Sunday, September 8, 2013

SIRI ILIYOPO KWA WATUMIAJI WA MADAWA YA KULEVYA

Mitaani vijana wanasikika wakisifia bangi inayouzwa na Khamis (siyo jina lake halisi). Wanashawishiana kwenda kununua kwa mtu huyo wakisifu kuwa ina ‘stimu’ nzuri isiyokwisha haraka tofauti na za mtu mwingine (wanamtaja kwa jina).
Mhadhiri na Mtaalamu wa Saikolojia katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Kitila Mkumbo
Kwa yule ambaye si mzoefu wa kutumia vilevi hivi huwezi kuuziwa, kwani kuna ishara ambazo hupeana ili kujua kama huyu ni mnunuaji au polisi.
Zipo ishara mbalimbali wanazozitumia wakati wa kununua bangi hizi, mfano ukiwa na gari usiku utatakiwa kuzima taa za nje na kuwasha za ndani. Muuzaji akiona hivyo tu anajua kuwa aliyefika ni mteja wake.
Aidha hata namna wanavyopeana pesa ni tofauti, muuzaji hakabidhiwi mkononi badala yake unaiweka tu kwenye kiti cha gari, naye akifika anaweka mzigo chini na kuchukua pesa yake.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umegundua kuwa, huu ndiyo mwanzo wa watumiaji wa bagi kuingia katika matumizi ya dawa za kulevya.
Aidha hata namna wanavyopeana pesa ni tofauti, muuzaji hakabidhiwi mkononi badala yake unaiweka tu kwenye kiti cha gari, naye akifika anaweka mzigo chini na kuchukua pesa yake.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umegundua kuwa, huu ndiyo mwanzo wa watumiaji wa bangi kuingia katika matumizi ya dawa za kulevya.
Wauza dawa za kulevya matajiri nchini, wanafanya hila kuhakikisha vijana wadogo wanaingia kwenye utumiaji wa dawa za kulevya, ili watengeneze wateja endelevu wa biashara yao.
Inasemekana kuwa kauli mbiu wanayoitumia ni ‘Get Them While They’re Young’, wakimaanisha kuwa wawaingize kwenye matumizi ya dawa za kulevya wakati wakiwa bado wadogo, ili wanapofikia umri wa kuingiza kipato wawafaidishe wao kwa kununua ‘unga’.
Uchunguzi unaonyesha kuwa matajiri hawa wakati mwingine huwalipa wauza bangi na kuwapa dawa za kulevya bure, ili wazichanganye wakiamini kuwa wanatengeneza wateja wengi kwa wakati mmoja.
Kwa wasiovuta bangi wamekuwa wakichanganyiwa katika sigara na matendo kama haya hufanyika zaidi katika klabu za usiku na waathirika wakubwa wa njia hii ni wasichana.
“Wasichana hudanganywa na wapenzi wao wakiambiwa vuta kidogo, ni nzuri nao hujikuta wakijaribu na kurudia tena kwa kuwa kile wanachovuta si sigara ya kawaida, mwisho wa siku huingia kwenye ‘uteja’” kinasema chanzo cha habari.
Mfano wa watu walioingizwa kwenye utumiaji wa dawa za kulevya bila kujua ni wasanii wa muziki wa Tanzania, akiwamo Rehema Chalamila, maarufu Ray C. Akisimulia mkasa wake Ray C alisema rafiki yake wa kiume, ndiye aliyemuingiza kwenye utumiaji wa dawa za kulevya bila yeye kujua.
Ray C alisema mpenzi wake alikuwa akimchanganyia katika sigara bila mwenyewe kujua.
Wasanii kama Q Chief, Mark II B, Chid Benz wamewahi kukiri kutumia dawa za kulevya, huku kila mmoja akisema kuwa aliingizwa katika ulevi wa aina hiyo bila kujua.
Akihojiwa na kituo cha kimoja cha redio msichana raia wa Kenya, alisimulia sababu za kutumia dawa za kulevya, kuwa rafiki yake wa kiume alimshawishi kuvuta bangi ambayo ilikuwa imechanganywa na aina nyingine ya dawa za kulevya (unga).
Msichana huyo alisema bangi aliyopewa na rafiki yake ilikuwa na ladha tofauti na nzuri, ikilinganishwa na bangi zingine na kwamba alipokuwa akiikosa bangi hiyo viungo vyake vya mwili vilikuwa vinachoka.
