Maoni ya Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala kuhusu
Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa 2013 yanadaiwa kuwa
yalibadilishwa dakika za mwisho na kwamba suala hilo ndicho kiini cha
vurugu zilizotokea bungeni mjini Dodoma juzi.
Gazeti la Mwananchi limefanikiwa kuona nakala inayodaiwa
kuwa ni maoni ya awali ya kamati hiyo ambayo yalikuwa na mapendekezo
yanayotaka kuwapo kwa marekebisho kadhaa kwenye muswada huo, tofauti na
yale yaliyowasilishwa bungeni juzi na Mwenyekiti wa Kamati, Pindi Chana.
Jumatano na Alhamisi wiki hii kulikuwa na mvutano
mkubwa bungeni kiasi cha wabunge wa upinzani kutoka vyama vitatu vya
NCCR -Mageuzi, Chadema na CUF kuungana na kususia mjadala kuhusu muswada
huo.
Imedokezwa kuwa mvutano mkali kuhusu muswada huo
ulianza ndani ya kamati hiyo wakati wajumbe wake ambao ni wabunge wa CCM
walipotumia wingi wao kubadili maoni ya awali na kuweka maoni mapya,
hatua ambayo inadaiwa kuwa ilikuwa na msukumo wa Serikali nyuma yake.
Ndani ya Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na
Utawala, wabunge wa upinzani ambao kwa idadi yao ni wachache walishindwa
kuzuia mabadiliko hayo ya “lala salama” yanayodaiwa kuwa yaliwekwa
Septemba 2, mwaka huu, hivyo waliazimia kuhamasisha wabunge wote wa
upinzani kupinga marekebisho hayo kutokana na sababu kuu mbili.
Sababu hizo ni kutofanyika kwa mikutano ya wazi
kwa umma (public hearing) upande wa Zanzibar na hatua ya kuwapo kwa
mapendekezo ya Rais kurundikiwa madaraka makubwa ya uteuzi wa wabunge
kutoka asasi za kijamii watakaoingia katika Bunge la Katiba.
Habari zinasema wakati fulani Naibu Spika wa
Bunge, Job Ndugai alitembelea kamati hiyo wakati ikiedelea na vikao
vyake na kukuta mvutano mkali kuhusu suala la marekebisho ya sheria ya
sheria hiyo na alishauri kwamba pale ambapo hawataweza kuelewana basi
wasubiri uamuzi ndani ya Bunge.
Jana gazeti hili lilimtafuta Chana kupitia simu
yake ya mkononi na baada ya kumweleza kuhusu madai hayo alisema:
“Tafadhali sana kwa sasa niko kwenye kikao, kwanza simu yako nimeipokea
kwa heshima tu, tutafutane wakati mwingine”.
Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe
alikiri kwamba kulikuwa na mapendekezo ya kuongeza idadi ya wabunge na
namna ya kuwapata, lakini Serikali iliyakataa katika hatua ya
majadiliano kabla ya suala hilo kufikishwa bungeni.
Tofauti ya maoni
Nakala ya taarifa ya awali ilipendekezwa kuwa
katika kuteua wajumbe 166 wa Bunge la Katiba, Rais azingatie kikamilifu
mtiririko wa mapendekezo ya kila kundi lililoainishwa katika kifungu cha
(1) (c).
“Na endapo Rais hatazingatia mapendekezo ya kundi
mojawapo, Rais afanye mrejesho kwa taarifa kwa kundi husika juu ya
sababu za kutozingatia mtiririko wa mapendekezo yaliyowasilishwa kwake,”
inasema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo inaongeza kuwa kamati hiyo ilikuwa na maoni kwamba
makundi mengine ya kijamii yaongezwe katika kifungu cha 22(1) (c) cha
sheria mama, ili kupanua wigo wa uwakilishi mpana katika Bunge la
Katiba, hivyo kuongeza idadi ya wabunge hao kutoka idadi ya awali 166
hadi kufikia 201.
“Kamati inashauri kuwa idadi ya wajumbe iwe 201
badala ya idadi ya wajumbe 166 iliyotajwa katika sheria mama, ili kupata
idadi ya wajumbe watakaounda Bunge Maalumu la Katiba,” inasomeka
taarifa hiyo.
Hata hivyo, maoni hayo yanatofautiana na yale
yaliyowasilishwa bungeni juzi na jana, kwani yanaonyesha kwamba kulikuwa
na majadiliano na mashauriano baina ya kamati na Serikali, hivyo
ilikubaliana kuwa “Rais apewe mamlaka ya kufanya uteuzi wa wajumbe Bunge
la Katiba” huku idadi ya wabunge wa kuteuliwa wakibaki 166.
