Monday, April 22, 2013

SERIKALI YATENGA BILIONI 326 KUWAKOPESHA WANAFUNZI 95,902 WA ELIMU YA JUU NCHINI KWA MWAKA 2012/13.


SERIKALI imetenga shilingi Bilioni 326.0 katika mwaka wa masomo 2012/2013 kwa ajili ya kuwakopesha wanafunzi 95,902 wakiwemo wanafunzi wa mwaka wa kwanza, ikilinganishwa na kiasi cha Shilingi Bilioni 56.1 kilichokuwa kimetengwa mwaka wa masomo 2005/2006 kilichomudu kukopesha wanafunzi 42,729.

1
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi,
Mhe. Philipo Mulugo
 Kauli hiyo imetolewa leo Bungeni mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Mhe. Philipo Mulugo wakati akijibu swali la  Mhe. Rashid Ali Abdallah Mbunge Jimbo la Tumbe alilotaka kujua kwanini Serikali imeshindwa kuwapatia mikopo baadhi ya Wanafunzi wenye sifa za kuendelea na masomo na Serikali ina mpango gani wa makusudi kuhakikisha kuwa Wanafunzi hao wanapata elimu.

Alisema kuwa ongezeko hilo la fedha ni ishara tosha kuwa Serikali ina nia ya kuhakikisha kuwa wanafunzi wote wenye sifa za kusoma Vyuo vya Elimu ya Juu wanapata mikopo itakayowawezesha kupata elimu yao katika mazingira mazuri.

 “Serikali ina nia njema ya kuhakikisha kuwa kila Mtanzania mwenye uwezo wa kusoma Chuo cha Elimu ya Juu anapata fursa hiyo”. Naibu Waziri Mulugo alisema. Aliongeza kuwa kwa mwaka wa masomo 2012/2013, wanafunzi wa mwaka wa kwanza waliowasilisha maombi ya kupata mkopo walikuwa 37,315, baada ya uchambuzi kufanyika wanafunzi waliobainika kuwa na sifa ya kukopeshwa walikuwa 34,140 lakini kati ya hao ni wanafunzi 30,319 sawa na asilimia 88.9 walipata mikopo.
 
“Kwa mantiki hii wanafunzi waliokosa mikopo ni 3,821 sawa na asilimia 11.1 ya wanafunzi wote walioomba mkopo, wanafunzi hawa wachache walikosa mikopo hiyo kutokana na ukomo wa kibajeti pamoja na vipaumbele vilivyowekwa na Serikali”. Mhe. Mulugo alisema.

Na Benedict Liwenga-Maelezo, Dodoma.

No comments:

Post a Comment