Sunday, September 8, 2013

WACHEZAJI WA TANZANIA NJE YA NCHI WAPOTEZA MASHIKO

Nguvu ya soka ya nchi fulani huonyeshwa kwa njia mbalimbali, mojawapo ikiwa ni idadi na aina ya wachezaji wake wanaocheza kwenye ligi kubwa duniani.

Mchezaji kupanda umaarufu hadi kuweza kuvuka mipaka ya nchi na kucheza katika nchi zilizo juu ya ile yake ni dhihirisho la umahiri wake.
20130908-183438.jpg
Kadhalika huwa taswira ya hali ilivyo nyumbani, ndiyo maana daima limekuwa jambo la kusisimua na kufurahisha tunaposikia mmoja wa wachezaji wa Kitanzania wamekwenda nje kucheza soka ya kulipwa.

Hiyo kwa upande mmoja huwa kuitangaza soka yetu, jina la nchi yetu na kujifunza makubwa ili hatimaye arudi kuchangia tunu zake katika Taifa Stars.

Lakini upande wa pili ni kwamba mchezaji huyo hufaidika kiuchumi, kwa sababu kama atakwenda kwenye nchi iliyo juu kisoka, maslahi yatakuwa makubwa zaidi kuliko Tanzania.

Ndiyo maana tunaona wachezaji wa Brazil wanakwenda Hispania, wanakuja Uingereza na wengine wengi wa asili za Afrika wanatamba Ligi Kuu ya England, Ufaransa na kwingineko.
Ni sawa na kusema mchezaji huyo anapata ‘ulaji’ zaidi, kwa kufuatisha msemo wa Kiingereza kwamba wamefuata malisho bora zaidi.


Kwa mchezaji kupata kandarasi ya kucheza soka Ulaya, maana yake ni kupandishwa daraja na kimo cha umahiri wake wa soka na wa nchi yake.

Binafsi naona mchezaji hufaidika sana anaposajiliwa na kucheza katika klabu za Ulaya, ambazo hakuna ubishi kwamba katika vigezo vya soka zipo juu kimaendeleo.
Ni kwa sababu hiyo hufurahisha habari zinapotoka kwamba mchezaji fulani amefanikiwa na anakwea pipa kutoka Tanzania kuja Ulaya ama kwa ajili ya kusakata soka.
Katikati ya miaka ya ’70 tulikuwa na akina Kassim na Sunday Manara waliopata kucheza kwenye ligi za Austria.


Katika miaka ya ’80 tulikuwa na wachezaji kama Zamoyoni Mogella, hayati Hamis Gaga na Hamis Kinye waliofanikiwa kuvuka mpaka na kwenda nchini Kenya kuchezea Shabana FC na AFC Leopards.

Wachezaji wengine walijaribu bahati yao Mashariki ya Kati, nao ni akina Yanga Bwanga, Thueni Ali na Mohamed Salim na wakaweka makazi yao huko baada ya muda wao wa soka kumalizika.

Kutokana na kukua kwa uwazi na ujio wa matangazo ya mpira kwa televisheni katika pembe mbalimbali za dunia, baadhi ya wachezaji wa Taifa Stars wamefanikiwa kupata nafasi za kucheza kwenye ligi za daraja la pili Ulaya. Kwa daraja la pili si dhalili bali ni hatua moja mbele na ya kuanzia kupanda.

Siku hizi si jambo la ajabu wala haichukui muda mrefu kusikia kwamba mchezaji wa Taifa Stars amesafiri hadi Ulaya au mabara mengine kwa ajili ya kufanyiwa majaribio kabla ya kusaini mkataba wa kucheza huko.

Kwa muda sasa, idadi ya wachezaji ambao walikuwa wakitoka Tanzania kuingia Ulaya ilikuwa ikipanda, na hizo ni habari njema.

