Saturday, January 5, 2013

MONJA LISEKI ASAJILIWA MIEMBENI AKITOKEA MTIBWA SUGAR



Monja Privas Liseki 
MSHAMBULIAJI wa Mtibwa Sugar ya Morogoro, Monja Privas Liseki amejiunga na Miembeni ya Daraja la Kwanza Zanzibar kwa mkataba wa miaka miwili.
                                                
Monja yupo kwenye kikosi cha Miembeni FC kinachoshiriki Kombe la Mapinduzi visiwani hapa, ambayo leo usiku itamenyana na Azam FC, ikitoka kuifunga 4-1 Mtibwa Sugar katika mchezo wake wa kwanza wa Kundi B.

“Nipo hapa Miembeni, nadhani nitastaafu nikiwa na timu hii. Huku nimekuja kumalizia soka yangu nafikiri,”alisema

Monja alizaliwa Agosti 8, mwaka 1975, Kinondoni Muslim mjini Dar es Salaam na alipata elimu yake pekee, ya Msingi katika shule ya Muhimbili, Upanga mjini Dar es Salaam.

“Mimi nilikuwa napenda sana soka, nilipomaliza shule ya Msingi tu, nikaachana na shule kabisa nikaanza mitikasi ya soka hadi nikasajiliwa Sigara mwaka 1991 nikiwa bado mdogo sana nina miaka 16 tu,”alisema Monja.

Alicheza Sigara hadi mwaka 1996 iliposhushwa daraja, akahamia Simba SC ambako alidumu hadi mwaka 1998 alipotolewa kwa mkopo Yanga ili aichezee kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.

COASTAL UNION SARE NA MTIBWA SUGAR




COASTAL Union ya Tanga imelazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na Mtibwa Sugar ya Morogoro, katika mchezo wa Kundi B Kombe la Mapinduzi, jioni hii kwenye Uwanja wa Amaan visiwani Zanzibar.
 
Hadi mapumziko, hakuna timu iliyofanikiwa kuona lango la mwenzake na Coastal Union ndio walitakiwa kujilaumu kwa kushindwa kutumia mwanya wa Mtibwa Sugar kucheza pungufu kutokana na beki wake, Salum Swedi kutolewa nje kwa kadi nyekundu dakika ya 43.

Timu zilishambuliana kwa zamu katika kipindi hicho, upande wa Coastal ukiongozwa na Danny Lyanga na Mtibwa Hussein Javu.

Baada ya Swedi kutolewa nje kwa kadi nyekundu, kocha Mecky Mexime alimuinua beki Rajab Mohamed kwenda kuchukua nafasi ya mshambuliaji, Hassan Seif.

Kipindi cha pili, Mtibwa walirudi kwa kasi na kufanikiwa kupata bao la kuongoza dakika ya 58, mfungaji Ally Mohamed ‘Gaucho’ aliyepiga shuti la umbali wa mita 19 na kumtungua Juma Mpongo.

Coastal Union ilisawazisha bao hilo dakika ya 81, mfungaji Jerry Santo aliyefumua shuti la chini la umbali wa mita 24 na kumtungua kipa Hussein Sharrif.

Katika mchezo huo, kikosi cha Mtibwa Sugar kilikuwa; Hussein Sharrif, Hamisi Issa, Yussuf Nguya, Salvatory Ntebe, Salum Swedi, Babu Ally Seif, Ally Mohamed ‘Gaucho’, Rashid Gumbo, Hussein Javu, Hassan Seif/Rajab Mohamed dk43 na Vincent Barnabas.

Coastal Union; Juma Mpongo, Ismail Khamis, Othman Tamim, Philip Metusela, Mbwana Khamis ‘Kibacha’, Hamisi Shengo, Suleiman Kassim ‘Selembe’, Jerry Santo, Mohamed Miraj, Mohamed Soud Othman na Danny Lyanga. 

YANGA YATOKA SARE NA ARMINIA BIELEFELD YA UJERUMANI


Mchezo wa kirafiki kati ya timu ya Arminia Bielefeld kutoka Ujerumani, huko Uturuki, umemalizika kwa sare ya 1-1.

