Sunday, March 24, 2013

POLISI ALIYEAUA NAYE AUAWA

ASKARI Polisi PC Yohana mwenye namba 7771 amemuua kwa kumpiga risasi mwendesha bodaboda, Makisio Ngonyani (27), kisha naye akauawa na watu wenye hasira kwa kutumia mawe na mbao.


https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEjYRpLaTUORv-H3a6MGSfB1EHIQXPj0TjQCuCNb3wJ7pyZB2NKG0slR3jbMNUEJgvau9olX5c5A12m4O5bdEWLNLQVcOcc2_CCvuyGSOTy-sSuLH_Aj57OId-oe2igyx9j5qI8-PNaV_RsT/s400/ofisi+ya+rpc+copy.jpg
Tukio hilo la kusikitisha lilitokea jana katika eneo la Ngwinde wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma.

Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, lilitokea majira ya saa 8 mchana jana ambapo PC Yohana na mwenzake PC Venance Kamugisha wa kituo kikuu cha polisi cha wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, walikuwa katika doria ya kawaida.

Walipofika katika Kijiji cha Litola na kupata chakula cha mchana kwenye moja ya migahawa iliyopo hapo, walianza kazi ya doria ya kawaida ambapo alitokea mwendesha bodaboda huyo akiwa amebeba abiria wawili kinyume na sheria ya usalama barabarani na walipomsimamisha, hakutii amri hiyo huku kundi jingine la waendesha bodaboda likiwazuia askari hao kufanya kazi yao.

Kwa mujibu wa mashuhuda hao, hali hiyo ilimfanya PC Yohana kufyatua risasi iliyompata mmoja wa abiria kwenye kidole cha mkono na kisha kupitiliza na kumpiga Ngonyani kichwani na kusababisha kifo chake papo hapo.

Baada ya tukio hilo, askari hao walikimbia na pikipiki waliyokuwa nayo, huku wakifukuzwa na kundi la waendesha bodaboda wengine hadi katika Kijiji cha Ngwinde ambapo waliwazingira na kumpiga kwa mawe PC Yohana na kumsababishia kifo huku wakimjeruhi PC Kamugisha ambaye alikimbizwa katika hospitali ya Mkoa wa Ruvuma mjini Songea.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma, Deusdedit Nsimeki aliliambia gazeti hili kwa njia ya simu akiwa eneo la tukio kwamba askari huyo aliuawa kwa kutumia mawe na mbao.
CHANZO: TANZANIA DAIMA

No comments:

Post a Comment