Saturday, September 7, 2013

KOCHA WA YANGA ADANGANYIKA

Kocha Mkuu wa Yanga, Ernie Brandts
Kocha wa Yanga, Ernie Brandts wakati anaondoka kwenda likizo Ulaya aliacha maagizo kwa Kamati ya Usajili ya klabu hiyo kumsajili beki Salvatory Ntebe wa Mtibwa. Hata hivyo, badala yake, Kamati ya Usajili ikamsajili Rajabu Zahir kutoka Mtibwa.

Mmoja wa viongozi wenye ushawishi mkubwa Yanga aliidokeza Mwanaspoti wiki hii kwamba: “Unajua kocha wakati anaondoka kwenda likizo baada ya ligi kumalizika alitaka Kamati ya Usajili imsajili beki wa Mtibwa Sugar yule mrefu mwenye rasta (akimaanisha Salvatory Ntebe) na si huyu wa sasa Zahir (Rajabu).”
Kiongozi huyo alisema Rajabu Zahir amesajiliwa kimakosa kwani chaguo sahihi la Brandts lilikuwa ni yule beki wa kati wa Mtibwa, Salvatory Ntebe mwenye rasta aliyewafunga Simba.
“Ndiye aliyemvutia kocha kwenye mechi ya ligi dhidi ya Simba iliyofanyika Uwanja wa Taifa. Katika mchezo huo Mtibwa walishinda 1-0, bao hilo pekee likifungwa na Ntebe.”
Alisema kuwa tangu hapo, Brandts alianza kumsifia beki huyo na kutaka huduma yake kabla ya kupendekeza kamati ya usajili kumsajili ili asaidiane na Kelvin Yondan ‘Vidic’ na Nadir Haroub ‘Cannavaro’
Hata hivyo, alieleza kuwa Brandts aliporejea na kukutana na kamati hiyo aliambiwa Mtibwa waligoma kumtoa na kutaja gharama kubwa, ndipo walipoamua kumsajili Zahir.
Brandts alipoulizwa na Mwanaspoti kuhusu hilo alishangaa mwandishi amejuaje? Lakini akagoma kutolea ufafanuzi kwa madai si wakati wake na hakuna kiongozi yeyote wa kamati ya usajili aliyetaka kupokea simu kutamka lolote.
Hata hivyo, Brandts amesoma uwezo wa Zahir na kumwingiza kwenye programu yake huku akimsifia kama mchezaji mdogo anayependa kujifunza na kujituma zaidi.
Zahir ni miongoni mwa wachezaji waliofanya vizuri msimu uliopita lakini Ntebe anamzidi kwa kitu kimoja tu. Uzoefu na utulivu uwanjani

No comments:

Post a Comment