Alisema baada ya muda mrefu ndipo aligundua bangi hiyo ilikuwa imechanganywa na dawa za kulevya na kwamba kuanzia hapo akawa mtumiaji wa dawa za kulevya.
Mhadhiri na Mtaalamu wa Saikolojia katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Kitila Mkumbo amesema kwa mpango huo taifa litakuwa na watuamiaji wengi wa dawa za kulevya katika miaka ijayo, kama tabia hii haitadhibitiwa kutokana na urahisi wa kuwashawishi vijana wadogo.
Anasema vijana wa miaka 11 hadi 18 ni rahisi kushawishika, kwa kuwa katika umri huu hujaribu kufanya kila kitu kwa lengo la kujifurahisha.
“Kama kweli wanafanya hivi hii nchi itakosa nguvu kazi ya vijana katika siku za usoni, kwa kuwa vijana katika umri huu wanafanya kila kitu bila kujua faida au hasara zake, katika kipindi hiki cha kubalehe ,” anasema.
Naye Meneja wa Fedha na Rasilimali katika shirika la vijana lijulikanalo kama Youth of Africa, Avitus Mushumba amesema ni wajibu wa kila Mtanzania kutumia nafasi aliyonayo kupambana na uharamia huu kwa kuwa ni kweli vijana wengi wanaingizwa katika matumizi ya dawa za kulevya bila kujua.
“Watanzania wanapaswa kuliwekea kipaumbele hili suala la vita dhidi ya dawa za kulevya, kama hatutashikamana taifa litateketea kwa kuwa vijana wengi wataingia huko,” anasema Mushumba.
Naibu Waziri wa Habari Vijana Utamaduni na Michezo, Amos Makala amesema wao kama wizara hawana taarifa na mbinu mpya ya kuingiza vijana kwenye utumiaji wa dawa za kulevya.
Hata hivyo Makala amesema wazazi wanapaswa kuwa karibu na watoto wao na kuwaelewesha mambo yanayohatarisha maisha yao, ikiwemo haya ya matumizi ya dawa za kulevya.
“Tunawashukuru watu kama nyie ambao mnaisaidia serikali kufichua maovu, lakini tusaidiane kwenye vita hii, ili tuwanusuru watoto wetu,” alisema Makala.
Naye Kamanda wa Kikosi cha Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya, Godfrey Nzowa alisema lengo lao ni kuwaangamiza wafanyabiashara wa dawa za kulevya.
“Hawa wana mbinu za kila aina, lakini hatutawaacha, tunataka kusafisha kabisa kwani dawa hizi zimewaathiri watu wengi na kupunguza nguvu kazi ya taifa, hivyo sisi kama watu wenye dhamana tutahakikisha tunashinda,” alisema Nzowa.
Alisema wafanyabiashara wamekuwa wakibuni mbinu mbalimbali ili kuwashinda, bila kujua nao wameunda mtandao mkubwa katika nchi zote za Afrika.
“Wanajaribu kufanya hila mbalimbali ili kudhoofisha juhudi zetu. Hakika sasa mwisho wao umefika kwani tumejizatiti kwani nasi tuna mtandao mkubwa,” alisema Nzowa.
Akizungumza wakati wa kuahirisha mkutano 12 wa Bunge mjini Dodoma, Waziri Mkuu Mizengo Pinda alisema kumekuwa na changamoto ya uharakishaji wa kesi za dawa za kulevya hali inayoifanya Serikali kufikiria kuwa na mahakama maalumu.
Pinda alisema kati ya mwaka 2010 hadi Julai, 2013, kuna kesi 368 mahakamani zinazohusu dawa za kulevya, kati ya hizo, 91 zilimalizika kwa watuhumiwa kufungwa na wengine kutozwa faini.
Takwimu za tiba kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, zinaonyesha kuwa watumiaji wa dawa za kulevya waliofika katika vituo vya tiba katika kipindi cha 2008 hadi 2011, walikuwa 20,626.
Kwa mujibu wa Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya, kilo 754.57 za heroin, kilo 356.30 za cocaine, kilo 210,335.80 za bangi na kilo 44,570.80 za mirungi zilikamatwa katika kipindi cha kuanzia mwaka 2008 hadi mwaka 2013.

No comments:

Post a Comment