Thursday, September 12, 2013

KESI YA SHEIKH PONDA YAAHIRISWA

Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Morogoro jana iliitaja na kuahirisha kesi inayomkabili Katibu wa Jumuiya na Taasisi ya Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda bila ya kiongozi huyo kuwapo mahakamani.
 
Kesi hiyo ilitajwa jana na Mwanasheria wa Serikali, Gloria Rwakibalila mbele ya Hakimu wa Mahakama hiyo, Agnes Ringo na kuahirishwa hadi Septemba 17 mwaka huu, wakati Mahakama itakapotoa uamuzi kuhusu maombi ya kiongozi huyo kupatiwa dhamana.
Hii ni mara ya kwanza kwa kesi hiyo kutajwa bila Ponda kuwapo, huku kukiwa na utulivu tofauti na siku zilizopita.
Mara ya mwisho Agosti 29, Ponda alifikishwa mahakamani hapo na kusababisha kusimama kwa shughuli za Serikali wilayani Morogoro baada ya ofisi kadhaa ikiwamo ya Mkuu wa Wilaya na baadhi ya mitaa kufungwa ili kupisha kusikilizwa kwa kesi hiyo.
Kadhalika Agosti 19, mwaka huu Ponda alisafirishwa kwa helikopta akiwa chini ya ulinzi mkali, na kesi yake ilivuta umati mkubwa watu.
Jana kesi hiyo ikitajwa kwenye mahakama ya ndani (chamber court) na baadhi ya wafuasi wa Ponda walionekana nje ya uzio wa mahakama hiyo huku wakiwa hawajui nini kinachoendelea.
Ilimlazimu Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Richard Kabate kutoka nje ya ofisi yake na kuwaeleza wafuasi hao sababu za kutofikishwa kwa kiongozi wao mahakamani hapo.
“Kesi hiyo imeshindikana kutajwa kwenye mahakama ya wazi kwa sababu mahakama hiyo inatumiwa kuendeshea kesi nyingine chini ya majaji wa Mahakama Kuu, hatutaki kuleta mwingiliano.
“Ninataka kuwaeleza kuwa mwondoke kwa kuwa Sheikh Ponda hakufikishwa mahakamani hapa leo hadi Septemba 17 atakapoletwa kwa ajili ya kutolewa kwa uamuzi wa dhamana,” alisema Hakimu Kabate.
Baada ya Hakimu Kabate kutoa ufafanuzi huo, wafuasi hao walionekana kutoridhishwa na kauli hiyo na kuanza kujikusanya vikundi vikundi, lakini baadaye walianza kutawanyika.
Mashtaka yaliyotajwa mahakamani hapo na kumkabili Sheikh Ponda ni matatu ambayo ni uchochezi, kuharibu imani ya watu wengine na kushawishi kutendeka kwa kosa, mashtaka ambayo anadaiwa kuyatenda Agosti 10 mwaka huu eneo la Kiwanja cha Ndege Manispaa ya Morogoro.
Sheikh Ponda anatetewa na mawakili watatu wakiongozwa na wakili Msomi Juma Nassor ambaye tayari amewasilisha ombi la dhamana.

No comments:

Post a Comment