Saturday, January 19, 2013

UONGOZI WA MBEYA PRESS WAVULIWA KWA TUHUMA ZA UBADHIRIFU


Uongozi wa Klabu ya Waandishi wa Habari umejiuzulu kutokana na makundi ndani ya viongozi yaliyosababisha ubadhilifu wa fedha.

Duru za Habari kutoka mkoani Mbeya zinasema Wanachama wa Klabu hiyo waliamua kupiga kura ya kutokuwa na imani nao hali iliyowafanya viongozi wengine watokwe na machozi ya huzuni. Chanzo kimoja kimesema taarifa mbili ziliwasilishwa katika mkutano wa Wanachama waandishi Habari moja ikiwa ya kundi moja la viongozi kulipinga kundi jingine la viongozi na taarifa ya wanachama waliowasilishwa na kusomwa na Mwandishi Habari Rashid Mkwinda. Aidha ile ya kundi jingine la viongozi iliwasilishwa na kusomwa na Mwandishi Habari mwanachama wa Klabu hiyo Festo Sikagonamo. Taarifa hizo mbili zimeonyesha kulandana katika chanzo kinachosababisha  makundi ndani ya klabu hiyo mkoani Mbeya kuwa ni tamaa ya fedha huku ikionekana Mwwenyekiti Christopher Nyanyembe na Mtunza Hazina wake Pendo Fundisha wakionena kunyoshewa vidole hali iliyowalazimu kujiuzulu bila kupenda.
 
Hatimaye Uongozi wa Muda umeteuliwa chini ya Mwenyekiti Modest Nkulu. 
MODEST NKULU (ALIYESIMAMA) 
CHANZO: GORDON KALULUNGA, Mbeya

YANGA SC YAIGAGADUA BLACK LEOPARDS 3-2

UTURUKI, Uturuki, Uturuki, naam hizo ndizo zilikuwa shangwe za mashabiki wa Yanga leo kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, baada ya kuifunga timu ngumu kutoka Afrika Kusini, Black Leopard katika mchezo wa kirafiki.
Mkurugenzi wa Masoko wa Benki ya NMB, Imani Kajula akimkabidhi zawadi ya Sh. 500,000 mchezaji bora wa mechi ya leo, Frank Domayo wa Yanga.
 
Yanga iliyokuwa kwenye kambi ya mafunzo nchini Uturuki kwa wiki mbili kabla ya kurejea Dar es Salaam Jumapili iliyopita, imeibuka na ushindi wa mabao 3-2 jioni hii dhidi ya timu hiyo inayoshirki Ligi Kuu ya Afrika Kusini.

Hadi mapumziko, Yanga walikuwa mbele kwa bao 1-0 lililowekwa kimiani na mshambuliaji wake aliyefufua makali, Jerry John Tegete dakika ya 33.

Tegete, alifunga bao hilo kwa mkwaju wa penalti, baada ya kiungo wa kimataifa wa Rwanda, Haruna Hakizimana Niyonzima kuangushwa kwenye eneo la hatari na beki Nkosiyaba Xakane na refa Hashim Abdallah wa Dar es Salaam akatoa adhabu hiyo.

Kipindi cha pili, kocha wa Yanga, Mholanzi Ernie Brandts alifanya mabadiliko, akiwatoa pacha kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) wenye uraia wa Rwanda, Mbuyu Twite na Kabange Twite na kipa Ally Mustafa ‘Barthez’ na kuwaingiza Simon Msuva, Juma Abdul na kipa Said Mohamed.

Mabadiliko hayo, hayakuisaidia Yanga, kwani Leopard walifanikiwa kusawazisha bao hilo dakika ya kwanza tu tangu kuanza kipindi cha pili, lililofungwa kwa kichwa na Humphrey Khoza aliyetumia udhaifu wa mabeki wa timu hiyo ya Jangwani na kumtungua kipa Said Mohamed Kasarama.  
    