Taarifa ya Yanga katika ukurasa wa facebook wa klabu hiyo, Bao la Yanga lilifungwa katika dakika ya 60 na Tegete, akiunganisha pasi safi aliypewa na Saimon Msuva aliyewatoka walinzi wa Arminia Bielefeld.

Katika mchezo huo Athumani Iddi na Hamis Kiiza hawakuhusishwa katika mchezo huo baada yakutokuwa fiti kwa mchezo.

Kocha Mkuu wa Young Africans Ernest Brandts amesema amefurahishwa na kiwango walichokionyesha wachezaji wake na anaamini kadri siku zinavyokwenda wanazidi kuimarika na kuwa bora, hivyo katika michezo mingine wataendelea kuonyesha mabadiliko makubwa.

1.Ally Mustafa ‘Barthez’
2.Mbuyu Twite
3.Oscar Joshua
4.Nadir Haroub ‘Cannavaro’
5.Kelvin Yondani
6.Kabange Twite
7.Haruna Niyonzima
8.Frank Domayo
9.Said Bahanuzi
10.Didier Kavumbagu
11.David Luhende

Subs:
1.Said Mohamed
2.Shadrack Nsajigwa
3.Stephano Mwasika
4.Juma Abdul
5.Nurdin Bakari
6.Nizar Khalfani
7.Simon Msuva
8.George Banda
9.Jerson Tegete 

JAJI WARIOBA ATOA UFAFANUZI HOTUBA YA RAIS JK MWAKA MPYA




Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji Joseph Warioba ametoa ufafanuzi kuhusu hotuba ya Rais Jakaya Kikwete aliyoitoa usiku wa mwaka mpya na kuzungumzia mchakato wa Katiba unaoendelea na kusema Rais hapaswi kulalamikiwa kwani yote aliyosema yamo ndani ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.

Jaji Warioba Akitoa Ufafanuzi

Jaji Warioba alitoa ufafanuzi huo leo (Jumamosi, Januari 5, 2013) katika mkutano wake na Waandishi wa Habari wakati akizungumzia tathmini ya kazi ya kukusanya maoni binafsi ya wananchi kupitia mikutano iliyomalizika tarehe 19 Disemba mwaka jana (2012).

“Kuna kitu gani kipya alichosema Rais? Yote aliyosema yapo kwenye Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na mimi katika mikutano yangu yote nanyi nimeyaeleza na hakuna asiyejua,” alisema Jaji Warioba ambaye ameshawahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Waziri Mkuu na Makamu wa Rais.

“Rais alielezea mchakato wote kuanzia kukusanya maoni, kuandaa rasimu, kufanyika kwa Mabaraza ya Katiba, Bunge Maalum la Katiba na kura ya maoni…haya yote yapo kwenye sheria ambayo Wabunge waliipitisha,” alisema Jaji Warioba wakati akijibu swali la Mwandishi wa Habari Jabir Idrissa aliyetaka kujua kauli ya Tume kuhusu maoni ya baadhi ya wanasiasa kuwa Rais aliingilia kazi za Tume.

“Hivi ingekuwaje kama Rais angetoa salam za Mwaka Mpya bila kuzungumzia mchakato muhimu kwa nchi kama huu wa Katiba,” alihoji Jaji Warioba.

Akizungumzia mikutano ya kukusanya maoni iliyomalizika mwezi uliopita, Jaji Warioba alisema kazi ya kukusanya maoni ilianza tarehe 2 Julai mwaka jana na Tume yake imetembelea na kufanya mikutano 1,776 katika mikoa yote 30 ya Tanzania Bara na Zanzibar.

Kwa mujibu wa Jaji Warioba, jumla ya wananchi 1,365,337 walihudhuria mikutano hiyo na kati yao, wananchi 64,737 walitoa maoni kwa kuzungumza katika mikutano na wengine 253,486 walitoa maoni yao kwa maandishi katika mikutano hiyo.

