MANDELA ALAZWA KWA MARADHI YA MAPAFU
Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Nelson Mandela, amelazwa hospitali baada ya kupatwa tena na maambukizi katika mapafu yake. Hii ni mara ya pili ndani ya mwezi huu kwa mwanaharakati huyo, shujaa wa kupinga ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini, kulazwa hospitalini.
Hapo Mwezi Disemba, Mandela alilazwa kwa wiki tatu hospitalini kwa maambukizi kama hayo na upasuaji wa kuondoka uvimbe tumboni. Mapema mwezi huu, Mandela alikaa hospitalini kwa usiku mmoja kwa ajili ya uchunguzi wa afya yake.
Ofisi ya Rais Jacob Zuma imesema madaktari wanaendelea kumhudumia, kuhakikisha kuwa anapata matibabu bora zaidi ya kitaalamu na faraja. Mandela amekumbwa na maradhi kadhaa yanayotishia afya yake katika miaka ya hivi karibuni.
Mapema mwaka 2012 alilazwa kwa ajili ya uchunguzi mdogo wa maumivu ya tumbo, na mwaka 2011 alilazwa kwa siku mbili kutokana na tatizo katika mfumo wa upumuaji.
No comments:
Post a Comment