Thursday, September 19, 2013

MWAKYEMBE ADANGANYWA

Chama cha Wamiliki wa Mabasi Nchini(Taboa), kimesema Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe, alidanganywa kuhusu ubora wa magari ya Toyota Noah kuhusu kuruhusu magari hayo kubeba abiria.
 
Kauli hiyo ya Taboa inafuatia hatua ya Dk Mwakyembe kuruhusu magari hayo kubeba abiria na kufanya safari zenye umbali wa zaidi ya kilometa 50, jambo wanalodai ni kinyume cha sheria.
Uamuzi huo wa Dk Mwakyembe aliutoa bungeni mjini Dodoma, ikiwa ni siku moja baada ya kukutana na wawakilishi wa chama cha magari hayo waliofunga safari kwenda kumuona.
Hata hivyo Katibu Mkuu wa Taboa, Enea Mrutu alisema jana kuwa, uamuzi huo wa Dk Mwakyembe utasababisha kuparaganyika kwa huduma ya usafiri kwa baadhi ya mikoa.
“Wamiliki wa mabasi makubwa wameanza kuondoa magari yao kwa baadhi ya barabara na hii itasukuma nauli kupanda na tayari Toyota Noah wameomba kupandisha nauli,” alisema.
Mrutu alisema, uwezo wa magari hayo ni kubeba abiria wanane hivyo ni hasara gari kwenda umbali mrefu na ndiyo maana wameomba kupandisha nauli jambo litakaloumiza wananchi.
Alisema uamuzi wa Dk Mwakyembe hauungwi mkono na Shirika la Viwango (TBS) na Mamlaka ya Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra) kutokana na ubora wa magari hayo.
“Tumeshaomba appointment (miadi) ya kukutana na Waziri (Dk Mwakyembe) ili kumsihi arudi kwenye mstari wa sheria kwa maslahi ya nchi na Watanzania,” alisema Mrutu.
Akiwa Dodoma, Dk Mwakyembe pia aliiagiza Sumatra kufikiria ombi la wamiliki wa magari ya Toyota Noah kubeba abiria 10 badala ya wanane, jambo ambalo Taboa wanasema ni hatari.

No comments:

Post a Comment