Baada ya kufungwa bao hilo, Yanga walicharuka na kufanikiwa kupata bao la pili dakika ya 63, lililofungwa na Frank Domayo aliyeunganisha krosi maridadi ya Niyonzima.

Jerry Tegete aliifungia Yanga bao la tatu dakika ya 72 akiunganisha pasi ya beki Juma Abdul na kuwafanya mashabiki wa timu hiyo waruke kwa shangwe za ‘Uturuki, Uturuki’, kuashiria hayo ni matunda ya ziara ya timu hiyo nchini Uturuki kwa wiki mbili zilizopita.

Beki Nadir Haroub ‘Cannavaro’ alimuangusha kwenye eneo la hatari Humphrey Khoza dakika ya 88 na refa akawapa penalti Leopard ambayo ilikwamishwa kimiani na Rodney Romagalela na kufanya matokeo yawe 3-2.

Katika mchezo huo, kikosi cha Yanga kilikuwa; Ally Mustafa ‘Barthez’/Said Mohamed dk 46, Mbuyu Twite/Juma Abdul dk46, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Athumani Iddi ‘Chuji’, Kabange Twite/Simon Msuva dk 46, Frank Domayo, Jerry Tegete, Didier Kavumbangu/Said Bahanuzi dk75 na Haruna Niyonzima.

Black Leopard; Ayunda Mtshati, Ernort Zaga, Nkosiyaba Xakane, Harry Nyirenda, Humphrey Khoza, Muganga Dyange Jean, Mongezi Bobe, Thomas Madiba/Mhletse Maako, Abbas Amidu, Edgar Manake/Karabo Tshepe na Rodney Romagalela.  (PICHA ZOTE KUTOKA JIACHIE BLOG)

AZAM SC YANYUKWA 2-1 NA AFC LEOPARDS


AZAM FC imeanza vibaya ziara yake ya Kenya, baada ya kufungwa mabao 2-1 kwa tabu na wenyeji AFC Leopard katika mchezo wa kirafiki uliofanyika kwenye Uwanja wa Nyayo, Nairobi, jioni hii.

Mabao ya washindi katika mchezo huo, yalifungwa na Paul Were na Mike Barasa, wakati la Azam lilifungwa na Sammih Hajji Nuhu kwa penalti.

Hata hivyo, Azam itabidi wajilaumu wenyewe kupoteza mchezo huo, kwani walipoteza penalti mbili kupitia kwa Joackins Atudo na Khamis Mcha ‘Vialli’.

Pamoja na kufungwa, Azam ilionyesha soka maridadi jioni ya leo mjini hapa kiasi cha kuwavutia mashabiki wa Kenya, waliojikuta wakiishangilia baada ya kuzimikia soka yao.

Katika mchezo huo, kikosi cha Azam FC kilikuwa; Mwadini Ally, Himid Mao, Samir Hajji Nuhu, Luckson Kakolaki, Joackins Atudo, Abdulhalim Humud/Ibrahim Mwaipopo, Jabir Aiziz/Humphrey Mieno, Salum Abubakar/Kipre Balou, Gaudence Mwaikimba/Brian Umony, Khamis Mcha na Uhuru Suleiman/Abdi Kassim ‘Babbi’

Friday, January 18, 2013

MATAIFA YA AFRIKA KUANZA KESHO JANUARI 19


Kesho ni Ufunguzi wa michuano ya Mataifa ya Afrika kwa mwenyeji Afrika Kusini kufungua na Timu ya Taifa Cape Verde. Na Angola watafungua na Morocco katika kundi A.

Michuano ya Mataifa ya Afrika imeanza kujulikana kwa kasi hususani na watafiti wa soka ulimwengu kwani wamekuwa wakija Afrika kutafuta vipaji kwa ajili ya kucheza soka barani Ulaya na kwingineko.

