Popote utakapotulia na kutazama pambano lolote litakaloonyeshwa
moja kwa moja au kwa marudio, kupitia kituo cha Televisheni cha Azam
(Azam TV), usiwe na shaka, utaliona pambano maridadi.
Weka soda yako sebuleni kando kisha watazame Jerry
Santo na Amri Kiemba wakichuana katikati ya uwanja wowote ule wa soka
nchini huku kamera nane za Azam TV zinazorekodi pambano lao zikiwachukua
kwa umaridadi.
Kamera nane zamrekodi mchezaji.
Katika pambano lolote litakaloonyeshwa na Azam TV
kutakuwa na kamera nane uwanjani. Huu ni wastani wa juu wa idadi ya
kamera zinazopaswa kuonyesha kwa ufasaha pambano lolote la soka ingawa
katika mechi za ligi nyingine au michuano mingine kunakuwa na kamera
zaidi za kuonyesha mbwembwe mbalimbali.
Kamera hizi ni ghali zikiwa zimegharimu kiasi cha
kuanzia dola 180,000 hadi dola 200,000 kwa kila moja. Ndani ya kila
kamera kuna mchanganyiko wa mashine ya Sony huku lensi ya kuvutia
matukio kwa ufasaha ikiwa ni ya kampuni ya Cannon. Kamera mbili zitakuwa
zinakaa katika kila nyuma ya lango la uwanja. Kamera hizi mbili zina
kishikilio kirefu na kuifanya ining’inie katika eneo lote la nyuma ya
lango kama tunavyoona katika mechi za Ligi Kuu England na michuano
mbalimbali.
Katika pande mbili za uwanja, karibu na benchi la
kila timu kutakuwa na kamera mbili ambazo watu wanaorekodi mpira
wataweza kukimbia nazo huku na kule kwa ajili ya kutokana matukio
yanayoendelea katika upande wa kulia na kushoto kuanzia pale anapokaa
mwamuzi wa akiba.
Kamera ya nne ni ile iliyosimama katikati ya
uwanja, karibu na mwamuzi wa akiba. Kamera hiyo huwa inasimama ilipo na
haisogei. Dhumuni kubwa ni kuzivuta kwa karibu sura za wachezaji au
mwamuzi inapohitajika.
Jukwaani kuna kamera kubwa zaidi, pengine kuliko
zote. Mtambo huu unarekodi mechi yote kwa juu na ni nzuri kwa mwelekeo
mzima wa ‘muvu’ kwa timu zote mbili. Lakini pia kando ya kamera hii kuna
kamera nyingine kubwa ambayo nayo inadaka kwa haraka matukio ya ndani
ya uwanja.
Pia bado kuna kamera ya saba ya mtu ambaye
anazunguka katika kando ya uwanja kwa ajili ya kuchukua mahojiano kabla
ya mechi, wakati wa mapumziko na mechi ikiisha. Kamera zote hizi saba
zina uwezo wa kurekodi na kuvuta kwa karibu tukio lililo umbali wa mita
400 kutoka zilipo. Hii ni sawa na muunganiko wa viwanja vinne vya
mpira!
OB Van ya kisasa zaidi barani Ulaya.
Kamera hazina kazi yoyote kama huna OB (Outside
Broadcasting)Van ya kisasa. OB Van ni gari linalokamata matangazo
uwanjani na kwingineko nje ya studio kutokea katika kamera na kurusha
katika setalaiti iliyo hewani. OB Van ya Azam TV ni ya kisasa zaidi
ambayo ni zaidi ya OB Van zinazotumiwa na kampuni nyingine za Afrika.
Ikiwa imegharimu kiasi cha Euro 4 milioni, OB Van
hiyo ililetwa nchini na Kampuni ya Broadcast Solutions ya Ujerumani
chini ya mhandisi wake maarufu, Armando Santos ambaye ameondoka nchini
jana Ijumaa baada ya kuendesha mafunzo maalumu ya jinsi ya kuitumia OB
Van hiyo.
Santos anakiri kwamba hiyo ni OB Van ya kisasa zaidi barani
Ulaya na kampuni yao imekuwa ikipokea oda mbalimbali kwa ajili ya
kutengeneza OB Van ambazo zimekuwa zikitumiwa katika michuano mbalimbali
duniani kote.