Kifungu hicho kiliondoa haki ya kila taasisi
kuteua jina la mjumbe wake katika Bunge hilo na badala yake,
ikapendekezwa kuwa Rais atapelekewa matatu ili ateue moja kati ya hayo.
Hata hivyo, jana wakati Bunge lilipoketi kama
kamati kwa ajili ya kupitia vifungu vya marekebisho ya muswada huo,
Serikali iliwasilisha marekebisho ya nyongeza ambayo yanazitaka asasi za
kiraia ziteue majina tisa na kati ya hayo Rais anaweza kuteua jina moja
na kama asiporidhika anaweza kuteua mtu kutoka nje ya orodha hiyo.
Kuhusu suala hilo Chikawe alisema: “Tangu awali
ilikuwa inaonyesha wajumbe ni 166. Ni kweli Kamati ilipendekeza wajumbe
hao waongezeke hadi 201 lakini pendekezo hilo halikukubaliwa, ikabakia
wajumbe watakuwa 166.”
Ushiriki wa Zanzibar
Itakumbukwa kuwa Kamati ya Katiba, Sheria na
Utawala ilipewa wiki nne za kuendesha vikao vyake kabla ya kuanza kwa
Mkutano wa 12 wa Bunge uliomalizika jana, tofauti na kamati nyingine
ambazo zilipewa wiki mbili.
Baadhi ya wabunge (hasa wa upinzani) wanasema
madhumuni ya kupewa muda huo ni kama hayakutimia kwani hawakuweza
kupokea maoni kutoka kwa makundi muhimu hasa ya upande wa Zanzibar kama
ilivyokusudiwa.
Hata hivyo, jana Makamu wa Pili wa Rais wa
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Balozi Seif Ali Idd,
alilihakikishia Bunge kuwa upande wa Zanzibar ulishirikishwa katika
kutoa maoni ya muswada huo.
Hatua ya Balozi Idd kutoa ufafanuzi ilitokana na
mwongozo ulioombwa na Mbunge wa Sikonge, Said Nkumba(CCM) aliyeomba kwa
vile Balozi Seif yuko ndani ya Bunge basi apewe fursa kufafanua utata
huo.
Kauli ya Balozi Idd inapingana na ile iliyotolewa
juzi jioni na Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu ambaye
alisema ni kosa kubwa kamati kutochukua maoni ya Wazanzibar.
Lissu alisema kulikuwa na njama tangu mwanzo za kuhakikisha kuwa
Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala haichukui maoni ya
Wazanzibari na hilo linathibitishwa na ratiba zilizokuwa zimeandaliwa na
kamati.
“Katika orodha ya wadau wote 22 waliokuwa
wameorodheshwa katika kutoa maoni yao juu ya muswada huu hakukuwa na
Mzanzibari hata mmoja…tulipoipitia tukasema hapana Wazanzibari wako
wapi,” alisema.
Lissu alisema yeye, Mwenyekiti wa Kamati, Chana na
Makamu Mwenyekiti, William Ngeleja walikwenda kumwona Katibu wa Bunge,
Dk Thomas Kashililah na kumweleza azma yao ya kwenda kuzungumza na wadau
wa Zanzibar.
“Katibu akatwambia kwamba yeye ana fedha za
kutuwezesha kukaa Zanzibar hata wiki moja, kwa hiyo tukarudi kwenye
kamati tukatengeneza ratiba mpya na tukaongeza wadau sita wa Tanganyika
na Wazanzibari wanane,” alisema Lissu.
Aliwataja wadau hao kuwa ni Chuo cha Taifa
Zanzibar, Chuo Kikuu cha Zanzibar, Chama cha Mawakili Zanzibar, Chama
cha Wanasheria Wanawake Zanzibar, Chama cha Walemavu Zanzibar na Profesa
Abdul Shariff.
Wadau wengine walikuwa ni Shirikisho la Vyama
visivyo vya Kiserikali Zanzibar (Angoza) na Jumuiya ya Misikiti Zanzibar
na Jumuiya ya Maimamu Zanzibar, lakini hatukuwahi kukutana nao na
kupokea maoni yao.
“Tukakubaliana kuwa tutakaa Zanzibar kwa siku tatu
kuanzia Julai 14 hadi Julai 16 mpaka leo hatujawahi kuambiwa kwa nini
tulizuiwa kwenda Zanzibar, lakini maneno yaliyokuwa yakisikika eti kwa
sababu za kiusalama,” alisema.
Lissu alisema wakati kamati yao ikiambiwa haiwezi
kwenda Zanzibar kwa sababu za kiusalama, wajumbe wa Kamati ya Ulinzi ya
Bunge hilo ilikuwa Pemba ikiendelea na ziara zake.
No comments:
Post a Comment