Jana, Bingwa wa Dunia wa uzani wa kati (super middle), unaotambuliwa na Shirikisho la Ngumi Duniani (WBF), Francis Cheka alitembelea Bunge baada ya kutwaa taji hilo karibuni na jana hiyohiyo, Bunge hilo lilishuhudia ngumi kavukavu katika vurugu kubwa pengine kuliko zote zilizowahi kutokea katika ukumbi wake.
Katika masumbwi hayo yasiyo rasmi, Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ anadaiwa kumpiga kichwa Askari wa Bunge na kumchania sare na kung’oa kipaza sauti.
Mbilinyi jana alisema alikuwa anatafutwa na polisi huku akisema hilo limemshangaza akidai kwamba yeye ndiye aliyeshambuliwa na askari huyo.
Vurugu hizo zilitokea baada ya Naibu Spika, Job Ndugai kuamuru kutolewa nje kwa Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe.
Katika vurugu hizo Mbilinyi alibebwa juujuu na polisi hadi nje ya ukumbi huku akiwa hana viatu.
Pamoja na tafrani hiyo, Ndugai alisema wakati akihitimisha kikao cha Bunge kipindi cha asubuhi kuwa amewasamehe wabunge wote waliohusika na kosa hilo la utovu wa nidhamu na kuwaruhusu kurejea kipindi cha jioni kuendelea na Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. Hata hivyo, wabunge wote CUF, NCCR-Mageuzi na Chadema ambao baada ya tukio hilo walitoka nje ya ukumbi, hawakurejea na baadaye walitoa msimamo wa pamoja wakisema hawatashiriki katika mjadala huo.
Msimamo huo ulitolewa na Mbowe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia na Mbunge wa CUF, Habib Mnyaa.
Mbowe alisema wameamua kususia majadiliano hayo kuonyesha msimamo wao wa kupinga kupitisha mambo yasiyo na masilahi kwa nchi.
“Hatuko tayari kushiriki katika uchakachuaji wa Katiba... Matumizi ya nguvu ya polisi kamwe hayatatupatia Katiba nzuri,” alisema. Alisema kambi rasmi ya upinzani inalaani vikali kitendo cha Ndugai kuruhusu Bunge kunajisiwa kwa kuruhusu polisi kuingia ndani kinyume na kanuni.
Mnyaa alisema kitendo cha wadau wa Zanzibar kutoshirikishwa katika kutoa maoni yao katika muswada huo wa marekebisho ni dharau kubwa.
Mbatia alisema Tanzania haiwezi kuingia Uchaguzi Mkuu wa 2015 kwa kutumia Katiba ya sasa kwa sababu tayari kuna mgongano wa kikatiba kati ya Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu alimtaka Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Kuu, (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi kutoa ushahidi kama Rais aliteua wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba kulingana na mapendekezo ya taasisi zao
No comments:
Post a Comment