Thursday, September 12, 2013

ALIYEIBA 'BODABODA' AKUTWA AMEJIFICHA KWENYE PAA LA NYUMBA

Mtu anayedaiwa kuwa mwizi wa pikipiki za biashara maarufu kama Bodaboda, hivi karibuni alichomolewa kutoka ndani ya paa la nyumba alikokimbilia kujificha baada ya kuoneshwa bastola ya polisi huko Temeke, karibu na kituo cha mabasi cha daladala cha Bandari jijini Dar.

  Mwizi huyo akitolewa kwenye paa la nyumba.
Tukio hilo lililojaza umati lilitokea baada ya mtuhumiwa huyo kukimbizwa na askari waliokuwa na silaha kufuatia jaribio lake la kupora pikipiki hiyo kushtukiwa.
Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo ambaye jina linahifadhiwa, alisema kuwa mtuhumiwa alipofika nyumbani hapo kwa nia ya kujificha, mikononi mwake alikuwa ameshika visu viwili huku akidai kuwa mwenzake aliyekimbia, ndiye aliyekuwa na  bunduki iliyotumika kumtishia dereva wa bodaboda ili kumnyang’anya pikipiki.
Baada ya kuingia katika nyumba moja iliyo pembeni mwa kituo hicho cha daladala, mtuhumiwa huyo alipanda juu ya dari na kuanza kutambaa akitokomea chumba kimoja baada ya kingine.
Kuona hivyo, wananchi walisaidiana na polisi kumdhibiti.
Mmoja wa askari asiye na sare alipanda juu ya paa hilo na kumwelekezea bastola, akitishia kumlipua kama hatashuka kwa hiyari, kitendo kilichomlazimisha jamaa huyo kutii amri na kuteremka.
Shuhuda huyo alisema kuwa matukio hayo ya uporaji wa pikipiki yamekuwa mengi wilayani Temeke ambapo yamekuwa kero kubwa kwa wananchi, kiasi kilichosababisha mtuhumiwa huyo kupata wakati mgumu kuponyoka.
“Unajua ujambazi umezidi sana hapa Temeke na kuna baa moja kubwa (jina linahifadhiwa) ndiyo wamekuwa wakikaa kwa ajili ya kupanga mipango yao, sisi hivi karibuni tuliibiwa gari lakini tunashukuru Mungu tulilikamata baada ya Fuso moja kuligonga wakati majambazi walipokuwa wakikimbia nalo,” alisema.

Baada ya kukamatwa mtuhumiwa huyo alipelekwa kwenye Kituo cha Polisi cha Chang’ombe lakini Kamanda wa Polisi mkoa wa Temeke, Englibert Kiondo alipoulizwa na gazeti hili hatma ya tukio hilo, alisema bado halijafika mezani kwake na kuwa atafuatilia kwa mkuu wa kituo na kutoa ufafanuzi baadaye.

KESI YA SHEIKH PONDA YAAHIRISWA

Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Morogoro jana iliitaja na kuahirisha kesi inayomkabili Katibu wa Jumuiya na Taasisi ya Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda bila ya kiongozi huyo kuwapo mahakamani.
 
Kesi hiyo ilitajwa jana na Mwanasheria wa Serikali, Gloria Rwakibalila mbele ya Hakimu wa Mahakama hiyo, Agnes Ringo na kuahirishwa hadi Septemba 17 mwaka huu, wakati Mahakama itakapotoa uamuzi kuhusu maombi ya kiongozi huyo kupatiwa dhamana.
Hii ni mara ya kwanza kwa kesi hiyo kutajwa bila Ponda kuwapo, huku kukiwa na utulivu tofauti na siku zilizopita.
Mara ya mwisho Agosti 29, Ponda alifikishwa mahakamani hapo na kusababisha kusimama kwa shughuli za Serikali wilayani Morogoro baada ya ofisi kadhaa ikiwamo ya Mkuu wa Wilaya na baadhi ya mitaa kufungwa ili kupisha kusikilizwa kwa kesi hiyo.
Kadhalika Agosti 19, mwaka huu Ponda alisafirishwa kwa helikopta akiwa chini ya ulinzi mkali, na kesi yake ilivuta umati mkubwa watu.
Jana kesi hiyo ikitajwa kwenye mahakama ya ndani (chamber court) na baadhi ya wafuasi wa Ponda walionekana nje ya uzio wa mahakama hiyo huku wakiwa hawajui nini kinachoendelea.
Ilimlazimu Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Richard Kabate kutoka nje ya ofisi yake na kuwaeleza wafuasi hao sababu za kutofikishwa kwa kiongozi wao mahakamani hapo.
“Kesi hiyo imeshindikana kutajwa kwenye mahakama ya wazi kwa sababu mahakama hiyo inatumiwa kuendeshea kesi nyingine chini ya majaji wa Mahakama Kuu, hatutaki kuleta mwingiliano.
“Ninataka kuwaeleza kuwa mwondoke kwa kuwa Sheikh Ponda hakufikishwa mahakamani hapa leo hadi Septemba 17 atakapoletwa kwa ajili ya kutolewa kwa uamuzi wa dhamana,” alisema Hakimu Kabate.
Baada ya Hakimu Kabate kutoa ufafanuzi huo, wafuasi hao walionekana kutoridhishwa na kauli hiyo na kuanza kujikusanya vikundi vikundi, lakini baadaye walianza kutawanyika.
Mashtaka yaliyotajwa mahakamani hapo na kumkabili Sheikh Ponda ni matatu ambayo ni uchochezi, kuharibu imani ya watu wengine na kushawishi kutendeka kwa kosa, mashtaka ambayo anadaiwa kuyatenda Agosti 10 mwaka huu eneo la Kiwanja cha Ndege Manispaa ya Morogoro.
Sheikh Ponda anatetewa na mawakili watatu wakiongozwa na wakili Msomi Juma Nassor ambaye tayari amewasilisha ombi la dhamana.

