Watu watatu wamefariki hapo hapo baada ya gari walimokuwa wanasafiria aina ya Fuso lenye namba T 526 AVZ kupinduka eneo la kilimatembo wilayani Karatu na dereva kujeruhiwa vibaya wakati wakitokea Serengeti Moa wa Mara kwenda Arusha.
Akizungumza na wanahabari ofisini kwake Kamanda wa jeshi la polisi mkoani hapa Liberatus Sabas aliwataja waliokufa kuwa ni Peter Herman 40 ,Ramadhani Hamza 45 na Peter Kimaro 40 ,wote ni wakazi wa mkoa wa Arusha. Kamanda Sabas alimtaja pia Dereva wa gari hilo Ombeni Urassa kuwa alipata majeruhi kwenye ajali hiyo na anaendelea kupatiwa matibabu kwenye hospitali ya Selian iliyopo jijini hapa.
Kamanda wa polisi Liberatus Sabas |
Sabas alisema kuwa chanzo cha ajali hakijajulikana na ajali hiyo ilitokea kwenye mteremko wa kilimatembo na lilikuwa likitokea wilyani Serengeti kuja wilaya ya Meru mkoani hapa huku akisema kuwa jeshi la polisi mkoani hapa linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo.
Wakati huo huo jeshi la polisi mkoani hapa limetoa pongezi kwa wananchi mkoani hapa kwa kutoa ushirikiano kwenye ulinzi shirikishi wakati wote wa kipindi cha sikukuu na kuwataka kuendelea kutoa ushirikiano katika kupambana na vitendo vya uhalifu kwenye maeneo ya yao.
Kamanda Sabas alisema kuwa wananchi walisherekea sikukuu za mwisho wa mwaka bila ya matukio ya kutisha na kuwa hakukuwa na wimbi la uhalifu wa kutishia amani ya wananchi na usalama wa mali zao.
No comments:
Post a Comment