Saturday, January 19, 2013

UONGOZI WA MBEYA PRESS WAVULIWA KWA TUHUMA ZA UBADHIRIFU


Uongozi wa Klabu ya Waandishi wa Habari umejiuzulu kutokana na makundi ndani ya viongozi yaliyosababisha ubadhilifu wa fedha.

Duru za Habari kutoka mkoani Mbeya zinasema Wanachama wa Klabu hiyo waliamua kupiga kura ya kutokuwa na imani nao hali iliyowafanya viongozi wengine watokwe na machozi ya huzuni. Chanzo kimoja kimesema taarifa mbili ziliwasilishwa katika mkutano wa Wanachama waandishi Habari moja ikiwa ya kundi moja la viongozi kulipinga kundi jingine la viongozi na taarifa ya wanachama waliowasilishwa na kusomwa na Mwandishi Habari Rashid Mkwinda. Aidha ile ya kundi jingine la viongozi iliwasilishwa na kusomwa na Mwandishi Habari mwanachama wa Klabu hiyo Festo Sikagonamo. Taarifa hizo mbili zimeonyesha kulandana katika chanzo kinachosababisha  makundi ndani ya klabu hiyo mkoani Mbeya kuwa ni tamaa ya fedha huku ikionekana Mwwenyekiti Christopher Nyanyembe na Mtunza Hazina wake Pendo Fundisha wakionena kunyoshewa vidole hali iliyowalazimu kujiuzulu bila kupenda.
 
Hatimaye Uongozi wa Muda umeteuliwa chini ya Mwenyekiti Modest Nkulu. 
MODEST NKULU (ALIYESIMAMA) 
CHANZO: GORDON KALULUNGA, Mbeya

YANGA SC YAIGAGADUA BLACK LEOPARDS 3-2

UTURUKI, Uturuki, Uturuki, naam hizo ndizo zilikuwa shangwe za mashabiki wa Yanga leo kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, baada ya kuifunga timu ngumu kutoka Afrika Kusini, Black Leopard katika mchezo wa kirafiki.
Mkurugenzi wa Masoko wa Benki ya NMB, Imani Kajula akimkabidhi zawadi ya Sh. 500,000 mchezaji bora wa mechi ya leo, Frank Domayo wa Yanga.
 
Yanga iliyokuwa kwenye kambi ya mafunzo nchini Uturuki kwa wiki mbili kabla ya kurejea Dar es Salaam Jumapili iliyopita, imeibuka na ushindi wa mabao 3-2 jioni hii dhidi ya timu hiyo inayoshirki Ligi Kuu ya Afrika Kusini.

Hadi mapumziko, Yanga walikuwa mbele kwa bao 1-0 lililowekwa kimiani na mshambuliaji wake aliyefufua makali, Jerry John Tegete dakika ya 33.

Tegete, alifunga bao hilo kwa mkwaju wa penalti, baada ya kiungo wa kimataifa wa Rwanda, Haruna Hakizimana Niyonzima kuangushwa kwenye eneo la hatari na beki Nkosiyaba Xakane na refa Hashim Abdallah wa Dar es Salaam akatoa adhabu hiyo.

Kipindi cha pili, kocha wa Yanga, Mholanzi Ernie Brandts alifanya mabadiliko, akiwatoa pacha kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) wenye uraia wa Rwanda, Mbuyu Twite na Kabange Twite na kipa Ally Mustafa ‘Barthez’ na kuwaingiza Simon Msuva, Juma Abdul na kipa Said Mohamed.

Mabadiliko hayo, hayakuisaidia Yanga, kwani Leopard walifanikiwa kusawazisha bao hilo dakika ya kwanza tu tangu kuanza kipindi cha pili, lililofungwa kwa kichwa na Humphrey Khoza aliyetumia udhaifu wa mabeki wa timu hiyo ya Jangwani na kumtungua kipa Said Mohamed Kasarama.  
    
Baada ya kufungwa bao hilo, Yanga walicharuka na kufanikiwa kupata bao la pili dakika ya 63, lililofungwa na Frank Domayo aliyeunganisha krosi maridadi ya Niyonzima.

Jerry Tegete aliifungia Yanga bao la tatu dakika ya 72 akiunganisha pasi ya beki Juma Abdul na kuwafanya mashabiki wa timu hiyo waruke kwa shangwe za ‘Uturuki, Uturuki’, kuashiria hayo ni matunda ya ziara ya timu hiyo nchini Uturuki kwa wiki mbili zilizopita.

