Thursday, September 19, 2013

JE, MASTAA WA BONGO WAMEHUSIKA VIPI KATIKA KASHFA ZA MADAWA YA KULEVYA?

Taifa linazidi kutikisika kufuatia idadi kubwa ya vijana kujiingiza katika utumiaji wa madawa ya kulevya. Awali ilianza taratibu lakini miaka ya hivi karibuni, hali imezidi kuwa mbaya.

Starehe za ujana ndiyo chanzo cha yote, vijana wengi wamekuwa wakijikuta wameingia katika matumizi ya madawa ya kulevya kwa kushindwa kudhibiti nguvu za ujana.

Jamii ilikuwa ikiamini kwamba wasanii ndiyo kioo cha jamii, ndiyo maana taasisi mbalimbali hupenda kuwatumia wasanii ili waweze kufikisha ujumbe na kuwaokoa wale wote walioathirikia lakini cha kushangaza, kadiri miaka inavyozidi kwenda, wao ndiyo wamekuwa chanzo cha tatizo, wanatumika kusafirisha na pia wametopea katika matumizi.

MASTAA
Mastaa wamegeuka kuwa ndiyo ‘punda’ wa kusafirisha mizigo ya madawa. Ndiyo wanaongoza kubwia ulevi huo, jamii inabaki kujiuliza kuwa vipi kuhusu kile kizazi ambacho kilikuwa kikiwatazama wao kama kioo chao? Inasikitisha.

UTAJIRI WA HARAKA
Takwimu zinaonesha kwamba, wengi wanajishughulisha na biashara ya kusafirisha madawa hayo ili kusaka utajiri wa haraka.
Wapo waliofanya biashara hiyo kwa miaka mingi na kunusurika na mkono wa sheria lakini baadhi yao wamebanwa katika mikono ya sheria na sasa hawajui hatima ya maisha yao.
Amani linakukumbusha baadhi mastaa ambao taifa lilikuwa likiwategemea katika kujenga taifa kama si kuwakomboa wale ambao wamejitosa katika madawa, badala yake wao ndiyo wakajikuta wamezama katika janga la matumizi au kusafirisha madawa ya kulevya:

AGNESS MASOGANGE
Ni binti mwenye mvuto, umbo lake kila mmoja alilitamani kulitumia katika kazi mbalimbali za sanaa. Muonekano wake ulikuwa kama chachu kwa kuweza kuhamasisha jambo fulani na hata yeye binafsi kujiingizia kipato kupitia kazi ya ‘video queen’ aliyokuwa akiifanya lakini akanaswa akisafirisha madawa ya kulevya nchini Afrika Kusini.
Alinaswa akiwa na madawa ya kulevya kilo 150, Mkuu wa Kitengo cha Kudhibiti na Kupambana na Madawa ya Kulevya nchini, Godfrey Nzowa hivi karibuni akiwa na jopo lake walikwenda kumhoji nchini humo na kuahidi kuwasaka wote waliohusika kumtuma mzigo huo.

MELISA EDWARD
Umaarufu wake haukuwa mkubwa sana lakini alikuwa karibu na mastaa ndipo jina lake lilianza kuchanua.
Baadhi ya watu walimjengea picha ya mbali atakuja kuwa muigizaji mkubwa.
Wakati watu wakiwa na mtazamo huo, akajikuta amenaswa katika mtego mmoja na Masogange nchini Afrika Kusini, naye haijulikani hatima yake hadi pale kesi yao itakaposikilizwa.

REHEMA CHALAMILA ‘RAY C’
Ndani ya Bongo Fleva alikuwa tegemeo, ndoto zake zilizima kama taa. Alikiri kushawishiwa na aliyekuwa mpenzi wake, Lord Eyes na kutopea katika utumiaji wa madawa hayo.
Hivi karibuni ametangaza kuacha na kurejea katika ulimwengu wa kawaida. Akifanikiwa itakuwa vizuri lakini kwa sehemu aliyokuwa amefikia ukilinganisha na jamii ilivyokuwa ikimtazama kama kioo, ilikuwa ikisikitisha sana.

AISHA MADINDA
Anajulikana sana na wapenzi wa muziki wa dansi kama mnenguaji, alizitumikia vyema bendi mbalimbali za dansi hapa nchini. Ndoto yake ilizima ghafla pale alipojitumbukiza katika matumizi ya madawa ya kulevya, alitangaza kuacha hivyo jamii inamtazama kwa karibu kuona kama anaweza kufanikiwa kuacha.

