Wazazi hao hawafurahishwi na kuongezeka kwa uhakika wa wahitimu wa darasa la saba kuendelea na kidato cha kwanza, ambao umeelezwa kuwakosesha watoto wao muda wa kufanya shughuli za shamba.
Wakizungumza na gazeti hili katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo, walimu, wanafunzi na viongozi wa serikali, walikiri kuwepo kwa tatizo hilo.
Walitoa mifano ya baadhi ya wazazi waliowahi kuchukuliwa hatua, baada ya kushawishi watoto wao wafeli mitihani. Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Ntoyoyo katika kijiji cha Nyakasanda wilayani Kibondo, Amos Mabula alisema tatizo hilo lipo na limekuwa kikwazo kwa baadhi ya watoto wenye uwezo darasani katika kufanya vizuri kwenye mitihani yao ya kumaliza elimu ya msingi.
Mabula alisema kuwa ana muda mfupi tangu ahamie katika shule hiyo, lakini habari ambazo amezipata kutoka kwa wanafunzi na walimu wenzake ni za wazazi kushawishi watoto wao kujibu vibaya mitihani yao ya mwisho, ili wafeli na kushindwa kuendelea na masomo ya sekondari.
Katika kuthibitisha hilo, Mwalimu Mabula alimwita mmoja wa wanafunzi hao, anayesoma darasa la sita katika Shule ya Msingi Nyakasanda, ambaye alidai wazazi wake wamewahi kufanya jambo hilo kwa dada yake.
Mwanafunzi huyo alidai kuwa dada yake (jina limehifadhiwa) aliyemaliza darasa la saba shuleni hapo mwaka 2011, alifanya vibaya kwenye mitihani ya kumaliza darasa la saba na kushindwa kuendelea na masomo ya sekondari.
Alisema kwa sasa dada yake huyo yuko nyumbani akiwasaidia wazazi wake kazi za vibarua shambani na biashara za mpakani mwa Tanzania na Burundi.
Alidai kuwa dada yake huyo, alikuwa na uwezo darasani na alikuwa akishika nafasi kati ya kwanza na tano na hakuwahi kushuka hapo.
Lakini, alisema mama yao alimwambia dada yake afanye vibaya kwenye mitihani yake ili afeli, kwani hawataweza kumsomesha masomo ya sekondari. Mwaka huo, wanafunzi wanane walifaulu kuendelea na masomo ya sekondari katika shule hiyo, na kumwacha msichana huyo akiwa amefeli. Jambo, hilo liliwashangaza walimu na walipomhoji imekuwaje, alieleza kwamba alipata maelekezo ya wazazi wake kufanya hivyo.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mkarazi, Asumwisye Peter, alisema baadhi ya wazazi wamekuwa tatizo kubwa katika kusimamia taaaluma za watoto wao, kwani wazazi wengi katika eneo hilo hawataki watoto wao waendelee na masomo ya sekondari.
Mwalimu Peter alisema aliwahi kukumbana na tatizo hilo katika Shule ya Msingi Nyange na Shule ya Msingi Mabamba, ambako amewahi kufanya kazi, baada ya matokeo ya baadhi ya wanafunzi katika mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka jana kutia shaka.
Alisema katika kutafuta kiini cha kufeli kwa wanafunzi hao walikuwa na uwezo darasani, alimtafuta mmoja wa wanafunzi hao ambaye alimwambia kuwa alifeli kwa sababu alijibu hovyo hovyo kwenye mitihani yake, kama alivyoambiwa na wazazi wake.
Hatua Ofisa Elimu ya Msingi katika Halmashauri ya Wilaya Kibondo, John Kasigwa, amekiri kuwepo kwa tatizo hilo.
Alitoa mfano wa mtihani wa mwaka 2011, ambapo mwanafunzi mmoja alipewa maelekezo ya kufanya hivyo na wazazi wake. Hata hivyo alisema kuwa mwanafunzi huyo alitoa taarifa kwa walimu, ambao waliutaarifu uongozi wa wilaya na mzazi wa mwanafunzi huyo, alikamatwa na kufikishwa Polisi.
Kesi hiyo ilifikishwa pia kwa Mkuu wa Mkoa Kigoma, Issa Machibya. Mkuu wa Wilaya Kibondo, Venance Mwamoto, alisema kuwa tatizo hilo lipo kwa shule za msingi zilizopo katika mwambao wa mpaka wa wilaya hiyo na nchi jirani ya Burundi.
Alisema alishawahi kukumbana na tukio la mwanafunzi ambaye wazazi wake walitaka afanye vibaya kwenye mitihani yake ya kumaliza elimu ya msingi, lakini mwanafunzi huyo alifanya vizuri na kufaulu. Mwamoto alisema mwanafunzi huyo alifika ofisini kwake na kutoa taarifa kuhusu wazazi wake kugoma kumlipia ada, kwa sababu amefaulu kinyume na matakwa yao.
Mkuu huyo wa wilaya alisema tatizo hilo kwa kiasi kikubwa linatokana na mwamko duni wa elimu wa wakazi wengi wa wilaya hiyo, na kwamba anatarajia kuitisha kikao cha wadau wa elimu kuzungumzia changamoto inayoikabili sekta ya elimu katika wilaya hiyo.
Alisema kuwa pamoja na kikao cha wadau wa elimu, pia ataitisha kikao cha viongozi wa dini zote ili wasaidie kuhimiza umuhimu wa elimu ya watoto kwa wakazi wa wilaya hiyo ambao wanapenda kuhudhuria kwenye nyumba za ibada.
Baaadhi ya wananchi na viongozi wa serikali za vijiji wamekiri kuwepo kwa tatizo hilo na kusema kuwa kwa kiasi kikubwa linachangiwa na hali duni ya kipato cha wananchi wa wilaya hiyo na hivyo kutoona umuhimu wa elimu kwa watoto wao kutokana na kuwatumia watoto hao katika shughuli za kiuchumi kwa ajili ya kipato cha familia.
CHANZO: HABARILEO
No comments:
Post a Comment