Hali imeendelea kuwa tete ndani ya Jumuiya ya Vijana ya Chama cha Mapinduzi (UVCCM), huku jumuiya hiyo ikitengua uteuzi wa wakuu watatu wa idara zake ambao walikataliwa na Baraza Kuu la chombo hicho lililokutana hivi karibuni, Visiwani Zanzibar.
Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Sadifa Juma Khamis akihutubia wanachama hivi karibuni |
Wakati hayo yakiendelea kuna na taarifa kwamba kumekuwa na mwendelezo wa harakati za kuandaa mkakati wa kumwondoa madarakani mwenyekiti wa jumuiya hiyo, Sadifa Juma Khamis na kwamba vikao vya kupanga mkakati huo vilianza mara tu baada ya mkutano wa Zanzibar.
Watendaji waliosimamishwa ni Wakuu wa Idara za Oganaizesheni, Tumaini Mwakasege, Fedha na Uchumi, Omary Suleiman na yule wa Idara ya Chipukizi na Uhamasishaji, Omary Justus.
Katibu Mkuu wa UVCCM, Sixtus Mapunda alilithibitishia gazeti hili kung’olewa kwa watendaji hao na kwamba kuendelea kwao na majukumu yao kutategemea iwapo watathibitishwa na Baraza Kuu la jumuiya hiyo linalokutana mjini Dodoma Oktoba mwaka huu.
“Sisi tuliomba hawa wathibitishwe kwenye kikao kijacho kwa kuwa kulitokea kidogo mkanganyiko wajumbe wakataka tujadili suala hili kwenye Baraza Kuu lililopita lakini kwa kuwa tulikuwa na ajenda moja tu ya kumthibitisha Katibu tukaomba suala hili lisogezwe mbele,” alisema Mapunda.
Mapunda alisema tayari watendaji hao walikuwa wameanza kazi lakini kutokana na baadhi ya kanuni kujikanganya, wameona ni vyema waache suala hilo mpaka kwenye mkutano ujao.
“Kuna kanuni inayotoa mamlaka kwa Kamati ya Utekelezaji na vilevile Baraza Kuu, kwa hiyo inabidi sasa tuweke kwanza mambo sawa kisha kwenye Baraza Kuu la Oktoba, hawa watathibishwa,” alisema.
Hata hivyo habari ambazo zimelifikia gazeti hili zinasema si rahisi kwa wakuu hao wa idara kurejea kwenye nafasi zao, kwani kitendo cha wajumbe kuwakataa katika kikao cha Zanzibar kinathibitisha kwamba hawana imani nao.
“Kama wajumbe wa Baraza Kuu wangekuwa wanawaamini, shinikizo lingekuwa ni kuwathibitisha, lakini sisi wajumbe ni kwamba hatuwataki. Inabidi Sadifa na kamati yake ya utekelezaji watuteulie watu wengine,” alisema mmoja wa viongozi wa UVCCM wa mikoa ambaye hakutaka kutajwa jina lake.
Suala la uteuzi wa wakuu wa idara za UVCCM pia ni mtihani wa kwanza kwa Katibu Mkuu mpya, Mapunda ambaye mara baada ya kuthibitishwa alionja chungu ya mgogoro katika taasisi ambayo yeye ni mtendaji mkuu wake, pale alipopingwa vikali na wajumbe, alipojaribu kumtetea Sadifa.
Katika mazingira hayo, Mapunda anaweza kujikuta katika mgogoro mkubwa zaidi na wajumbe wa Baraza Kuu, ikiwa atawasilisha majina ya watu walewale waliong’olewa ili wapigiwe kura kwa ajili ya kuthibitishwa.
Habari kutoka katika mkutano wa Zanzibar zilisema kuwa, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana ndiye aliyeokoa jahazi baada ya kuingilia kati mvutano baina ya baadhi ya wajumbe na Sadifa.
Kinana alinukuliwa akikiri kufanyika kwa makosa katika uteuzi wa wakuu wa idara hivyo alishauri suala hilo lipangwe kuzungumzwa katika mkutano wa Oktoba utakaofanyika Dodoma.
Baada ya mkutano wa Baraza Kuu, baadhi ya wenyeviti wa UVCCM wa mikoa, waliripotiwa kuendesha vikao vya siri katika sehemu mbalimbali za jiji la Dar es Salaam, huku kundi kubwa likitajwa kupanga mikakati ya kuhakikisha Sadifa anang’oka.
Miongoni mwa hoja zinazojengwa dhidi ya mwenyekiti huyo ni pamoja na hiyo ya ukiukwaji wa kanuni za uteuzi wa wakuu wa idara, hasa Ibara ya 91 ya toleo la nane la Kanuni za Umoja huo kwa kuwatangaza kabla ya kuundwa kwa Kamati ya Utekelezaji ambayo alipaswa kushirikiana nayo, kabla ya kuridhiwa na Baraza Kuu.
Wajumbe wengi watatumia kusimama kazi kwa watumishi hao kama hoja ya kuthibitisha kuwapo kwa makosa ya kiutendaji, hivyo watahoji iwapo kuna sababu za UVCCM “kuendelea kuwa na mwenyekiti ambaye hawezi kuzingatia kanuni na miongozo katika utendaji wake”.
Tuhuma nyingine ambazo zimekuwa zikizungumzwa dhidi ya Sadifa ni matumizi mabaya ya fedha za Umoja huo pamoja na kukodi walinzi binafsi watano; wawili Tanzania Bara na watatu Zanzibar, ambao wamekuwa wakilipwa na UVCCM.
Jana Sadifa alipotafutwa kuzungumzia tuhuma hizo mpya alisema: “Hayo masuala mimi bwana siyataki, chochote unachopewa wewe andika unavyojua”.
Aliongeza:“Ukiwa na issue (suala) yoyote inayohusu Umoja wa Vijana, wewe mtafute Katibu Mkuu, hata kama hayo mambo yananihusu mimi, wewe usinitafute mimi, mtafute Katibu Mkuu yeye nimempa mamlaka ya kuwa msemaji mkuu.”
Naye Mapunda alipoulizwa kuhusu tuhuma dhidi ya bosi wake alisema hawezi kuzungumzia matumizi mabaya ya fedha kwani hana taarifa.
“Tangu niteuliwe sijamaliza hata siku saba, kwa hiyo niwe muwazi tu kuwa sina taarifa nayo na sasa siwezi kusema fedha zilivyotumika,” alisema Mapunda.
Kuhusu suala la walinzi (mabaunsa),Mapunda alisema hao si sehemu ya watumishi aliokabidhiwa na kwamba jumuiya hiyo haina waajiriwa wa aina hiyo.
No comments:
Post a Comment