Kwa mujibu wa maelezo ya Jaji Warioba, takwimu hizi hazijumuishi maoni yanayoendelea kukusanywa na Tume yake kupitia posta, totuvi ya Tume, mitandao ya kijamii na ujumbe mfupi wa simu za mkononi ambao hadi kufikia jana (Ijumaa, Januari 4, 2013) jumla ya ‘sms’ 16,261.

Kuhusu idadi ya wananchi waliojitokeza mikutanoni na kutoa maoni yao, Mwenyekiti huyo alisema Tume imeridhika na idadi hiyo na kufafanua kuwa kilichokuwa kinatafutwa na Tume ni hoja na kwamba haukuwa wakati wa kupiga kura.

“Ilikuwa ni muhimu kufikia watu wengi iwezekanavyo na ndiyo maana tumefika kila sehemu. Lakini tangu awali, tulishasema hatutaweza kumfikia kila mtu,” alisema na kuongeza kuwa Tume yake imeridhika na idadi na maoni yaliyotolewa na wananchi na kutoa mfano wa Tume ya Nyalali ambayo alisema ilipokea maoni ya wananchi 21,000 lakini Ripoti ya Tume hiyo ilisheheni mambo muhimu kwa taifa.

Jaji Warioba alifafanua kuwa katika awamu zote nne za mikutano ya kukusanya maoni, wananchi wametoa maoni kuhusu maeneo yote muhimu kama utawala, haki, maadili na mamlaka yao na mengineyo.

Aliongeza kuwa mikutano ya Tume ya kukusanya maoni ililelenga kupata hoja za msingi ili Tume iweze kuandaa Rasimu ya Katiba ambayo itawasilishwa katika mikutano ya Mabaraza ya katiba itakayofanyika kila wilaya.

Akizungumzia hatua inayofuata, Jaji Warioba alisema kuwa kuanzia keshokutwa (Jumatatu, tarehe 7 Januari, 2013), Tume hiyo itaanza kukutana na makundi mbalimbali kwa lengo la kukusanya maoni yao kuhusu Katiba Mpya. Makundi hayo ni Vyama vya Siasa; Vyama vya Kitaaluma; Asasi za Kiraia; Taasisi za Kidini, Vyama vya Wafanyakazi, Wakulima na Wafanyabiashara na makundi mengine mbalimbali.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo, Tume yake imeshawasiliana na makundi hayo na imeandaa utaratibu wa kukutana na wawakilishi wao katika ofisi za Tume na baadhi ya kumbi jijini Dar es Salaam na Zanzibar.

Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilianza kazi rasmi Mei 2 mwaka jana (2012) na kazi ya kukusanya maoni kupitia mikutano imefanyakika kwa awamu nne. Awamu ya kwanza ilifanyika kati ya Julai 2 – 30, 2012 wakati awamu ya pili ilifanyika kuanzia tarehe 27 Agosti – 28 Septemba, 2012. Awamu ya tatu iliyofanyika kati ya terehe 8 Oktoba, 2012 na tarehe 6 Novemba, 2012 na awamu ya nne na ya mwisho ilifanyika kati ya tarehe 19 Novemba – 19 Disemba mwaka jana (2012).

Friday, January 4, 2013

WATATU WAFA AJALINI ARUSHA

ARUSHA

Watu watatu wamefariki hapo hapo baada ya gari walimokuwa wanasafiria aina ya Fuso lenye namba T 526 AVZ kupinduka eneo la kilimatembo wilayani Karatu na dereva kujeruhiwa vibaya wakati wakitokea Serengeti Moa wa Mara kwenda Arusha.

Akizungumza na wanahabari ofisini kwake Kamanda wa jeshi la polisi mkoani hapa Liberatus Sabas aliwataja waliokufa kuwa ni Peter Herman 40 ,Ramadhani Hamza 45 na Peter Kimaro 40 ,wote ni wakazi wa mkoa wa Arusha. Kamanda Sabas alimtaja pia Dereva wa gari hilo Ombeni Urassa kuwa alipata majeruhi kwenye ajali hiyo na anaendelea kupatiwa matibabu kwenye hospitali ya Selian iliyopo jijini hapa.
 
