Monday, January 14, 2013

PONGEZI UONGOZI MPYA KATAVI

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linatoa pongezi kwa uongozi mpya wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Katavi (KAREFA) uliochaguliwa katika uchaguzi uliofanyika jana (Januari 13 mwaka huu).

Ushindi waliopata viongozi waliochaguliwa kuongoza chama hicho unaonesha jinsi wajumbe wa Mkutano Mkuu wa KAREFA walivyo na imani kubwa kwao katika kusimamia mchezo huo mkoani Katavi.

TFF inaahidi kuendeleza ushirikiano wake kwa Kamati ya Utendaji ya KAREFA chini ya ukatibu wa Peter Hella aliyeibuka mshindi katika uchaguzi huo uliofanyika ukumbi wa DC mjini Mpanda kwa kumshinda Emmanuel Chaula kwa kura sita dhidi ya mbili.

Uongozi huo mpya una changamoto nyingi, kubwa ikiwa ni kuhakikisha unaendesha shughuli za mpira wa miguu mkoani Katavi kwa kuzingatia katiba ya KAREFA pamoja na vyombo vya mpira wa miguu vilivyo juu yake.

Pia tunatoa pongezi kwa Kamati ya Uchaguzi ya KAREFA na Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa kuhakikisha uchaguzi huo unaendeshwa kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF.

Viongozi waliochaguliwa ni Hella (Katibu), Elias Mande (Mjumbe wa Mkutano Mkuu TFF) na Deo Bakuba (Mwakilishi wa Klabu TFF). Nafasi ya Mwenyekiti haikuwa na mgombea wakati Mawazo Maso aliyekuwa mgombea pekee wa nafasi ya Makamu Mwenyekiti alipata kura nyingi za hapana. Nafasi zilizo wazi zitajazwa katika uchaguzi mdogo.

Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

No comments:

Post a Comment