LORD EYES
Huu ni mwamba wa Hip Hop kutoka Arusha, alikuwa mpenzi wa Mwanamuziki Ray C. Anatajwa kuwa mwalimu wa Ray C katika suala zima la matumizi ya madawa ya kulevya. Hadi sasa haieleweki kama bado anatumia au la.

MBWANA MATUMLA
Nguli wa mchezo ya ngumi Bongo, aliwika sana miaka ya nyuma hadi alipoamua kuhamishia makazi yake nchini Ethiopia, awali alidai anakwenda kufanya biashara za kawaida lakini ghafla, ikaripotiwa amenaswa na madawa ya kulevya wiki chache zilizopita.

CHID BENZ
Mkali wa muziki wa Hip Hop nchini, sauti yake na nyimbo zake zilipendwa na wengi. Hakuna ambaye aliweza kufikiri kuwa staa huyu anatumia madawa ya kulevya hadi yeye mwenyewe alipoamua kuweka wazi wiki chache zilizopita.
Mbali na Chid, wapo wasanii wengi wa muziki wa Bongo Fleva ambao wanatajwa kushiriki katika matumizi ya madawa ya kulevya. Tatizo kwa sasa limeongezeka mara dufu na takwimu zinaonesha umri ambao ni hatari zaidi ni vijana kuanzia miaka 15-34.

NINI KIFANYIKE?
Kuna haja ya jamii kushirikiana ili kuitokomeza biashara hiyo ambayo imekuwa ni janga la taifa kwani vijana wengi wanaathirika kila kukicha na matumizi ya dawa za kulevya.

LULU NA RICHIE

KUFUATIA kitendo cha galacha wa sinema za nyumbani, Single Mtambalike ‘Richie’ kumtunza fedha nyingi msanii mwenzake Elizabeth Michael ‘Lulu’ hivi karibuni, warembo wengi wa mjini wamekuwa wakimsumbua wakitaka kuzichuma.
Akizungumza na paparazi wetu Jumanne ya wiki iliyopita, Kinondoni Makaburini, jijini Dar, Richie alikiri kupokea simu nyingi za kina dada tangu siku ile ya uzinduzi wa filamu ya Lulu, Foolish Age uliofanyika katika Ukumbi wa Mlimani City wakimuomba urafiki wa kawaida kumbe wana yao moyoni.
“Duh! Umeipata! Ni kweli kabisa simu ni nyingi siku ile tulikutana na mashabiki wetu wengi sana, wakachukua namba lakini kumbe wengi wao lengo lilikuwa ni kutaka mkwanja, daah Napata usumbufu kweli kwa kupigiwa simu kila dakika,” alisema Richie.