Tunaona fahari kwa hali hiyo na kuomba wimbi hili lizidi kwa wachezaji zaidi kuibuka, kupata nafasi za kwenda kucheza katika nchi zilizoendelea kisoka.
Henry Joseph Shindika aliondoka Simba mwaka 2009 akaenda Norway alikotia saini kuchezea klabu ya daraja la pili.

Wachezaji wengine walioweza kupata nafasi ya kuvuka mipaka yetu na kwenda kupata ulaji zaidi ni Haruna Moshi na Nizar Khalfan.

Baada ya miaka minne, Shindika amepanda ndege kurudi nyumbani na kujiunga tena na Simba, pengine ndoto zake za kuendelea kucheza Ulaya zimeisha.
Itakumbukwa kwamba Shindika aliondoka nchini akiwa Nahodha wa Timu ya Taifa, kiungo mwenye kipaji na rekodi nzuri, lakini inasikitisha kuona anarejea nyumbani kimya kana kwamba hakuna kilichotokea.

Shindika, kama wenzake kadhaa waliotarajiwa kustawi, kung’aa na kupanda hadi kwenye klabu za hadhi za juu zaidi kama Wakenya wawili Mcdonald Mariga na Victor Wanyama walivyofanya.

Norway ilitakiwa itumiwe na Shindika kama manati ya kumrusha kwenye klabu kubwa, hivyo kuwa mtu wa kupigiwa mfano na wachezaji aliowaacha nyumbani.
Ligi ya Norway ina wachezaji wengi wa Afrika Magharibi ambao huitumie kujiboresha kisoka. Inasikitisha kwamba Shindika ametumia miaka yake minne na kupiga abautani kurudi mwanzo.

Wafuatiliaji wa karibu wa soka ya nyumbani lazima watakuwa wametambua hali ya wachezaji wetu kuanza kurejea nyumbani baada ya muda mfupi tu Ulaya na kwingineko.
Inaudhi zaidi kwa sababu aina ya wachezaji wanaorudi wakiwa hawana tena viwango wakati ndio waliokuwa lulu miongoni mwa wanasoka wetu waliobaki nyumbani. Ndiyo maana Shindika alikuwa nahodha.

Nizar Khalfan aliondoka Moro United akaenda nchini Canada kuchezea Vancouver White Caps kicha akarudi. Alikuwa hakosekani kwenye kikosi cha Taifa Stars kabla ya kuondoka, lakini hata mtoto mdogo sasa atakwambia kuwa hawezi kurejea katika timu ya taifa.
Alicheza ng’ambo kwa misimu kadhaa kabla ya kurejea na kushindwa kurejesha namba yake Taifa Stars. Wakati mwingine huonekana hata akiwa na wakati mgumu kupata namba katika kikosi cha kwanza cha Yanga anakocheza.


Mchezaji mwingine katika orodha yetu ndefu ya wachezaji walioshindwa kufikia malengo ni Haruna Moshi, ambaye hata baada ya kurudi hakuweza kupata namba kwenye klabu yake, akaanza kuingia mechi za mchangani, akikizika kipaji chake ambacho hakikuwa cha kawaida.
Wachezaji wote waliorejea walitakiwa kuwa na nyota inayong’aa kwa siku zijazo kwa sababu wengi walikuwa na umri wa miaka 20 na ushee, hivyo walitarajiwa kukaa ng’ambo wakicheza kwa mafanikio kwa miaka walau saba kisha warudi nyumbani kula pensheni baada ya kustaafu.


Orodha ni ndefu na inawajumuisha akina Athumani Machupa, Musa Mgosi, Athumani China, Danny Mrwanda na wengine waliosajiliwa Ulaya kimya kimya na hawakutaka kurejea nyumbani waziwazi.

Kurejea nyumbani kwa wasakata soka wetu hawa waliokwenda nje waking’aa kunawakwaza wachezaji makinda wetu.

Akili na mioyo ya wachezaji wanaofanya vizuri inaathiriwa, na hawa wanaowika na kushindwa kupata wa kuwapigia mfano ni akina Salum Abubakar, Haruna Chanongo na wengineo.

No comments:

Post a Comment