WANANCHIA WATUMIA VYANDARUA KUTENGENEZEA VYOO


Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mkoani Singida Edward Ole Lenga akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kinampundu mara baada ya kukabidhiwa Zahanati na nyumba mbili za mganga na shirika moja lisilo la kiserikali la HAPA,hafla hiyo ilifanyikajuzi kijijini hapo.

Ni Mwakilishi wa shirika la SIMAVI kutoka nchini Uholanzi Lieke Ongering akizungumza katika hafla ya kukabidhi mradi wake kwa ushirikiano na shirika la HAPA Singida kukamilisha mradi wa ujenzi wa Zahanati na nyumba mbili za mganga kijiji cha Kinampundu takribani umbali wa kilomita 70 kutoka mjini Singida.
 
Ni mmoja wa kinamama wajawazito akipimwa uzito na mkuu wa Wilaya ya Mkalama Ole Lenga mara baada ya kukabidhiwa vifaa vya zahanati hiyo, anayeshuhudia kipimo hicho ni mhasibu mkuu wa shirika hilo Noel Makyao.

Mkurugenzi wa HAPA Davd Mkanje  (Kulia) kimkabidhi DC wa Mkalama Ole Lenga baadhi ya vifaa vya kutolea huduma kwenye Zahanati hiyo wakati wa hafla fupi ya makabidhiano ya mradi huo.

Ni baadhi ya wageni kutoka Mataifa mbalimbali nje ya nchi wakicheza muziki na wananchi wa kijiji cha Kinampundu mara baada ya kukabidhiwa mradi huo wa afya ya uzazi wa mama na mtoto.
Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Ole Lenga, kushoto mwenye suti, mwakilishi wa SIMAVI, Lieke, MMkurugenzi wa shirika la HAPA, Davd Mkanje na mhasibu mkuu wa shirika hilo Noel Makyao wakifurahia pamoja na wananchi mara baada ya kukabidhi mradi huo.


Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mkoani Singida ameonya tabia ya baadhi wananchi kuezekea kwenye vyoo vyandarua vya kujikinga na mbu wa malaria.

Onyo hilo limetolewa mwishoni mwa wiki iliyopita na Mkuu huyo wa Wilaya, Edward ole Lenga wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kinampundu muda mfupi baada ya kukabidhiwa Zahanti ya kijiji na shirika la HAPA.

Alisema imezuka tabia ya wananchi kutumia vyandarua hivyo kwa matumizi yasiyo rasmi ikiwa na pamoja na wengine kuvifanya kama mabanda ya kuhifadhi vifaranga vya kuku.

“Hii ni aibu, wenzetu wanatupatia vyandarua  ili tusipate malaria, nyie mnatumia kuezeka vyoo kwa kweli hii ni aibu kubwa sana na mimi nimetembea vijijini na kujionea hili, na kwa kweli atakayekamatwa atakiona cha moto.” Alisema Dc Lenga kwa masikitiko.

Aidha alisema serikali inatumia fedha nyingi kwa ajili ya kuagizi
vyandarua hivyo kwa ajili kujikinga na mbu wa malaria huku wananchi wakiziona kana kwamba hazina msaada na kuzitumia kama kinga kwenye vyoo.