BALOZI MTEULE WA UJERUMAN AKATALIWA TANZANIA

Tanzania imemkataa Balozi mteule wa Ujerumani ambaye alitakiwa kuja kufanya kazi nchini.
Balozi huyo, Margit Hellwig-Boette alikuwa amemaliza muda wake nchini Kenya na alitakiwa kuja kuiwakilisha nchi yake Tanzania.
Balozi Hellwig-Boette alikaririwa na Gazeti la Standard la Kenya akieleza kuwa anajipanga kurudi kwao baada ya kukataliwa na Serikali ya Tanzania.
Balozi Margit Hellwig-Boette
Alipoulizwa juu ya suala hilo, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alikataa kuzungumzia suala hilo akisema: “Watu wa Wizara ya Mambo ya Nje ndio wanaoshughulika na hayo mambo, waulizeni.”
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano cha Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mkumbwa Ally alisema wizara yake haijapata taarifa za kukataliwa kwa balozi huyo.
“Suala hilo linahusu ofisi ya Rais, mambo ya uteuzi ni ya Rais. Wizara ya Mambo ya Nje haina hiyo taarifa na hata kama ingekuwapo hiyo taarifa siyo ya `public’.
“Siyo taarifa ya umma kwa maana kwamba, mchakato wake ni wa siri na hayo mambo hayana kuuliza kwa nini. Ukileta jina la mtu unayetaka aje kuwa balozi likikataliwa, hakuna kuuliza eti ni kwa nini.
“Unachofanya ni kuleta jina jingine, hata Rais hapa akipeleka jina la mtu kwenye nchi nyingine lisiporudi, hakuna kuuliza unachofanya ni kuteua tu jina jingine,” alisema Mkumbwa.
Alikariri Kifungu cha Nne cha Azimio la Vienna ambacho kinaruhusu nchi kukataa balozi wa nchi nyingine bila ya kutoa sababu.
“Nchi inayopeleka balozi katika nchi nyingine inatakiwa kutoa jina mapema kwa nchi nyingine. Hata hivyo, nchi hiyo ina uwezo wa kumkubali au kukataa uteuzi,” kinaelekeza kifungu hicho.
Gazeti hilo la The Standard, lilimkariri Balozi Hellwig-Boette akisema kuwa amekataliwa kuja Tanzania bila ya kuelezwa sababu.
“Ndiyo, Tanzania imekataa uteuzi wangu. Kwa mujibu wa itifaki za kidiplomasia, nchi husika ina haki ya kumkataa mtu aliyeteuliwa kwenda kuwakilisha nchi yake au kumkubali.
Tanzania imenikataa lakini haijatoa sababu yoyote ya kufanya hivyo.
“Nitaondoka Nairobi kurudi Berlin Alhamisi (leo) asubuhi ili nikapangiwe sehemu nyingine,” lilieleza gazeti hilo.
Hivi karibuni aliyekuwa Waziri Mkuu wa Kenya, Raila Odinga aliandaa chakula cha jioni, lengo likiwa ni kumuaga balozi huyo baada ya kumaliza kipindi cha miaka minne akiwa anaiwakilisha Ujerumani nchini Kenya.
Misimamo yake imemponza
Gazeti hilo limesema Hellwig-Botte ambaye alikuwa Balozi wa Ujerumani nchini Kenya tangu mwaka 2009, alikuwa anajulikana kutokana na misimamo yake na hasa kupinga ukiukwaji wa haki za binadamu na mara nyingine kuunga mkono vyama vya upinzani.
Anadaiwa kutokuwa na uhusiano mzuri na Serikali ya Kenya kutokana na msimamo wake wa kuunga mkono Rais wa nchi hiyo, Uhuru Kenyatta na Naibu wake, William Ruto kushtakiwa kwenye Mahakama ya Makosa ya Jinai ya Kimataifa huko The Hague, Uholanzi.

TANZANIA YATENGWA EAC

HATIMAYE Tanzania imewekwa kando rasmi na nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), katika kuunda Shirikisho la Kisiasa litakaloziongoza nchi hizo.

Tayari marais wa nchi hizo, Paul Kagame wa Rwanda, Yoweri Museveni wa Uganda, Uhuru Kenyatta wa Kenya na Pierre Nkurunzinza wa Burundi wamekwishafikia makubaliano ya kuanzisha mchakato wa kuandikwa kwa Rasimu ya Katiba ya Shirikisho la Kisiasa la nchi wanachama wa EAC, bila kuishirikisha Tanzania.

Waziri wa Serikali za Mitaa wa Rwanda, James Musoni, amekaririwa na vyombo vya habari vya nchi hiyo akieleza kuwa makubaliano ya kuanzishwa kwa mchakato wa kuandikwa kwa Rasimu ya Katiba ya Shirikisho la Afrika Mashariki, yalifikiwa Septemba 12 mwaka huu, mjini Kampala na marais wa Rwanda, Kenya na Uganda na hivi karibuni Rais wa Burundi ambaye alialikwa katika mkutano huo na kushindwa kuhudhuria, naye sasa amethibitisha ushirika wake katika shirikisho hilo jipya.

Gazeti la The Sunday Times la Rwanda, limemnukuu Waziri Musoni kuwa marais wa nchi hizo wamekubaliana kukamilisha rasimu hiyo ndani ya muda mfupi.

Musoni ambaye alikiri kushiriki katika mkutano wa marais hao ulioshirikisha pia maofisa waandamizi wa nchi hizo isipokuwa Tanzania, alisema uamuzi uliofikiwa katika mkutano huo ambao ni wa pili kufanyika, ni moja ya maagizo ya uamuzi uliofikiwa kwenye mkutano wa kwanza uliofanyika pia mjini Kampala.

“Tumekubaliana juu ya kanuni za kisheria na mpango mzima utakaotuongoza ili kupata Rasimu ya Katiba itakayoliongoza shirikisho hilo la kisiasa,” alikaririwa Musoni.

