Aidha, Polisi imewataka wananchi kuondoa hofu na kuwapuuza watu wachache, ama kikundi cha watu wanaotumia kipindi hiki cha sikukuu, kuwatia hofu kwa kusambaza ujumbe mfupi wa maneno wenye vitisho kwa watu mbalimbali kwa lengo la kuvuruga amani na utulivu.
Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Senso katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, alisema kitendo hicho cha kusambaza ujumbe ni uhalifu kama uhalifu mwingine na wakibainika hatua za kisheria, zitachukuliwa dhidi yao.
Senso alisema Polisi imejipanga kikamilifu kuimarisha usalama wa raia na mali zao kwa kipindi chote cha sikukuu, kwa kuwataka wananchi kusherehekea kwa amani na utulivu kuazia leo hadi Aprili mosi.
Alisema uzoefu unaonesha baadhi ya watu hutumia kipindi cha sikukuu, kufanya matukio ya uhalifu kutokana na mikusanyiko hiyo ya watu katika maeneo mbalimbali.
Wakati huo huo Polisi imewataka wamiliki wa kumbi za starehe, kuhakikisha usalama na kuzingatia uhalali na matumizi yake katika uingizaji wa watu kulingana na uwezo wake.
Wazazi pia wametakiwa kuwa makini na watoto hasa katika disko toto kuepuka ajali na matukio mengine yanayoweza kusababisha madhara juu yao. Wakati huo huo Ibada ya Ijumaa Kuu kitaifa, inafanyika katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) Usharika wa Dodoma Mjini.
Ofisa Habari wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Mchungaji John Kamoyo alisema kuwa Ibada hiyo itaongozwa na Askofu wa Dayosisi ya Dodoma, Amon Kinyunyu. Ibada ya Misa ya Sikukuu ya Pasaka, itafanyika Jumapili katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Paulo wa Msalaba mjini Dodoma.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Idara ya Mawasiliano wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Anatoly Salawa, ibada hiyo itaongozwa na Askofu wa Jimbo la Dodoma, Mhashamu Gervas Nyaisonga.
No comments:
Post a Comment