“Hivi chandarua kukiezekwa kwenye choo si mtu unaonekana tu , acheni hii tabia chafu, nimeunda kikosi kila kijiji atakayebainika kufanya hivyo akamatwe na kuletwa kwangu mimi nitamshughulikia ipasavyo.” Alisisitza Ole Lenga.

Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Wilaya aliwataka wananchi wa Wilaya hiyo wanaoishi maeneo ya mijini kuja nyumbani na kujenga nyumba na vyoo bora.

Wednesday, September 11, 2013

BABY MADAH ASAINI MKATABA WA MAMILIONI YA PESA KENYA

Baby Madah
Msanii maarufu wa kike Tanzania anayefanya vizuri sana kwenye muziki na filamu,baby Madaha amelamba bingo ya uhakika na kampuni ya Candy n’ Candy Records Label ya jijini Nairobi iliyomsainisha mkataba msanii mwingine wa Tanzania Mr.Nice hivi karibuni.
Meneja wa msanii huyo  Joe Kariuki amesema kuwa  pamoja na msanii huyo kupewa mkataba huo wa million hamsini (50) pia wamempa mwanadada huyo gari ya kutembelea ya kisasa aina ya AUDI TT  na nyumba  kali mitaa kijitonyama jijini  Dar es salaam.
Pamoja na hayo pedeshee huyo wa Mr.Nice ambaye ndio mmiliki wa studio hiyo amesema wanataka kumuhamishia msanii huyo jijini Nairobi nchini Kenya kwa kipindi cha mwaka mmoja ili afanye nao kazi huko kwani wamegundua kuwa anakubalika sana nchini humo na wapenzi wa muziki.
Baby madaha ambaye  anatarajia kutua nchini leo akitoka Nairobi pamoja na meneja wake kwa ajili ya kuachia video ya  wimbo wake wa kwanza aliofanya na Label hiyo uitwao (Summer Holiday) ambao umefanywa huko huko jijini Nairobi

FRAT YAPINGA UAMUZI WA LIGI YA SHIRIKISHO TZ

Chama cha Waamuzi Tanzania (FRAT), kimepinga uamuzi wa Kamati ya Ligi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kuwafungia kwa mwaka mmoja waamuzi  Martin Saanya na Jesse Erasmo.
Ofisa Habari wa TFF, Bonifance Wambura alisema jana kuwa Saanya amefungiwa kwa kuchezesha chini ya kiwango na alitoa adhabu tata iliyoipa Union bao la kusawazisha wakati Erasmos alishindwa kumshauri mwamuzi wa kati katika tukio hilo.
Hata hivyo, Katibu Mkuu wa FRAT, Charles Ndagala alisema uamuzi huo wa Kamati ya Ligi kuwafungia Saanya na Erasmo si sahihi na hatari kwa maendeleo ya soka la Tanzania.
“Bado sijapata taarifa rasmi za kiofisi kwa vile nipo safarini, lakini kama uamuzi wao ndiyo huo wanafanya makosa makubwa ambayo matokeo yake ni kulizamisha soka letu,” alisema Ndagala na kuongeza:
“Jamani, makosa hata Ulaya yanafanywa, lakini si kosa mwamuzi anasimamishwa wakati mwingine tuwaonye na kuwapa nafasi nyingine ya kuwatazama vinginevyo tutawamaliza.”
Alisema, endapo adhabu ya aina hiyo itaendekezwa kuna hatari ligi kuchezeshwa na waamuzi wasiokuwa na uzoefu.
“Waamuzi wazuri wote wataondoka watakuja wasio na uzoefu na hapo hali ndiyo itakuwa mbaya zaidi, ebu fikiri tayari wamemfungia Akrama (Mathew) na Abbas Mahagi kama utaratibu huu utaendelea hai itakuwaje?”.
Naye mwamuzi wa zamani wa soka, Othman Kazi alisema: “Kamati ya Ligi haina tofauti na ile ya TFF  kwa sababu imefanya uamuzi uleule wa kukurupuka.

JE, KANUNI ZA BUNGE ZIMEWASHINDA NAIB SPIKA NA MBOWE?

