Monday, January 14, 2013

MIRUNGI "GOMBA" YAKAMATWA ARUSHA


Jeshi la Polisi mkoani Arusha  limewakamata watu wanne wakiwa na madawa ya kulevya aina ya mirungi. Watu hao walikuwa na jumla ya viroba 202 vya dawa hizo  ambazo zilikuwa kwenye gari aina ya Mitsubishi Canter lenye namba za usajili T 306 BUN.
 
Akizungumza na waaandishi wa habari nje ya jengo la Makao Makuu ya Jeshi hilo Mkoani hapa, Kamanda wa Polisi Mkoani humo Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Liberatus Sabas aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Joel Alfayo Lukumay (37), Rahim Azizi Gilla (35), Ibrahimu Solomon Katambwei (40) na Musa Lazaro Mollel (38) wote ni wakazi wa Mkoa wa Arusha.

Alisema tukio hilo lilitokea leo saa 1:00 asubuhi katika eneo la Engikareti lililopo wilayani Longido mkoani hapa. Aliongeza kwa kusema kwamba, mafanikio hayo yametokana na taarifa toka kwa raia wema ambao waliwasiliana na jeshi hilo, ambapo mara baada ya kupata taarifa hiyo waliweka mtego katika eneo hilo na kufanikiwa kulikamata gari hilo ambalo lilikuwa linatokea nchi jirani ya Kenya.

Kamanda Sabas aliwashukuru wananchi wa Mkoa wa Arusha kwa ushirikiano wao  mkubwa unaofanywa kwa jeshi hilo na kuwaomba waendelee kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu kwani kama wananchi wakiamua uhalifu unaweza ukapungua kwa kiasi kikubwa.

Baadhi ya waaandishi na askari waliokuwa kwenye eneo hilo walishuhudia viroba hivyo vikiwa na majina ya watu pamoja na uzito wa kila mzigo huku wengine wakidai kwamba inawezekana gari hilo huwa linabeba mizigo ya watu mbalimbali ambao wanakuja kugawana mara baada ya kuingia Arusha Mjini.

Kutokana na tukio hilo Jeshi la Polisi Mkoani hapa linaendelea kuwahoji watuhumiwa hao na pindi upelelezi utakapokamilika watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili. Aidha taarifa za ndani ya jeshi hilo zinasema kwamba gari hilo lilishawahi kukamatwa tarehe 16 mwezi Machi mwaka jana ambalo lilikutwa na madawa ya aina hiyo na kesi yake ilikwishafikishwa mahakamani na bado shauri hilo bado linaendelea.

No comments:

Post a Comment