Kamanda wa polisi Liberatus Sabas
Sabas alisema kuwa chanzo cha ajali hakijajulikana na ajali hiyo ilitokea kwenye mteremko wa kilimatembo na lilikuwa likitokea wilyani Serengeti kuja wilaya ya Meru mkoani hapa huku akisema kuwa jeshi la polisi mkoani hapa linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo.

Wakati huo huo jeshi la polisi mkoani hapa limetoa pongezi kwa wananchi mkoani hapa kwa kutoa ushirikiano kwenye ulinzi shirikishi wakati wote wa kipindi cha sikukuu na kuwataka kuendelea kutoa ushirikiano katika kupambana na vitendo vya uhalifu kwenye maeneo ya yao.

Kamanda Sabas alisema kuwa wananchi walisherekea sikukuu za mwisho wa mwaka bila ya matukio ya kutisha na kuwa hakukuwa na wimbi la uhalifu wa kutishia amani ya wananchi na usalama wa mali zao.

RAIS KIKWETE AKUTANA NA MSHAURI WA KIJESHI WA UN



Rais Jakaya Mrisho Kikwete akipeana mikono na Mshauri Mkuu wa Kijeshi wa Umoja wa Mataifa Luteni Generali Babacar Gaye baada ya kuonana naye Ikulu jijini Dar es salaam leo Januari 4, 2013.Kushoto Mbele ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mhe Mahadhi Mahadhi Juma Maalim, akifuatiwa na Mkuu wa Majeshi Tanzania  Jenerali Davis Mwamunyange, na wa pili kulia ni Balozi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa Balozi Tuvako Manongi na wengine ni maafisa waandamizi katika JWTZ na Umoja wa mataifa.


Rais Jakaya Mrisho Kikwete katika picha ya pamoja  na Mshauri Mkuu wa Kijeshi wa Umoja wa Mataifa Luteni Generali Babacar Gaye baada ya kuonana naye Ikulu jijini Dar es salaam leo Januari 4, 2013.Kushoto Mbele ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mhe Mahadhi Juma Maalim, akifuatiwa na Mkuu wa Majeshi Tanzania Jenerali Davis Mwamunyange, na wa pili kulia ni Balozi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa Balozi Tuvako Manongi na wengine ni maafisa waandamizi katika JWTZ na Umoja wa mataifa.


Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiwa  na Mshauri Mkuu wa Kijeshi wa Umoja wa Mataifa Luteni Generali Babacar Gaye baada ya kuonana naye Ikulu jijini Dar es salaam leo Januari 4, 2013.Kushoto ni  Mkuu wa Majeshi Tanzania Jenerali Davis Mwamunyange.

PICHA NA IKULU YA TANZANIA

BOKO HARAM WAFANYA MAUAJI NIGERIA


MAIDUGURI

Watu 13 wameuawa Kaskazini Mashariki mwa Nigeria wakati wa makabiliano ya siku mbili na Waasi wa Kundi la Kiislamu lenye Msimamo Mkali la Boko Haram

Polisi nchini Nigeria imesema mapema leo kuwa Askari aliyekuwa na Bunduki aliingia siku ya Jumatano aliingia katika Mji wa Marte ulio jangwani usiofikika kirahisi karibu na mipaka ya Cameroon na Chad akiwa na miripuko na kuzua hofu kubwa. Jeshi la Serikali limekabiliana  kwa siku mbili mfululizo katika mji huo ulio umbali wa kilometa 100 kutoka Maiduguri na kwamba miripuko hiyo ilikuwa rasmi kwa ajili ya maafisa wa Serikali na Ofisi za Polisi za Adamawa. Itakumbukwa kwamba watu akali ya 50 wameuawa katika eneo hilo lenye utajiri wa mafuta nchini Nigeria na wanamgambo wa Boko Haram wenye mafungamano na Al Qaeda.Jamā'atu Ahlis Sunnah Lādda'awatih wal-Jihad  hujulikana zaidi kama Boko Haram kwa lugha ya Kihausa ambapo watu 3000 wameuawa miaka 3 iliyopita na kundi hilo.