Kumekuwa na mjadala mkali kuhusu iwapo Naibu Spika, Job Ndugai alikiuka Kanuni za Bunge katika kushughulikia vurugu zilizotokea Bungeni Alhamisi iliyopita kwa kuamuru kutolewa nje kwa Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe.
Ndugai ambaye alikuwa kiongozi wa shughuli za Bunge siku hiyo, aliwaamuru askari kumtoa nje Mbowe baada ya kukaidi amri yake ya kutaka kuketi chini aliposimama kutaka kupewa nafasi ya kuzungumza, hali iliyozua tafrani bungeni.
Pamoja na mambo mengine Ndugai amekuwa akituhumiwa kwamba anaminya uhuru wa wabunge wa upinzani kutokana na mapenzi aliyonayo kwa chama chake, CCM.
Kwa upande mwingine, kumekuwa na lawama kwamba Mbowe alikosea kukaidi amri ya Naibu Spika kwa kuwa kanuni zinamtaka mbunge yeyote (hata akiwa waziri), kuketi pale kiongozi wa Bunge (Spika, Naibu au Mwenyekiti) anaposimama, hivyo kusababisha mtafaruku.
Mwenyekiti wa Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar, Profesa Chris Peter Maina alisema tatizo lililojitokeza bungeni linaweza kumalizwa na kuwapo kwa sheria inayokataza Spika wa Bunge kuwa mwanachama wa chama chochote cha siasa.
“Unajua kwa Katiba ya sasa Spika wa Bunge anaweza kuwa mwadilifu lakini akapata shinikizo kutoka upande wa chama chake, Ibara ya 128 ya Rasimu ya Katiba Mpya inaeleza kiundani kuhusu spika kutokutoka miongoni mwa wabunge jambo ambalo ni zuri,” alisema Profesa Maina na kuongeza:
“Mwenendo wa Bunge siyo mzuri. Wabunge hawaheshimiani hata kidogo, nadhani wanahitaji kukubaliana kwa hoja, wao ndiyo wanatunga sheria, hivyo wanatakiwa kulumbana kwa kufuata utaratibu uliowekwa.”
Spika wa zamani, Pius Msekwa alisema wakati akiongoza Bunge hakuwahi kuona vurugu, fujo na malumbano ya wabunge kama ilivyotokea Alhamisi iliyopita.
“Wakati nikiwa Spika sikumbuki kama kuna siku ziliwahi kutokea vurugu za aina hii, kilichotokea ni sawa na uhalifu kwa sababu taratibu hazikufuatwa,” alisema Msekwa.
Matakwa ya Kanuni
Ibara ya 76 (1) na (2) ya Kanuni za Bunge Toleo la Aprili 2013, zinaeleza jinsi ya kudhibiti fujo bungeni, lakini Ndugai anakosolewa kwamba hakuzingatia taratibu hizo kushughulikia vurugu za Alhamisi.
Kanuni ya 76 (1) inasema: “Kwa madhumuni ya kudhibiti fujo endapo itatokea ndani ya Ukumbi wa Bunge na Spika ataona kuwa kuna haja ya kutumia nguvu, basi anaweza kuahirisha shughuli za Bunge bila ya hoja yoyote kutolewa au kusitisha kikao kwa muda atakaoutaja ili fujo hiyo iweze kudhibitiwa na Mpambe wa Bunge”.
Kadhalika, fasili ya pili ya Kanuni hiyo inasema: “Baada ya utulivu kurudia, Spika atalipeleka kwenye Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge suala ambalo lilisababisha kutokea kwa fujo ikiwa ni pamoja na jina la mbunge au majina ya wabunge waliohusika na fujo hiyo ili kamati hiyo iweze kulishauri Bunge kuhusu adhabu inayostahili kutolewa”.
Wakati vurugu zilipozuka bungeni, Ndugai aliwaita askari badala ya mpambe, kumtoa nje Mbowe na hakuwa amesitisha wala kuahirisha shughuli za Bunge kama kanuni zinavyotaka.
Pia Naibu Spika alitangaza kumsamehe Mbowe na Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ kwa maana ya kuwaruhusu kuendelea na vikao vya Bunge siku hiyo jioni, badala ya suala hilo kupelekwa kwenye kamati husika kama kanuni ya 76 (2) inavyoelekeza.
Utetezi wa Ndugai
Ndugai alisema hakuzingatia kanuni hizo kwani mazingira ya vurugu hizo hayaendani na kanuni husika, hivyo alitumia nafasi yake ambayo pia inatambuliwa na kanuni za Bunge.
“Vurugu zilikuwa zimepangwa na zilifanywa kwa makusudi ili kuhakikisha kwamba shughuli za Bunge zinakwama maana hiyo kanuni wanafahamu kwamba ipo, sasa hatuwezi kuwa na Bunge ambalo mtu akiamua tu anafanya fujo ili liahirishwe,” alisema Ndugai na kuongeza:
“Mimi kama kiongozi wa shughuli za siku hiyo, kazi yangu ni kuhakikisha kwamba shughuli zilizopangwa zinafanyika, kwa hiyo nisingeweza kuruhusu watu wachache watukwamishe kutokana na masilahi yao.”
Alipoulizwa kwamba alifahamu vipi kuwapo kwa njama hizo, alisema kauli na matendo ya wabunge wa upinzani vilionekana tangu mwanzo wa mjadala kutaka kukwamisha shughuli za Bunge siku hiyo.
Kuhusu kuwatangazia wabunge hao msamaha badala ya kupeleka suala hilo kwenye kamati husika, Ndugai alisema: “Hakukuwa na adhabu kubwa ya kuwapa zaidi ya kuwatangazia msamaha.”
“Niliwasamehe kwa mujibu wa kanuni maana zinaruhusu kuzingatia uamuzi ambao uliwahi kutolewa na maspika waliopita, kwa hiyo kama unakumbuka kesi ya Mengi (Regnald) na Malima (Adam), Spika Samuel Sitta baada ya kumwita Malima akakataa kwenda alisema anamsamehe,” alisema na kuongeza:
“Yeye (Sitta) alitumia neno kwamba nimeamua kumpuuza lakini mimi sikusema hivyo, nilisema kwamba namsamehe kwa sababu tu namheshimu na ni kiongozi mkubwa tu katika jamii”.
Mbowe hakupatikana juzi na jana kuzungumzia suala hilo, lakini Mnadhimu Mkuu wa Upinzani Bungeni, Tundu Lissu alisema kiongozi wake huyo hakufanya makosa kwani alisimama wakati Mbunge wa Vunjo (TLP), Augustine Mrema alipokuwa akizungumza na kwamba hilo siyo kosa kikanuni.
Alisema Ndugai alipaswa kumheshimu Mbowe kwa kuzingatia wadhifa wake bungeni na kwamba kitendo cha kumwambia “kaa chini” hakikubaliki.
“Hatuwezi kuruhusu na hatutaruhusu Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kudhalilishwa, ikiwa tutaruhusu hilo litokee, basi miongoni mwetu sisi wapinzani hakuna atakayepona,” alisema Lissu na kuongeza:
“Naibu Spika amelidhalilisha Bunge kwa sababu kwa kumdharau Mbowe ni kwamba amemdharau mmoja wa viongozi wakuu wa Bunge”.
Wabunge wa Kambi ya Upinzani Bungeni wakizuia Kiongozi wa kambi hiyo, Freeman Mbowe (aliyevaa tai ya njano) asitolewe nje ya Ukumbi wa Bunge na Askari wa Bunge baada ya Naibu Spika, Job Ndugai kuamuru atolewe, kwenye kikao kilichofanyia Alhamisi ya wiki iliyopoita, mjini Dodoma. (Picha na Fidelis Felix)