Alieleza kuundwa kwa kikosi kazi maalumu kitakachojulikana kwa jina la High Level Task Force (HLTF), ambacho kitajumuisha wataalamu wa nyanja mbalimbali watakaoandika Rasimu hiyo kwa namna ile ile ya ulivyoandaliwa mpango wa Itifaki ya soko la pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Musoni alisema mawaziri wa nchi wanachama waliopangiwa kushughulikia shirikisho hilo, wanatarajiwa kuelezea mwelekeo wa mafanikio ya mpango huo katika mkutano mwingine uliopangwa kufanyika mwishoni mwa mwezi Oktoba huko Kigali Rwanda.

Kwa mara ya kwanza, marais Kagame, Museveni na Kenyatta walikutana kufikia makubaliano ya kuharakisha uundwaji wa shirikisho la kisiasa kwa nchi zao kwa kuondoa vikwazo vya kiuchumi na kuweka hati ya vitambulisho vya pamoja na ushirikiano wa kibiashara sambamba na kuzindua mradi wa ujenzi wa gati ya Bandari ya Mombasa.

Waziri Sitta ashangaa
Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, alipoulizwa kuhusu hatua ya nchi hizo kuanza kuitenga Tanzania kuelekea kwenye Shirikisho la Kisiasa, alisema Katiba ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, ibara ya 7 (e) ya mkataba inaruhusu nchi wanachama kufanya jambo la haraka kama nchi nyingine zinachelewa kufanya hivyo.

Sitta alilieleza MTANZANIA Jumatano kuwa, taratibu za Tanzania haziruhusu kibali cha utambulisho kutumika katika nchi zote wanachama, kwa sababu lazima raia wa nchi wanachama anapoingia Tanzania kufuata taratibu za uhamiaji.

Alisema licha ya hatua zinazochukuliwa na nchi wanachama wa EAC za kuitenga Tanzania katika baadhi ya mambo, itabakia na msimamo wake na haitakubaliana kuingia kwenye Shirikisho la Kisiasa huku masuala ya ushuru wa forodha, soko la pamoja na sarafu moja, hayajatengamaa.

“Huo ndio msimamo wa Tanzania, hivi vitu vinne vilikuwa bado havijakamilika, matumizi yake hayajaenda sawasawa na makubaliano ya kila nchi sasa wanaharakisha Shirikisho la Kisiasa, waache waende kwa sababu Katiba inawaruhusu na wana ajenda zao za siri.

“Hatuoni suluhisho katika suala hilo, ni vigumu kuanza kusuluhisha matatizo ya jumuiya kwa sasa kama ilivyo vigumu kusuluhisha matatizo ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

“Ukitazama sasa tunapambana kuendeleza Muungano na Zanzibar, hili la nchi zote nne litakuwaje? Mali zinatoka nchi nyingine, vivyo hivyo kwa upande wa bidhaa, kwa maana hiyo hatuwezi kufika kwenye shirikisho kabla hatujamaliza vikwazo hivi vingine,” alisema Sitta.

Tanzania yailima barua EAC
Waziri Sitta pia alieleza kuwa Tanzania imeiandikia barua sekretarieti ya baraza la mawaziri wa nchi wanachama wa jumuiya ya Afrika Mashariki, ikilalamikia baadhi ya mambo yanayoendeshwa kwa usiri na baadhi ya nchi katika jumuiya hiyo.

Alisema barua alikabidhiwa katika kikao cha baraza la mawaziri kilichofanyika Agosti 28 mwaka huu, mkoani Arusha, ikitaka wahusika kuweka wazi mambo yanayoendelea ndani ya jumuiya kwa kuzishirikisha nchi zote.

Aidha, Sitta alieleza kuwa wakati barua hiyo ikiwa imekwishawasilishwa kwa Sekretarieti, viongozi ambao wamekubaliana kuanza mchakato wa kuandika Rasimu ya Katiba ya Shirikisho la Kisiasa, wanapaswa kutambua kuwa Katiba itakayopatikana itakuwa batili kwa sababu haikuamuliwa na wananchi wa nchi husika bali watawala.

