JUMLA ya wanariadha wapatao 300 wameshathibitisha kushiriki mbio za kumbukumbu za kifo cha hayati Waziri Mkuu na mpambanaji wa uhuru wa nchi hii, Edward Moringe Sokoine ambazo zinatarajiwa kufanyika Aprili 12 wilayani Monduli, Mkoani Arusha.
Wanariadha kutoka katika mikoa ya, Kilimanjaro, Manyara, Tanga, Dar es salaam na Arusha wameshathibitisha kushirki katika mbio hizo za kwanza kufanyika katika historia ya nchi hii tangu uhuru.
Hayo yamebainishwa na mratibu wa mbio hizo ambaye pia ndiye mwongozaji wa mbio hizo, Wilhelm Gidabuday akizungumza, kwa njia ya simu kutoka Dar es salaam na kusema kwamba tayari kupitia ofisi za chama cha Riadha mkoa Arusha (ARAA), wamethibitisha kushiriki mbio hizo.
Gidabuday alisema kuwa kujitokeza kwa wanariadha hao ni ishara nzuri kwani pamoja na kwamba ndio mara ya kwanza, kwa muitikio huo, wanatarajia kuwa na washiriki zaidi ya 500.
Kuhusu zoezi la usajili, Gidabuday alisema kuwa zoezi hilo litaanza mapema baada ya sikuukuu za Pasaka kumalizika na kuongeza kuwa zoezi hilo litafanyikia katika Ofisi za ARAA, zilizoko katika uwanja wa mpira wa miguu wa Sheikh amri Abeid jijini Arusha kwa ada ya sh. 2000 za Tanzania.
Sokoine Marathon inatarajia kukukutanisha watu wa kada mbalimbali, wakiwemo viongozi, wabunge, mawaziri na wananchi kwa ujumla kuadhimisha kumbukumbu ya kifo cha Hayati Waziri Mkuu wa Tanzania, Edward Moringe sokoine yatakayofanyika Aprili 12, wilayani Monduli katika kijiji alichozaliwa na kuzikwa.
Mbio hizo za umbali wa Kilomita 10 na kilomita 2 kutembea na kukimbia maandalizi yake kwa mujibu wa Waratibu wake mpaka sasa zimeshafikia hatua nzuri na kwa mujibu wa Waratibu wake, hatua zinazofanyika ni kufanya mazungumzo na Mgeni Rasmi ambaye kuna uwezekano akawa mmoja wa viongozi wakuu wa taifa hili.
Mwandishi: FADHIL ATHUMAN
Mhariri: JOHNSON JABIR
No comments:
Post a Comment