Kiongozi wa Kambi Rasmi ya upinzani Bungeni, Freeman Mbowe (Chadema), jana aliitaka Serikali itoe tamko iwapo inasubiri hadi polisi waue watoto wao au baadhi ya mawaziri ndipo waunde tume huru ya kuchunguza.
Freeman Mbowe |
Mbowe alihoji hatua hiyo bungeni mjini hapa jana wakati alipokuwa akiuliza swali la nyongeza.
Katika swali la nyongeza jana bungeni, Mbowe ambaye ni Mbunge wa Hai alihoji ni kwa nini Serikali inapata kigugumizi cha kuunda tume huru ya kimahakama ili waweze kuchunguza na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria wale wote wanaohusika na mauaji hayo.
“Baada ya kuhoji jambo hili jana (juzi), naibu waziri alijibu kwa lugha nyepesi sana tena ya kejeli kwamba Serikali haijaona umuhimu wa kufanya jambo hilo ……..mh, Naibu Spika, raia wanauawa na Polisi kwa idadi kubwa na wanaendelea kuuawa kila siku je,mnasubiri hadi watoto wenu wauawe au mawaziri ndipo muone umuhimu huo,” aliuliza Mbowe.
Katika swali la msingi mbunge wa Mbeya Mjini Joseph Mbilinyi (Chadema), alitaka maelezo ya Serikali juu jeshi la polisi kuhusika na mauaji ya mwanafunzi wa Sekondari ya Iyunga, Michael Sikupya ambalo lilithibitishwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Mkoa Mbeya.
Pia mbunge huyo alitaka kujua ni hatua gani zilichukuliwa kwa mauaji hayo, na Serikali inasemaje kuhusu kulipa fidia Familia ya Mzee Sikupya ambaye ni baba mzazi wa marehemu aliyehangaika na suala hilo zaidi ya miaka 10 bila msaada wowote.
Marehemu Michael Sikupya alikufa akiwa hospitali mnamo Desemba 3, 2000 saa 5.20 asubuhi akitokea Kituo cha Polisi ambako alifikishwa yeye na wenzake 53 kwa kosa la kuhusika na vurugu za kuchoma nyumba ya mwalimu mmoja, Novemba 26, 2000.
No comments:
Post a Comment