Saturday, March 2, 2013

POLISI AUA MWALIMU KWA RISASI

MWALIMU wa Shule ya Sekondari Kitulo, wilayani Makete, Kastory Sote ameuawa baada ya kupigwa risasi begani na askari wa jeshi la polisi, wakati akitoa fedha kwenye mashine ya ATM katika benki ya NMB tawi la Makete.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Fulgensi Ngonyani alisema tukio hilo lilitokea katika eneo la benki na kumtaja askari aliyehusika kuwa ni PC Joseph Gelvas, mwenye namba G9790.

Alisema askari huyo, amekamatwa na anashikiliwa na jeshi hilo kwa tuhuma za mauaji na anatarajiwa kufikishwa mahakamani, wakati wowote kujibu tuhuma hizo.

Akisimulia tukio hilo, alisema askari huyo akiwa kazini alimuuliza mwalimu huyo kwanini anaendesha pikipiki eneo la benki, bila kuvaa kofia ngumu kichwani na kumwamuru aiweke pikipiki yake karibu na kibanda ambacho kinatumiwa na polisi, kwa ajili ya ulinzi ili atoe maelezo.
Alisema baada ya kuamuliwa kufanya hivyo, mwalimu huyo alitii agizo la kuweka pikipiki yake pembeni ili aweze kutoa maelezo kwa kosa alilokuwa akituhumiwa.

Alisema kwenye harakati za kuweka pikipiki, askari huyo alionekana akitaka kuondoka eneo la tukio, kitendo ambacho kilimfanya mwalimu naye aamue kuondoka na kuendelea na safari zake.
Akiwa umbali mfupi kutoka ilipo benki, askari huyo anadaiwa kumfyatulia risasi  ambayo ilimjeruhi bega la kulia na kuanguka chini, ambapo alifariki papo hapo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wakazi wa Makete walisema kifo cha mwalimu huyo, kinatokana na tabia ya baadhi ya askari ambao wamekuwa wakilinda benki hiyo, kuomba fedha kwa kutafuta makosa ya watu wanaoingia kuchukua fedha kwenye mashine.

Mmoja wa wakazi hao, Michael Sanga alisema kutokana na tabia ya askari hao kuendekeza kuomba fedha kwa wananchi, ni wazi  marehemu hakuwa tayari kutoa fedha hiyo.

Mwili wa marehemu, umesafirishwa kwenda  Mbalizi mkoani Mbeya kwa ajili ya mazishi.

CHANZO: TUMAINI MSOWOYA, NJOMBE

No comments:

Post a Comment