Siku sita baada ya Serikali kuyafungia magazeti ya Mwananchi na Mtanzania kwa madai ya kuandika habari za uchochezi, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeibuka na kueleza jinsi Serikali ilivyowasilisha bungeni Muswada wa Marekebisho ya Sheria mbalimbali wa 2013, ikiwemo sheria ya magazeti ya mwaka 1976 na kuongeza faini kutoka Sh150,000 hadi Sh5 milioni.
Kimesema muswada huo mbali na kulenga kuviminya zaidi vyombo vya habari, pia unalenga kuwabana wananchi katika haki yao ya kutoa maoni, kwamba hata katika kifungu cha kanuni za adhabu imependekezwa faini ya Sh5 milioni kwa watakaoandika maneno ya chuki na uchochezi.
Kutokana na hali hiyo, chama hicho kimeitaka Serikali kuwasilisha jedwali la mabadiliko ya muswada huo kabla ya kuanza kwa vikao vya kamati za Bunge Octoba 16 mwaka huu, kutishia kuwasilisha hati ya dharura marekebisho ya sheria hiyo bungeni kama mabadiliko hayatafanyika.
Kimeeleza kuwa uamuzi huo wa Serikali unalenga kuvifunga mdomo vyombo vya habari, katika kipindi hiki cha mchakato wa kuandika Katiba Mpya na maandalizi ya Uchaguzi Mkuu 2015.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Mkurugenzi wa habari na uenezi wa Chadema, John Mnyika alisema katika muswada huo, hakuna sehemu iliyopendekeza kufanyiwa marekebisho kifungu cha 25 cha sheria hiyo ya magazeti, ambacho kinaipa mamlaka Serikali kuyafungia magazeti, bila kuhitaji utetezi wowote, huku yenyewe ikiwa ndio mshtaki na mtoa adhabu.
Mnyika alisema muswada huo ulisomwa kwa mara ya kwanza katika mkutano wa bunge uliopita na utajadiliwa katika mkutano ujao wa bunge, utakaoanza mwishoni mwa mwezi huu.
“Katika sheria ya magazeti kifungu cha 25 hawajakigusa kabisa, badala yake wamegusa kifungu cha 36 na 37 tena kwa kuongeza faini” alisema na kuongeza;
“Vifungu hivi vinasema kuwa ukiandikwa uchochezi au uongo faini ni Sh150,000, lakini katika mapendekezo wanataka faini iwe Sh 5milioni, wakati huo huo kifungu cha adhabu ya kuyafungia magazeti hakijaguswa kabisa wakati ndio kinachopigiwa kelele na wadau wa habari kuwa hakifai.”
Mnyika alisema kinachofanywa na serikali ni kujaribu kuvibana vyombo vya habari na wananchi kutojadili au kutoa maoni ya jambo fulani, “Vyombo vya habari vinajiendesha katika mazingira magumu, hizi faini zinaongezwa ili iweje.”
Alisema tayari muswada huo umeshachapishwa katika gazeti la serikali tangu Agosti 23 mwaka huu, huku akiwataka wadau wa habari kupaza sauti na kupinga mapendekezo hayo, kushinikiza yachukuliwe mapendekezo ambayo waliwahi kuyatoa miaka ya nyuma juu ya kubadilishwa kwa sheria hiyo.
“Hata katika kanuni za adhabu kifungu cha 55,63 na 63(b), wamependekeza kuongezwa adhabu kwa watu watakaozungumza jambo lolote litakalotafsiriwa kuwa ni uchochezi na chuki, ingawa wamelenga katika masuala ya dini, ukabila na mengineyo, lakini lengo lao kuwabana wasema kweli” alisema Mnyika.
Alisema mapendekezo hayo yanalenga kuwanyima wananchi haki ya kutoa maoni, kwamba kifungu hicho kitawanyima uhuru na haki hata wale watakaokuwa wakitoa hotuba mbalimbali.
“Wanafanya hivi ili watu wasihoji kuhusu Katiba, wasihoji kuhusu uchaguzi mkuu, wasipofanya mabadiliko katika muswada huu tutajua wazi kuwa suala hilo linahitaji hati ya dharura ili kujadiliwa na kupatiwa ufumbuzi bungeni” alisema.
No comments:
Post a Comment