Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini TFF FREDERICK MWAKALEBELA amezidi kuushindilia msumari wa motomchakato wa uchaguzi Mkuu wa TFF ambao umesitishwa na serikali na kudai kwamba haukufuata taratibu husika kama katiba ya chama hicho inavyotaka.
MWAKALEBELA ambaye amewahi kukiongoza kwa mafanikio chama hicho amesema, kufuatia kukiukwa kwa taratibu husika wakati wa upitishwaji na usajili wa marekebisho yaliyofanywa na TFF kwa njia ya waraka hivi karibuni ndio maana Serikali imeingilia kati na kutaka katiba ya mwaka 2006 itumike ili kutenda haki kwa wagombea wote.
Kwa maana hiyo MWAKALEBELA anapingana na taarifa zilizotolewa na Katibu Mkuu wa TFF ANGETILE OSIAH na baadhi yak viongozi wa Shirikisho hilo kwa kwa kuusimamisha uchaguzi huo Serikali inaingia maamuzi ya TFF jambo ambalo linapingwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani FIFA.
Akizungumza na Sports Extra ya CLODS FM MWAKALEBELA ameelezea kuwa Serikali haijaingilia maamuzi yak TFF katika mchakato wa uchaguzi na ilichofanya kuangalia sheria na kanuni za serikali ambazo zilikiukwa jambo ambalo lilikuwa likiiindolea TFF sifa za kuendesha shughuli zake nchini.
“Unaposema kuingia ni pale ambapo TFF imetoa maamuzi yake kwa mfano Mtibwa Sugar imepewa point baada ya kukata rufaa dhidi ya Yanga, hapa ikiwa Serikali itaingia na kutaka ushindi huo ubaki kwa Yanga itakuwa imeingia maamuzi ya chama cha soka na hilo ndilo jambo linakatazwa,” alisema MWAKALEBELA.
Mbali na hayo amesema kama chama cha mpira wa soka katika nchi yoyote ile hakijasajiliwa kwa kufuata sheria za nchi husika FIFA haiwezi kutoa kibali kwa chama hicho kushiriki na kuendesha mashindani yoyote jambo ambalo hapa nchini linafanywa na Baraza la Michezo la Taifa BMT na Msajili ya Michezo nchini.
Akizungumzia juu ya utaratibu uliotumiwa na Msajili wa Michezo nchini kupitisha waraka bila kufuatwa kwa taratibu MWAKALEBELA amesema, tayari Serikali imeyaona mapungufu hayo na kuchukua hatua stahiki huku akiikingia kifua TFF kwamba iliamua kuendesha uchaguzi baada ya msajili kuusajili waraka wao.
Kwa upande wake Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF kutoka Mkoa wa Dodoma MULAMU NGHAMBI amesema mgogoro wote ulioikumba mchakato wa uchaguzi mkuu wa TFF umetokana na Shirikisho hilo kukiuka katiba yake iliyojiwekea.
Akifafanua amesema licha ya baadhi ya Wajumbe kutoka mikoa mbalimbali kupinga utaratibu wa kupitisha katiba ya shirikisho hilo kwa njia ya waraka, TFF haikuchukua hatua hali ambayo imepelekea kuzuka kwa mgogoro huo.
MULAMU amesema katiba ya TFF inaeleza kinagaubaga kila jambo namna linavyotakiwa kuendeshwa ikiwemo jinsi ya kufanya marekebisho ya katiba lakini kilichofanyika hivi karibuni ni wazi TFF ilikiuka katiba yake mwenyewe.
Akifafanua Mjumbe huyo amewataka wadau wa Soka nchini kuachana na upotoshaji unaoendelea kwamba Serikali imeyakataa mabadiliko yote ya Katiba yaliyofanywa tangu mwaka 2006 na kwamba kilichofanyika ni kupingwa kwa mabadiliko ya sheria yaliyopitishwa mwaka 2012 kwa njia ya waraka.
Kufuatia hatua hiyo MULAMU ameiomba TFF na wadau wengine wa soka kufuata taratibu za soka walizojiwekea na kupitishwa kwenye Katiba ya TFF inayokubalika na Serikali ili hatimaye shirikisho hilo liweze kupata viongozi bora watakaoinua kiwango cha soka nchini.
No comments:
Post a Comment