Chanzo;
Mtanzania

MWAKYEMBE ADANGANYWA

Chama cha Wamiliki wa Mabasi Nchini(Taboa), kimesema Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe, alidanganywa kuhusu ubora wa magari ya Toyota Noah kuhusu kuruhusu magari hayo kubeba abiria.
 
Kauli hiyo ya Taboa inafuatia hatua ya Dk Mwakyembe kuruhusu magari hayo kubeba abiria na kufanya safari zenye umbali wa zaidi ya kilometa 50, jambo wanalodai ni kinyume cha sheria.
Uamuzi huo wa Dk Mwakyembe aliutoa bungeni mjini Dodoma, ikiwa ni siku moja baada ya kukutana na wawakilishi wa chama cha magari hayo waliofunga safari kwenda kumuona.
Hata hivyo Katibu Mkuu wa Taboa, Enea Mrutu alisema jana kuwa, uamuzi huo wa Dk Mwakyembe utasababisha kuparaganyika kwa huduma ya usafiri kwa baadhi ya mikoa.
“Wamiliki wa mabasi makubwa wameanza kuondoa magari yao kwa baadhi ya barabara na hii itasukuma nauli kupanda na tayari Toyota Noah wameomba kupandisha nauli,” alisema.
Mrutu alisema, uwezo wa magari hayo ni kubeba abiria wanane hivyo ni hasara gari kwenda umbali mrefu na ndiyo maana wameomba kupandisha nauli jambo litakaloumiza wananchi.
Alisema uamuzi wa Dk Mwakyembe hauungwi mkono na Shirika la Viwango (TBS) na Mamlaka ya Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra) kutokana na ubora wa magari hayo.
“Tumeshaomba appointment (miadi) ya kukutana na Waziri (Dk Mwakyembe) ili kumsihi arudi kwenye mstari wa sheria kwa maslahi ya nchi na Watanzania,” alisema Mrutu.
Akiwa Dodoma, Dk Mwakyembe pia aliiagiza Sumatra kufikiria ombi la wamiliki wa magari ya Toyota Noah kubeba abiria 10 badala ya wanane, jambo ambalo Taboa wanasema ni hatari.

NDOA YAVUNJIKA KWASABABU YA KUMSALITI MWANAMKE MWINGINE

Hili  ni  tukio  la  kusikitisha, lakini  lenye  mafunzo  kibao  ndani  yake....

Tukio  hilo  lilitoke  mwanzoni  mwa  mwezi wa  nane  mwaka  huu ndani  ya  kanisa  la Pentekoste  la  nchini  Kenya  ambapo  wanandoa  wawili    walikuwa  wakila  kiapo  cha  maisha  mbele  ya  mchungaji  wa  kanisa hilo....

Dakika  chache  kabla  ya  wanandoa  hao  kuapishwa  na  kuruhusiwa  kuvishana  pete, Mchungaji  wa  kanisa  hilo   aliwauliza  waumini  kama  kuna  yeyote  mwenye  pingamizi  la  kufungwa  kwa  ndoa  ya  wapenzi  hao...

Baada  ya  swali  hilo, mwanamke  mmoja  alisimama  na  kuelekea  mbele  ya  kanisa  hilo  huku  akiwa  na  vyeti  mkononi....

Alipomkaribia  mchungaji, mwanamke  huyo  alipaaza sauti  yake  na  kusema  kuwa  ndoa  hiyo  haistahili  kufungwa  kwa  sababu  yeye  na  bwana  harusi  wanamtoto  waliyemzaa  pamoja  na  kwamba  walikuwa  na  mipango  ya  kuoana.
 