Maafisa mbalimbali wa vilabu na timu za mataifa mengine wanaendelea kumiminika kwa ajili ya fainali hizi ikiwa ni mara baada ya Kombe la Dunia mwaka 2010 nchini humo ikiwemo kocha Mkuu wa Taifa Stars ambaye ameondoka mapema leo mchana.

Katika kundi A linalofungua kwesho macho yatakuwa kwa nyota Youssef El Arabi raia wa Morocco anayechezea Ligi Kuu Hispania katika klabu ya Granada na upande wa Angola akitazamwa Manucho ambaye huchezea klabu ya Real Valladolid ya Hispania.

Kwa wenyeji Afrika Kusini umahiri wa  May Mahlangu (23) anayechezea klabu ya Helsingborgs ya nchini Sweden ambapo mwaka 2011 alitajwa kuwa mchezaji bora wa Allsveskan huku Cape Verde macho yakitupiwa kwa nyota   Ryan Mendes nyota wa klabu ya Lille ya Ufaransa aliyewaua Kameruni wasishiriki michuano hii mwaka 2013.

Mitanange ya Makundi inaanza hapo kesho Jumamosi Januari 19 na kumalizika Januari 30 mwaka huu.

UN YATHIBITISHA KUSHINDWA KWA MAZUNGUMZO NA IRAN



Mkaguzi mkuu wa nishati ya nyuklia wa Umoja wa Mataifa amethibitisha leo kuwa mazungumzo nchini Iran yameshidwa kufikia makubaliano ya kuchunguza uwezekano wa kufanyika kwa utafiti wa silaha za atomiki katika miaka iliyopita. 
Herman Nackaerts aliwaambia waandishi wa habari katika uwanja wa ndege wa Vienna, kuwa walikubaliana na Iran kukutana tena Februari 12 mjini Tehran. Nackaerts alisema wakati wa ziara yake ya mwisho mjini Tehran mwezi Disemba mwaka jana kuwa alitarajia kufikia makubaliano wiki hii, baada ya juhudi za mwaka mzima ambazo hazikuzaa matunda. Alisema hata wakati wa mazungumzo yaliyomalizika, shirika la kimataifa la kudhibiti kuenea kwa silaha za nyuklia, IAEA, halikuruhusiwa kukitembelea kituo cha Parchin, mojawapo ya vituo ambavyo shirika hilo linataka kuvikagua. Iran inasema kwa kuwa hakuna shughuli yoyote ya kinyuklia iliyofanyika Parchin, shirika la IAEA halina haja ya kukikagua kituo hicho.

Thursday, January 17, 2013

ZAIDI YA MILLION 31.9 ZAGHARAMIA VIFAA LIGI YA MOHAMMED DEWJI, SINGIDA


Mwenyekiti wa CCM jimbo la Singida mjini, Hamisi Nguli (kushoto) akikabidhi vifaa vya michezo kwa kiongozi wa tawi la Mitunduruni.
Foleni ya viongozi wa matawi katika jimbo la Singida mjini wakikabidhiwa vifaa vya michezo kwa ajili ya timu zao kushiriki kombe la MO inayotarajiwa kuanza Januari 20 mwaka huu. (Picha zote na Nathaniel Limu).

