Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania, (JWTZ) limeeleza kuwa
Tanzania haikupeleka kikosi cha jeshi hilo kwenye Kikosi cha Kulinda
Amani cha Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo
(DRC)(Monusco) kwa ajili ya kupigana na Rwanda, bali kusaidia kulinda
amani.
Ufafanuzi huo umekuja siku mbili baada ya Rais
Jakaya Kikwete kukutana na Rais Paul Kagame wa Rwanda, kufuatia baadhi
vyombo vya habari vikiandika habari jinsi JWTZ kilivyopambana na waasi
wa Kikosi cha M23 na kukisambaratisha, sambamba na malumbano kati ya
Tanzania na Rwanda.
Askari wa Tanzania na wale wa Afrika Kusini wako DRC kwa kazi ya kulinda amani. Malawi bado haijapeleka majeshi yake.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, msemaji
wa JWTZ, Meja Erick Komba alisema,“Kikosi cha Tanzania kilichopo DRC ni
sehemu ya Kikosi cha Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika
(SADC), kilichotoa mchango wake katika Jeshi la Umoja wa Mataifa
(Monusco) na kinafanya kazi chini ya komandi ya Monusco.”
Alifafanua kuwa kazi ya kikosi hicho ni kuzuia
waasi kujitanua, kuvunja nguvu yao pamoja na kuwapokonya silaha, huku
akisisitiza kuwa sio kweli kuwa Tanzania ilikuwa ikipigana na Rwanda au
waasi wa M23, kama ambavyo imekuwa ikielezwa.
“Ridhaa ya kikosi chetu kwenda DRC ilikubaliwa pia
na Rwanda, nchi ambayo ni mwanachama wa nchi za maziwa makuu. Aidha
Rwanda imesaidia kuruhusu kikosi cha Tanzania kupitisha watu,vifaa na
zana nchini kupitia nchi hiyo kwenda DRC,” alisema.
Alisema kuwa vikosi hivyo ambavyo mbali na Waasi
wa M23 pia vimekuwa vikipambana na vikosi vya Waasi vya ADF na FDLR,
kwamba bado vinaendelea kulinda amani nchini DRC na kama kunaibuka
mapambano navyo hulazimika kujibu mapigo.
Kikosi cha Munusco kilianza kupambana na waasi,
Agosti 27, mwaka huu na askari wa JWTZ, Khatibu Mshindo alikuwa miongoni
mwa waliouawa kwa kupigwa bomu na M23 Mjini Goma ulioko Mashariki mwa
DRC. baada ya kuzuka mapigano makali.
No comments:
Post a Comment