MFANYA BIASHARA AMWAGIWA TINDIKALI



Matukio ya wananchi kumwagiwa tindikali yameendelea kushika kasi nchini baada ya Mfanyabiashara wa vifaa vya ujenzi, Christian Msema wa Mburahati Dar es Salaam, kumwagiwa kemikali hiyo mwishoni mwa wiki na watu wasiojulikana.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camilus Wambura alisema hana taarifa hizo licha ya tukio hilo kutokea mbele ya Kituo cha Polisi Mburahati.
“Kwa sasa sina hizo taarifa, labda mpaka niulize,” alisema Kamanda Wambura.
Msema maarufu kama ‘Mnyalu’ amelihusisha tukio hilo lilitokea jioni ya Jumamosi Septemba 8 na mgogoro wa eneo la wazi ambapo yeye alikuwa akipinga mfanyabiashara mmoja (jina linahifadhiwa) kulitumia kuegesha magari yake.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Mburahati, Dickson Tungaraza amekanusha kuwepo kwa mgogoro huo“Mimi ninachojua hakuna mgogoro… wewe uko wapi? njoo ofisini ndiyo utajua yote,” alisema.
Akizungumza katika Hospitali ya Taifa Muhimbili alikolazwa, alisema baada ya kufunga duka lake, watu waliokuwa kwenye pikipiki ya matairi matatu (Bajaj) walimwagia kemikali hiyo na kutoweka.
“Ilikuwa saa mbili usiku baada ya kufunga duka langu nikawa naelekea nyumbani, mara ikaja Bajaj ikasimama mbele yangu. Mmoja wa abiria akaniuliza, vipi bosi, ndiyo unakwenda kuangalia kiwanja chako? Nilipomwangalia ndiyo wakanimwagia tindikali,” alisema Msema na kuongeza:
“Nilipiga mayowe wezi hao wezi hao! Lakini walikimbia bila kukamatwa. Walikuja watu wakanimwagia maji na maziwa na kuniwahisha hospitali.”