Tuesday, September 10, 2013

WABUNGE WAVUTANA MBELE YA MH. RAIS

 Wabunge wa majimbo mawili ya wilaya ya Kwimba Mkoani Mwanza, Mh. Richard Ndassa wa sumve na Mh. Shanifu Manssor wa jimbo la Kwimba wamevutana mbele ya rais Dk. Jakaya Mrisho Kikwete kuhusu utekelezaji wa mradi wa kupeleka maji mjini Ngudu na kumlazimu rais kumtaka waziri wa maji Prof. Jumanne Maghembe kutoa ufafanuzi kuhusu utekelezaji wa mradi huo.

Mvutano huo umekuja kufuatia taarifa ya wilaya ya Kwimba iliyosomwa kwa rais Jakaya Kikwete na mkuu wa wilaya hiyo Bw. Selemani Mzee, ambaye amesema hali ya huduma ya maji mjini Ngudu kwa sasa ni mbaya kupindukia ambapo idadi ya wananchi wanaopata majisafi na salama ni 11,310 tu kati ya watu 25,370, idadi ambayo ni sawa na asilimia 44.6 kutokana na mji huo kutegemea visima virefu vitano, ambavyo vilichimbwa miaka kati ya 27 na 57 iliyopita, huku pia uwezo wa chanzo cha maji kilichopo kikiwa ni mita za ujazo 265 kwa siku, ambapo maji hayo hutolewa kwa mgao kila baada ya siku tatu.

Huku kila mbunge akionekana kuvutia upande, mbunge wa Sumve Mh. Richard Ndasa ameshauri mradi huo wa kupeleka maji katika mji wa Ngudu utokee Magu kupitia jimboni kwake ili kuvinufaisha vijiji zaidi ya 40, huku mbunge wa jimbo la Kwimba Mh. Shanifu Mansoor akisema kuwa ni vizuri serikali iendelee na mpango wake wa kutumia maji ya ziwa victoria yanayotolewa kwenye mradi wa Kahama- Shinyanga ( kashwasa ) na kuyapeleka ngudu kutokea kijiji cha mhalo, hatua ambayo itanufaisha vijiji zaidi ya 60 vya tarafa ya mwamashimba na Ngudu.

Katika kuweka sawa hali ya mambo, waziri wa maji Mh. Prof. Jumanne Maghembe amesema kwamba serikali itatekeleza miradi yote miwili, ambayo ni ya kutoa maji kijiji cha Mhalo kwenda Runere na hatimaye kufika mjini Ngudu pamoja na ule wa kutoka wilayani Magu ambao uko kwenye mchakato wa kumpata mhandisi mshauri wa kusanifu mradi huo, na kuongeza kuwa mradi wa maji wa mwamashimba kwa mwaka huu umetengewa shilingi milioni 500.

Mapema akizungumza na wananchi wa wilaya ya Kwimba wakati akifungua uwanja wa ndani wa michezo katika chuo cha maendeleo ya michezo Malya, rais  Kikwete amesema atahakikisha miradi yote miwili inatekelezwa kama alivyohaidi wananchi wakati wa kampeni ili kuondoa kero ya maji katika wilaya ya kwimba yenye wakazi zaidi ya laki mbili.

No comments:

Post a Comment