J.K AMEAHIDI KUPAMBA NA NA WAUZA UNGA

Rais Jakaya Kikwete
Wakati Rais Jakaya Kikwete akisema Serikali yake haitawatetea Watanzania wanaokamatwa wakijishughulisha na biashara ya dawa za kulevya, Watanzania wawili Agnes Masongange na mwenzake, Melisa Edward jana walinyimwa dhamana na Mahakama Kuu ya North Gauteng katika kesi ya dawa ya kukamatwa na dawa hizo.
Rais Kikwete alisema Serikali yake itakabiliana na biashara hiyo kwa nguvu zote kwa kuwa ni haramu na ni kinyume na sheria za nchi.
Alisema hayo juzi usiku alipokutana na Watanzania wanaoishi katika Jimbo la California, Marekani...“Serikali yangu haitawatetea watu wanaojishughulisha na ubebaji wa dawa za kulevya na kusafirisha nje ya nchi. Hii ni biashara haramu na inavunja sheria za nchi yetu.”
Masogange na Melisa walikamatwa Julai 2, mwaka huu kwenye Uwanja wa Oliver Tambo, Afrika Kusini wakituhumiwa kusafirisha kilo 150 za dawa za kulevya zenye thamani ya Sh6 bilioni.
Aidha, amesema hayo siku chache baada ya meli ya mizigo ya Gold Star iliyosajiliwa nchini kukamatwa na maofisa forodha na askari wa doria wa Italia katika Pwani ya Sicily, Bahari ya Mediterranean ikiwa na tani 30 ya dawa ya kulevya aina ya bangi zenye thamani ya Paundi za Uingereza 50 milioni (Sh125 bilioni).
Pia, Agosti 31, mwaka huu, mshambuliaji nyota wa zamani wa timu ya soka ya Simba na Taifa, Joseph Kaniki ‘Golota’ na bondia Mkwanda Matumla walikamatwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Bole, Addis Ababa walipokuwa wakijiandaa kwenda Paris, Ufaransa wakituhumiwa kubeba dawa za kulevya.
Juzi, Rais Kikwete alisema ni wajibu wa Watanzania wanaoishi ughaibuni kuwa raia wema, kufuata na kuheshimu sheria katika nchi wanazoishi kwa sababu wakizivunja, Serikali yake haitawatetea.
“Ukikamatwa na dawa za kulevya hatukutetei kwa sababu hata sheria za nchi yetu zinazuia biashara hiyo. Sisi hatuwezi kuendelea kuwa na sifa ya kufanya biashara za ovyoovyo kiasi hicho. Serikali itawatetea Watanzania wanaoishi nchi za nje ikiwa wataonewa. Lakini ukifanya biashara ya dawa ya kulevya au kubaka watu hatukutetei kamwe,” alisema.
Masogange na mwenzake Melisa jana walikosa dhamana baada ya kupandishwa kizimbani katika Mahakama Kuu ya North Gauteng, Afrika Kusini kujibu mashtaka ya kusafirisha dawa zinazodaiwa kutumika kutengenezea dawa aina ya amphetamine (maarufu kama tik).
Taarifa kutoka Mahakama hiyo zinaeleza kuwa, Masogange na Melissa walirudishwa rumande na kesi yao itasikilizwa tena Novemba mwaka huu.
Mkuu wa Kitengo cha Kudhibiti Dawa za Kulevya cha Polisi nchini, Kamanda Godfrey Nzowa alithibitisha kuwa watuhumiwa hao walipanda kizimbani jana kujibu mashtaka yanayowakabili ya kusafirisha dawa za kulevya na kwamba wamerudishwa rumande hadi Novemba.

Nzowa alisema alikwenda Afrika Kusini kuwahoji Melisa na Masogange kabla ya kupandishwa kizimbani lakini alisema hawakumpa ushirikiano.
Kamanda huyo alisema imebainika kuwa mzigo walioubeba wasichana hao haukuwa dawa halisi za kulevya, bali kemikali zinazotumika kutengeneza dawa zinazoitwa amphetamine. Kutokana na madai hayo, Nzowa alisema wanaweza kupewa dhamana na kesi yao kuendelea kusikilizwa nchini baada ya yeye (Nzowa) kushauriana na Kitengo cha Dawa za Kulevya cha Afrika Kusini.
Alisema, inawezekana watuhumiwa wakapewa hukumu nyepesi kidogo kutokana na kosa hilo.

MTU MMOJA APOTEZA MAISHA KWA KULIWA NA SIMBA

SAMAHANI KWA PICHA HIZI ZA KUSIKITISHA

 
Hili  ni  tukio  la  kutisha  lililomkumba  mtanzania  mwenzetu  ambaye  ni  mkazi  wa  kijiji  cha  Lionja  kilichoko  wilayani Nachingwea  katika  mkoa  wa  Lindi...
Mtanzania  huyo  alishambuliwa  na  simba  wawili   na  kubakizwa  vipande  vipande   alfajiri  wakati  akielekea  katika  shamba  lake  la  korosh.
Kwa mujibu wa chanzo chetu cha habari, Jina lake halikuweza kufahamika mara moja!


Wanakijiji wakitaharuki baada ya kuuona mwili wa marehemu.