“Tumekuwa tukisambaza OB Van ambazo zimetumiwa
katika kombe la dunia lililopita, Olimpiki, Ligi Kuu Ujerumani, Euro
2012 na michuano mbalimbali duniani, si lazima soka tu. Tunatengeneza OB
Van kutegemea na mahitaji ya mteja,” anasema Armando ambaye ameanza
kazi hii tangu mwaka 1996.
Ndani ya OB Van hii kuna vyumba vinne vyenye kazi
mbalimbali. Ni kama uko ndani ya nyumba yako tu. Kuna chumba cha kupokea
picha zote kutoka kamera saba uwanjani ambacho kina runinga zaidi ya
10. Kuna chumba cha mchanganya picha ambacho kina runinga zaidi ya 10,
kuna chumba cha mtu wa sauti ambacho kina runinga chache.
Kuna tofauti yoyote na Ulaya?
Nilimuuliza swali hili Santos kama kuna tofauti
yoyote ya ziada baina ya kuonyesha mechi Ulaya na itakavyokuwa Azam TV.
Santos anakiri kwamba Ulaya kuna kamera nyingi zaidi uwanjani, lakini
ambazo hazina kazi kubwa zaidi ya zile saba muhimu.
“Wakati mwingine kunakuwa na kamera nyingi zaidi.
Fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2012 kulikuwa na kamera 68.
Lakini achilia mbali zile saba za msingi, hizi nyingine zote zilikuwa za
kumrekodi mchezaji mmoja mmoja kwa kila anachofanya uwanjani. Nyingine
ni kwa kila kocha. Hazifanyi kazi nyingine.
Kuna Kamera inamrekodi Didier Drogba basi,
unamrekodi yeye tu hata kama hana mpira. Zile saba ndizo zinazofanya
kazi za msingi. Zipo nyingine kwa ajili ya kurekodi watu maarufu tu
walio jukwaani au vituko vya jukwaani.
“Lakini hata hizi saba zilizopo, utagundua kwamba
tuna kamera tatu zinazoweza kuibia matukio mbalimbali ya majukwaani na
sehemu nyingine.”
Mechi za mikoani
Wakati OB Van moja ikiwa imewasili, OB Van
nyingine inatarajiwa kuingia muda wowote katika Bandari ya Dar es Salaam
ikitokea Ujerumani. OB Van hii ya kisasa, kama ilivyo ya awali, itakuwa
na kazi ya kurekodi mechi za mikoani na itakuwa na kamera nyingine saba
za kurekodi mpira mwingine kwa ubora ule ule tu.
Fitina nyingine itakayokatwa ni ile ambayo kila
uwanja utakuwa na kamera moja kubwa inayorekodi moja kwa moja mechi
nyingine 13 au 12 zitakazokuwa zinaendelea katika viwanja mbalimbali vya
Ligi Kuu.
Kamera hizo zitakuwa na kadi maalumu ambayo
itakuwa imeunganishwa moja kwa moja na OB Van ambayo itakuwa imebaki Dar
es Salaam ikiendelea kuonyesha mechi ya siku. Watu wa kwenye OB Van
watakuwa wanaziangalia moja kwa moja mechi nyingine na wanaweza
kuchomekea bao au kadi nyekundu iliyoonyeshwa katika uwanja mwingine
kama wa Mkwakwani kama Coastal Union imepata bao la kuongoza. Bao hilo
litaonekana moja kwa moja katika pambano mfano la Azam na Simba likiwa
linaendelea Uwanja wa Taifa au Chamanzi.
Pia, mechi za mikoani zitaanza kurudiwa kuonyesha muda wa usiku
kwa ajili ya kukata mzizi wa fitina wa kile ambacho kimeendelea mikoani.
Huu ni mwisho wa fitina!
Wazungu wamejaa Chamanzi
Nilibahatika kushuhudia mazoezi ya watu
watakaokuwa wanarekodi mechi hizo. Shughuli wanayo. Armando Santos
anaondoka nchini akiwa ameacha Wazungu zaidi ya watano kutoka Afrika
Kusini ambao wana kazi ya kuwafundisha Watanzania kadhaa ambao
wamebahatika kurekodi mechi za Azam TV kutokana na weledi wao.
Mpaka kufikia mwanzoni mwa Oktoba ambapo Azam
wataanza kuonyesha mechi hizo, inatazamiwa kwamba kundi hilo litakuwa na
weledi wa kutosha wa kuanza safari ndefu ya kuonyesha mechi za Ligi Kuu
Bara kwa walau miaka mitatu ya kuanzia kwa mkataba huo.
No comments:
Post a Comment