HATIMAYE Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimekubali kusitisha maandamano yake yaliyokuwa yafanyike leo katika majiji manne ya Dar es Salaam, Arusha, Mbeya na Mwanza, kuwashinikiza Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa na Naibu wake, Philipo Mulugo kuachia ngazi.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Said Mwema akiwa pamoja na Kamishina wa Oparesheni (CP) Paul Chagonja, Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleimani Kova na maofisa wengine kukutana na viongozi wa CHADEMA chini ya Mwenyekiti, Freeman Mbowe.
CHADEMA iliwapa viongozi hao wiki mbili tangu Februari 18 mwaka huu, kuachia ngazi kama sehemu ya uwajibikaji kutokana na matokeo mabaya vinginevyo wangefanya maandamano makubwa leo kuwashinikiza wang’oke.
Hata hivyo, juzi serikali ilitangaza kuyasitisha maandamano hayo ikidai inatoa nafasi kwa wananchi waweze kumpokea Rais wa China, Xi Jinping ambaye alianza ziara ya siku mbili nchini, jambo ambalo CHADEMA walilipinga na kusisitiza kuandamana.
Jana viongozi hao wa polisi na siasa walilazimika kukutana na kuzungumza kwa kirefu na Mbowe hatimaye kufikia muafaka kwa CHADEMA kukubali kusogeza maandamano yao hadi hapo baadaye.
No comments:
Post a Comment