Saturday, October 5, 2013

MKUU WA UPELELEZI KUTOA USHAHIDI KUHUSU MADAWA YA KULEVYA

Aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi  wa Polisi mkoani Mbeya, Anaclet Malindisa ambaye sasa hafanyi kazi hiyo, Jumatatu ijayo anatarajiwa kutoa ushahidi wa kesi  ya kusafirisha kilo 34 za  dawa za kulevya  zenye thamani ya Sh1 bilioni  inayowakabili  raia wawili wa Afrika Kusini, Vuyo Jack na Anastazia Cloet.
Washtakiwa hao wanadaiwa kukamatwa Novemba 18, 2010 eneo la Tunduma wakisafirisha dawa hizo kwa kutumia gari  namba   CA 508650, ambapo walifunguliwa kesi  ya makosa ya kusafirisha dawa za kulevya kinyume na sheria za nchi.
Kesi yao ilianza kusikilizwa tangu mwishoni mwa mwezi uliopita na inaendelea mfululizo jijini hapa.
Tayari mashahidi wanne kati ya wanane, wameshatoa ushahidi wao, na kwa mujibu wa Msajili wa Mahakama Mbeya, Aaron Lyamuya, shahidi Malindisa anatarajiwa kutoa ushahidi wake Jumatatu akiongozwa na mawakili wa upande wa mashtaka..
Upande wa mashtaka unasimamiwa na mawakili wa Serikali, Edwin Kakolaki na Basilius Namkambe, wakati washtakiwa wanatetewa na  mawakili Ladslaus Rwekaza na Mary Gatuna.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Mbeya, Noel Choja aliahirisha kesi hiyo, Alhamisi iliyopita  hadi Jumatatu akisisitiza umuhimu wa kuzingatia muda wakati wote wa kesi hiyo, ambayo ni kubwa kuliko kesi nyingi zilizowahi kufanyika mkoani hapa kuhusu dawa za kulevya.

No comments:

Post a Comment