipaji walivyonavyo.
Anasema vipaji vingi vinapotea kwa kutoendelezwa na kuwa badala yake wanapatikana wataalamu wanaofanya kazi kwa shinikizo la kukosa ajira na siyo kwa sababu ya kupenda kazi husika.
‘’Tusomee vipaji vyetu, ukiona daktari anakukaripia baada ya kumfikisha mgonjwa hospitali, ujue huyo ana damu ya ajira katika kazi yake na siyo udaktari wa kujitambua’’anabainisha Mugango
Naye Mwalimu Domician Domonick kutoka Shule ya Sekondari Bukoba, anashangaa gwiji huyo kutopewa shahada ya heshima na taifa, kama sehemu ya kutambua mchango wake katika kukuza lugha ya Kiswahili.
Anasema Shaabani Robert ana mchango mkubwa katika kuifanya lugha hiyo iheshimike duniani. Analalamika kuwa hivi sasa Serikali inapitisha vitabu vya kufundishia lugha hiyo ambavyo maudhui yake ni dhaifu.
Anasema vitabu vinavyotumika hivi sasa vingi havina mantiki ya fasihi na kwa vyovyote haviwezi kulinganishwa na vile vilivyotungwa na Shaaban Robert. Anarejea baadhi ya vitabu vyake kama vile Mapenzi Bora kinachoonyesha umuhimu wa elimu.
Ikbal Shaaban ambaye ni mtoto wa Shaaban Robert anasema kazi za baba yake hazijasaidia kuboresha maisha ya familia aliyoiacha.
Anaeleza kuwa wapo wajanja wanaofaidika na jasho la baba yao na kuwa hakuna pato linaloingia katika familia yao kutokana na mauzo ya kazi hizo.
‘’Bado hatujaona faida ya kazi zake zaidi ya kuitwa kwenye semina, kuna wajanja wanaonufaika na jasho lake,tuko mbioni kuanzisha vita mpya dhidi ya kazi za marehemu’’ analalamika.
Ikbal anadai kuwa gwiji huyo wa lugha ya Kiswahili hajapewa heshima ya kutosha na Taifa, licha ya kuwa kazi zake zinaendelea kutumika kuendeleza na kuitangaza lugha hiyo.
Kwa hali yoyote ile, huu ni wakati wa kumuenzi Shaaban Robert kwa kutambua mchango wake kwa taifa, huku tukiendelea kuwaandaa wanafasihi wengine wa baadaye.
Mtoto wa marehemu Shaaban Robert Ikbal Shaaban akiwa katika moja ya makongamano ya kujadili mchango wa kazi za baba yake katika fasihi ya Kiswahili. (Picha na Phinias Bashaya) |
No comments:
Post a Comment