Sunday, March 24, 2013

MTOTO AFA KWA KUTUMBUKIA KISIMANI


MTOTO Kalebi Martine mwenye mwaka mmoja, amefariki dunia muda mfupi baada ya kutumbukia katika kisima chenye urefu wa mita tatu kilichopo jirani na nyumba aliyokuwa anaishi.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Marietha Minagi alisema tukio hilo lilitokea juzi jioni maeneo ya Tabata-Kimanga ambapo mtoto huyo alikuwa anacheza na wenzake kwa jirani yake aitwaye Bilali Ally (43).

Minagi alisema kuwa kwa mujibu wa mtoa taarifa Martine Alexandria (33) ambaye ni baba mzazi wa mtoto huyo, baada ya mtoto wake kutumbukia aliokolewa na watu waliokuwepo katika eneo hilo.

Alisema mtoto huyo alifariki dunia wakati akiwa njiani kumpeleka hospitali na mwili wake umehifadhiwa katika hospitali ya Amana kwa upelelezi zaidi.

Katika tukio lingine, mkazi wa Bunju, Patrick Chuwa (28) amefariki dunia papo hapo baada ya kusukumwa barabarani na kukanyagwa na gari.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni Charles Kenyela alisema tukio hilo lilitokea juzi asubuhi maeneo ya barabara ya Sam Nujoma, Mwenge ambapo Chuwa alikuwa akivuka barabara kutoka kushoto kwenda kulia.

Kenyela alisema kuwa ajali hiyo ilitokea baada ya gari aina ya Toyota Land Cruiser yenye namba za usajili T 126 AXK iliyokuwa ikiendeshwa na Zakiel Mwangike (52) mkazi wa Mbezi Beach akitokea Ubungo kumsukuma Chuwa na kuanguka barabarani.

Alisema Chuwa akiwa bado chini barabarani, alikanyagwa kichwani na gari aina ya DAF yenye namba za usajili T 635 CEK iliyokuwa ikiendeshwa na Selestina Segwa (45) na kusababisha kifo chake papo hapo.

Kamanda huyo alisema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali ya Mwananyala na madereva wa magari yote mawili wameshikiliwa na polisi kwa upelelezi zaidi.

CHANZO: TANZANIA DAIMA

No comments:

Post a Comment