MTU mmoja ambaye anasadikiwa kuwa ni jambazi ameuawa kwa kupigwa risasi na Askari wa Jeshi la Polisi akiwa kwenye harakati za kuteka magari katika Eneo la Mlima Nyoka Jijini Mbeya baada ya kutokea kwa majibizano ya kurushiana risasi.
ACP DIWANI ATHUMANI NA JAMBAZI MOCHWARI RUFAA MBEYA
Jambazi huyo ni miongoni mwa watu waliokuwa wakitafutwa na Jeshi la Polisi Mkoani hapa akituhumiwa kuhusika na mauaji ya Askari Polisi mwenye namba G 68 PC Jafari yaliyotokea Februari 6, Mwaka huu katika eneo la Matundasi Wilayani Chunya.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Diwani Athumani amethibitisha kutokea kwa tukio hilo katika Mkutano alioufanya na waandishi wa Habari Ofisini kwake ambapo amesema tukio hilo limetokea majira ya Saa 10(kumi) Alfajiri usiku wa kuamkia leo Machi 25, Mwaka huu.
Kamanda Diwani amesema kabla ya tukio majambazi wapatao wanne tayari walikuwa wameweka mawe barabarani kwa nia ya kuteka magari ili wafanye uporaji katika eneo hilo la Mlima Nyoka ambalo limekuwa na matukio kadhaa ya watu kuporwa mali zao.
Amesema Jeshi la polisi baada ya kupata habari za kutegwa mawe, askari walifika kwa wakati kwa kuwa polisi walikuwa jirani na eneo hilo na kuweka mtego kwa kuwa majambazi hawakuwa wameonekana kwa wakati ule.
Diwani alisema katika mapambano hayo alijeruhiwa jambazi mmoja kwa risasi kiunoni na ubavuni kulia na wengine watatu walifanikiwa kutoroka ambapo Marehemu alipowahishwa hospitali kwa matibabu daktari alibaini kuwa amekwisha fariki.
Amesema jambazi huyo alikutwa na silaha moja SMG yenye namba AB huku namba nyingine zikiwa zimefutwa na magazine yake ikiwa na risasi ishirini na mbili (22) pamoja na mapanga mawili(2).
Baada ya Marehemu kufanyiwa upekuzi maungoni mwake jambazi huyo alikutwa na kitambulisho cha mkazi chenye namba B.0010453 chenye jina la Emanuel Blasius Mdendemi aliyezaliwa mwaka 1984 eneo la Matamba wilayani Makete Mkoa wa Iringa makazi yake ni Uwemba Mkoani Njombe.
CHANZO: MBEYA YETU
CHANZO: MBEYA YETU
No comments:
Post a Comment