Mpaka sasa watu watatu wameshakufa kutokana na mashambulio ya mabomu mawili yaliyoripuka wakati wa mbio ndefu za marathon katika mji wa Boston nchini Marekani.
Mabomu mawili yaliripuka kwenye mitaa iliyokuwa imejaa watu karibu na sehemu ya kumalizia mbio za marathon. Watu wasiopungua watatu wamekufa kutokana na miripuko ya mabomu hayo yaliyoutikisa mji wa Boston katika jimbo la Marekani la Massachusettes.
Je ni magaidi tena?
Watu wengine zaidi ya140 walijeruhiwa katika kadhia ya umwagikaji wa damu. Vioo vilivunjika na sehemu za miili ya binadamu ilitapakaa- hali iliyosababisha wasiwasi kwamba magaidi wameishambulia tena Marekani. Msemaji wa Ikulu ya Marekani ambae hakutaka kutajwa kwa sababu uchunguzi bado unaendelea, ameeleza kuwa mashambulio hayo yanazingatiwa kuwa ni kazi ya magaidi.
Akitoa tamko juu ya mashambulio hayo Rais Obama aliepuka kutumia neno gaidi, alieleza kwamba maafisa wa Marekani hawajui ni nani aliyeyatega mabomu hayo na kwa nini. Hata hivyo afisa mmoja wa Ikulu ya Marekani alisema baadae kuwa miripuko hiyo iliyotokea kwenye mbio za marathoni zenye jadi ya miaka mingi, inazingatiwa kuwa kitendo cha ugaidi.
Obama asema aliefanya mashambulio atapatikana:
Rais Obama alilihutubia taifa kwa kuwahakikishia Wamarekani kwamba, tukio hilo litachunguzwa kwa undani. Obama alisema "Tutabainisha nani ameyafanya mashambulio haya na kwa sababu gani." Ameeleza kuwa wote wale waliohusika, au kikundi chochote- kitauona mkono mkali wa sheria. Rais Obama amesema Marekani itamjua alieyafanya mashambulio hayo.
Mabomu hayo mawili yalipishana kwa muda wa sekunde chache tu. Mwokoaji anaetoa huduma ya kwanza, amesema wanajaribu kupata damu kwa haraka. Amearifu kuwa wapo waliojeruhiwa kwa kukatika viungo vya mwili na, wengine waliumizwa na vipande vya vioo, na pote palisambaa damu.
CHANZO: DW/DPA
No comments:
Post a Comment