Thursday, September 19, 2013

JE, MASTAA WA BONGO WAMEHUSIKA VIPI KATIKA KASHFA ZA MADAWA YA KULEVYA?

Taifa linazidi kutikisika kufuatia idadi kubwa ya vijana kujiingiza katika utumiaji wa madawa ya kulevya. Awali ilianza taratibu lakini miaka ya hivi karibuni, hali imezidi kuwa mbaya.

Starehe za ujana ndiyo chanzo cha yote, vijana wengi wamekuwa wakijikuta wameingia katika matumizi ya madawa ya kulevya kwa kushindwa kudhibiti nguvu za ujana.

Jamii ilikuwa ikiamini kwamba wasanii ndiyo kioo cha jamii, ndiyo maana taasisi mbalimbali hupenda kuwatumia wasanii ili waweze kufikisha ujumbe na kuwaokoa wale wote walioathirikia lakini cha kushangaza, kadiri miaka inavyozidi kwenda, wao ndiyo wamekuwa chanzo cha tatizo, wanatumika kusafirisha na pia wametopea katika matumizi.

MASTAA
Mastaa wamegeuka kuwa ndiyo ‘punda’ wa kusafirisha mizigo ya madawa. Ndiyo wanaongoza kubwia ulevi huo, jamii inabaki kujiuliza kuwa vipi kuhusu kile kizazi ambacho kilikuwa kikiwatazama wao kama kioo chao? Inasikitisha.

UTAJIRI WA HARAKA
Takwimu zinaonesha kwamba, wengi wanajishughulisha na biashara ya kusafirisha madawa hayo ili kusaka utajiri wa haraka.
Wapo waliofanya biashara hiyo kwa miaka mingi na kunusurika na mkono wa sheria lakini baadhi yao wamebanwa katika mikono ya sheria na sasa hawajui hatima ya maisha yao.
Amani linakukumbusha baadhi mastaa ambao taifa lilikuwa likiwategemea katika kujenga taifa kama si kuwakomboa wale ambao wamejitosa katika madawa, badala yake wao ndiyo wakajikuta wamezama katika janga la matumizi au kusafirisha madawa ya kulevya:

AGNESS MASOGANGE
Ni binti mwenye mvuto, umbo lake kila mmoja alilitamani kulitumia katika kazi mbalimbali za sanaa. Muonekano wake ulikuwa kama chachu kwa kuweza kuhamasisha jambo fulani na hata yeye binafsi kujiingizia kipato kupitia kazi ya ‘video queen’ aliyokuwa akiifanya lakini akanaswa akisafirisha madawa ya kulevya nchini Afrika Kusini.
Alinaswa akiwa na madawa ya kulevya kilo 150, Mkuu wa Kitengo cha Kudhibiti na Kupambana na Madawa ya Kulevya nchini, Godfrey Nzowa hivi karibuni akiwa na jopo lake walikwenda kumhoji nchini humo na kuahidi kuwasaka wote waliohusika kumtuma mzigo huo.

MELISA EDWARD
Umaarufu wake haukuwa mkubwa sana lakini alikuwa karibu na mastaa ndipo jina lake lilianza kuchanua.
Baadhi ya watu walimjengea picha ya mbali atakuja kuwa muigizaji mkubwa.
Wakati watu wakiwa na mtazamo huo, akajikuta amenaswa katika mtego mmoja na Masogange nchini Afrika Kusini, naye haijulikani hatima yake hadi pale kesi yao itakaposikilizwa.

REHEMA CHALAMILA ‘RAY C’
Ndani ya Bongo Fleva alikuwa tegemeo, ndoto zake zilizima kama taa. Alikiri kushawishiwa na aliyekuwa mpenzi wake, Lord Eyes na kutopea katika utumiaji wa madawa hayo.
Hivi karibuni ametangaza kuacha na kurejea katika ulimwengu wa kawaida. Akifanikiwa itakuwa vizuri lakini kwa sehemu aliyokuwa amefikia ukilinganisha na jamii ilivyokuwa ikimtazama kama kioo, ilikuwa ikisikitisha sana.

AISHA MADINDA
Anajulikana sana na wapenzi wa muziki wa dansi kama mnenguaji, alizitumikia vyema bendi mbalimbali za dansi hapa nchini. Ndoto yake ilizima ghafla pale alipojitumbukiza katika matumizi ya madawa ya kulevya, alitangaza kuacha hivyo jamii inamtazama kwa karibu kuona kama anaweza kufanikiwa kuacha.

LORD EYES
Huu ni mwamba wa Hip Hop kutoka Arusha, alikuwa mpenzi wa Mwanamuziki Ray C. Anatajwa kuwa mwalimu wa Ray C katika suala zima la matumizi ya madawa ya kulevya. Hadi sasa haieleweki kama bado anatumia au la.

MBWANA MATUMLA
Nguli wa mchezo ya ngumi Bongo, aliwika sana miaka ya nyuma hadi alipoamua kuhamishia makazi yake nchini Ethiopia, awali alidai anakwenda kufanya biashara za kawaida lakini ghafla, ikaripotiwa amenaswa na madawa ya kulevya wiki chache zilizopita.

CHID BENZ
Mkali wa muziki wa Hip Hop nchini, sauti yake na nyimbo zake zilipendwa na wengi. Hakuna ambaye aliweza kufikiri kuwa staa huyu anatumia madawa ya kulevya hadi yeye mwenyewe alipoamua kuweka wazi wiki chache zilizopita.
Mbali na Chid, wapo wasanii wengi wa muziki wa Bongo Fleva ambao wanatajwa kushiriki katika matumizi ya madawa ya kulevya. Tatizo kwa sasa limeongezeka mara dufu na takwimu zinaonesha umri ambao ni hatari zaidi ni vijana kuanzia miaka 15-34.

NINI KIFANYIKE?
Kuna haja ya jamii kushirikiana ili kuitokomeza biashara hiyo ambayo imekuwa ni janga la taifa kwani vijana wengi wanaathirika kila kukicha na matumizi ya dawa za kulevya.

No comments:

Post a Comment