Mbunge wa jimbo la Singida mjini,Mohammed Gullam Dewji,ametoa msaada wa vifaa mbalimbali vya michezo vyenye thamani ya zaidi ya shilingi 31.9 vitakavyotumika kwenye ligi ya kombe lake, inayotarajiwa kuanza kutimua vumbi januari 20 mwaka huu.
Vifaa hivyo ni pamoja na jezi pea 854,mipira 122, soksi pea 854 na cloves za magolikipa 61.Vifaa hivyo ni kwa ajili ya timu zitakazoshiriki ligi ngazi ya kitongoji katika jimbo la Singida mjini.Baada ya ligi hiyo,itafuatwa na ligi ngazi ya kata ambayo atakuwa na vifaa vyake pia.
Akizungumza kwenye hafla ya kukabidhi vifaa hivyo,mwenyekiti wa CCM jimbo la Singida mjini, Hamisi Nguli amepongeza mbunge Dewji kwa kuendelea kutoa misaada mikubwa mbalimbali katika jimbo lake kwa lengo la kuendeleza wapiga kura wake na wananchi kwa ujumla.
“Dewji toka awe mbunge wa jimbo la Singida mjini,siku zote yupo karibu zaidi na vijana. Amewasaidia mambo mengi makubwa ikiwemo kuwaendeleza kimichezo na pia ametoa pikipiki kwa ajili ya vijana wa bodaboda watakaojiunga katika vikundi”,alisema.
Awali msaidizi wa mbunge Dewji, Duda Mughenyi,amesema msaada huyo wa vifaa,ni mwendelezo wa Dewji kuhakikisha vijana wanatumia michezo kujiendeleza kimaisha.

WASANII WA FILAMU BONGO KUPELEKWA NIGERIA


 Mkurugenzi wa Mad Mad Entertainment, Yasmin Razak (katikati) akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana kuhusu kampuni yake kuingia mikataba na wasanii wa filamu wa Tanzania watakaokwenda Nigeria na Jmahuri  ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kwa ajili ya kutengeza filamu. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Superior, Issack Kasanga na Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania, Simon Mwakifamba. 
Msanii wa filamu, Steve Nyerere (kulia) akifafanua jambo wakati wa mkutano hupo.Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Superior, Issack Kasanga na Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania, Simon Mwakifamba.  

DAR ES SALAAM, Tanzania
KAMPUNI ya Mad Mad Entertainment iliyopo jijini London nchini Uingereza, imeanzisha program maalum ya kupeleka wasanii wa filamu za bongo nje ya nchi kwa lengo la kukuza sanaa hiyo hapa nchini.
 Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo Yasmin Razak alisema ameamua kufanya kazi na wasanii  hao ili kuleta mabadiliko na kuwakwamua kiuchumi wasanii wa filamu hapa nchini.


 “Kwa muda mrefu niliokaa London sioni kama sanaa hii ina maendeleo, nikafikiria kitu gani nifanye ili  kukuza tasnia hii, katika mkataba na kampuni msanii atakayetengeneza filamu na wasanii wa nje atalipwa kiasi cha sh 50 milioni pamoja na malipo mengine yatakayokuwepo kwenye mkataba, ikiwa ni pamoja na asilimia fulani kwa kila kazi itakayouzwa hapa nchini.

“Nimekuwa nikifanya kazi hiyo na wasanii wengi kutoka Nigeria wakiwemo kina Omotola, Two Face na wengineo na pia Ghana, Congo na hata Uingereza, hivyo nimeonelea kuwa itakuwa vema Tanzania nao kuingia katika mchakato huo,”alisema Razak.

Razak ambaye amewahi kufanya kazi ya filamu na Fally Ipupa,  alitaja vigezo vya msanii atakayechaguliwa ikiwa ni pamoja na umaarufu,  kuijua lugha ya kiingereza, uwezo wa kuigiza na kuuvaa uhusika wowote pamoja na mavazi.

Naye rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania, Simon Mwakifamba aliwataka wasanii hao kujipanga katika kuhakikisha wanaingia kwenye ushindani huo na kuwataka wale watakaochaguliwa kujituma na kuonyesha nidhamu ya uhakika.

“Hapa kuna kuinua vipaji, soko la kimataifa na mengineyo, hivyo ni vema kufanya kazi kikamilifu kwa wale watakaochaguliwa na si kujisahau, wanatakiwa wasanii watatu na tupo katika hatua za awali za mchujo,” alisema
Mwakifamba.

Naye muigizaji Issa Musa maarufu kama Cloud, alisema kuwa lugha itakuwa ni tatizo kubwa kwa wasanii walio wengi, hivyo kuitaka kampuni hiyo iangalienamna ya kuweza kuwasaidia wasanii hao.