Saturday, March 23, 2013

WIZARA YA ELIMU YAKANA KUWATAPELI WALIMU


WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi imekana kuhusika kwa namna yoyote kuandika barua ya kuwaita walimu kwenye semina hewa iliyokuwa ifanyike mkoani Morogoro kuanzi Machi 11 hadi 26 mwaka huu.
https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEgYmClo80XRGW2w0L2mdVWGrAlYDYWbLXdasTYKpBwW16g_AqAx7_loqEwDmi4UjL5WfMDfpjGhDjYrncmyygj39r39j3hM849hX9NQcwIJECllePfrW7ssAmwyqxVeJZxsEyOO3hPzqeJU/s1600/Dk+Kawambwa.JPG
Hatua hiyo inakuja baada ya gazeti hili kuchapisha habari kuhusu baadhi walimu kudai kutapeliwa kwa kutumiwa nakala ya mwaliko na hivyo kuingia hasara ya gharama za usafiri na malazi.

Nakala ya barua hiyo yenye Kumb. Na. AHRD /98/789/03S//40 ya Februari 18, 2013 ilisainiwa na mtu aliyejitambukisha kuwa ni O. L. Michael kwa niaba ya katibu mkuu wa wizara hiyo ikiwataka kuhudhuria semina ya kitaifa ya rushwa, ukimwi, uzalendo na uwajibikaji kwa walimu wa Tanzania Bara.

Walimu hao walidai kuwa mbali na barua hiyo, pia walipigiwa simu kupitia namba 0756 018031 kwa msisitizo ikiwaomba kuhudhuria pasipo kukosa.

Akizungumza na gazeti hili jana kwa simu kufafanua suala hilo, Ofisa habari wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Ntambi Bunyazu alitoa sababu tano kuonesha uongo huo uliofanywa na watu wasiojulikana.

Alisema kuwa wizara inapoandika barua kwa mwalimu haiendi moja kwa moja kwake bali kupitia mwajiri wake ambaye ni halmashauri.

Bunyazu aliongeza kuwa hata jina la mwandishi wa barua hiyo O. L. Michael si mtumishi wa wizara na kumbukumbu namba iliyotajwa haipo wizarani.

“Hata Chuo cha Ualimu kilichotajwa cha Kigurunyembe hakiitwi hivyo bali kinajulikana kama Chuo cha Ualimu Morogoro. Halafu barua ingetoka wizarani, Kamishna wa Elimu asingeweza kupewa nakala,” alifafanua.

Barua hiyo ilisema kuwa wizara kwa ushirikiano na Shirika la Misaada la Marekani (USAID), Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) zingefanya semina ya kitaifa kwa walimu wa shule za msingi na sekondari kwa pamoja kuanzia Machi 11 hadi 26 mwaka huu, katika Chuo cha Ualimu cha Kigurunyembe kilichopo mkoani Morogoro.

Ikiwa na muhuri wa wizara, barua hiyo ilionesha kuwa nakala zake zilitumwa pia kwa Kamishna wa Elimu, Mkurugenzi Mkuu TAKUKURU na Mkurugenzi wa USAID na kuambatanishwa na ratiba.
CHANZO: TANZANIA DAIMA

No comments:

Post a Comment