Beki Nadir Haroub ‘Cannavaro’ alimuangusha kwenye eneo la hatari Humphrey Khoza dakika ya 88 na refa akawapa penalti Leopard ambayo ilikwamishwa kimiani na Rodney Romagalela na kufanya matokeo yawe 3-2.

Katika mchezo huo, kikosi cha Yanga kilikuwa; Ally Mustafa ‘Barthez’/Said Mohamed dk 46, Mbuyu Twite/Juma Abdul dk46, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Athumani Iddi ‘Chuji’, Kabange Twite/Simon Msuva dk 46, Frank Domayo, Jerry Tegete, Didier Kavumbangu/Said Bahanuzi dk75 na Haruna Niyonzima.

Black Leopard; Ayunda Mtshati, Ernort Zaga, Nkosiyaba Xakane, Harry Nyirenda, Humphrey Khoza, Muganga Dyange Jean, Mongezi Bobe, Thomas Madiba/Mhletse Maako, Abbas Amidu, Edgar Manake/Karabo Tshepe na Rodney Romagalela.  (PICHA ZOTE KUTOKA JIACHIE BLOG)

AZAM SC YANYUKWA 2-1 NA AFC LEOPARDS


AZAM FC imeanza vibaya ziara yake ya Kenya, baada ya kufungwa mabao 2-1 kwa tabu na wenyeji AFC Leopard katika mchezo wa kirafiki uliofanyika kwenye Uwanja wa Nyayo, Nairobi, jioni hii.

Mabao ya washindi katika mchezo huo, yalifungwa na Paul Were na Mike Barasa, wakati la Azam lilifungwa na Sammih Hajji Nuhu kwa penalti.

Hata hivyo, Azam itabidi wajilaumu wenyewe kupoteza mchezo huo, kwani walipoteza penalti mbili kupitia kwa Joackins Atudo na Khamis Mcha ‘Vialli’.

Pamoja na kufungwa, Azam ilionyesha soka maridadi jioni ya leo mjini hapa kiasi cha kuwavutia mashabiki wa Kenya, waliojikuta wakiishangilia baada ya kuzimikia soka yao.

Katika mchezo huo, kikosi cha Azam FC kilikuwa; Mwadini Ally, Himid Mao, Samir Hajji Nuhu, Luckson Kakolaki, Joackins Atudo, Abdulhalim Humud/Ibrahim Mwaipopo, Jabir Aiziz/Humphrey Mieno, Salum Abubakar/Kipre Balou, Gaudence Mwaikimba/Brian Umony, Khamis Mcha na Uhuru Suleiman/Abdi Kassim ‘Babbi’

Friday, January 18, 2013

MATAIFA YA AFRIKA KUANZA KESHO JANUARI 19


Kesho ni Ufunguzi wa michuano ya Mataifa ya Afrika kwa mwenyeji Afrika Kusini kufungua na Timu ya Taifa Cape Verde. Na Angola watafungua na Morocco katika kundi A.

Michuano ya Mataifa ya Afrika imeanza kujulikana kwa kasi hususani na watafiti wa soka ulimwengu kwani wamekuwa wakija Afrika kutafuta vipaji kwa ajili ya kucheza soka barani Ulaya na kwingineko.

Maafisa mbalimbali wa vilabu na timu za mataifa mengine wanaendelea kumiminika kwa ajili ya fainali hizi ikiwa ni mara baada ya Kombe la Dunia mwaka 2010 nchini humo ikiwemo kocha Mkuu wa Taifa Stars ambaye ameondoka mapema leo mchana.

Katika kundi A linalofungua kwesho macho yatakuwa kwa nyota Youssef El Arabi raia wa Morocco anayechezea Ligi Kuu Hispania katika klabu ya Granada na upande wa Angola akitazamwa Manucho ambaye huchezea klabu ya Real Valladolid ya Hispania.

Kwa wenyeji Afrika Kusini umahiri wa  May Mahlangu (23) anayechezea klabu ya Helsingborgs ya nchini Sweden ambapo mwaka 2011 alitajwa kuwa mchezaji bora wa Allsveskan huku Cape Verde macho yakitupiwa kwa nyota   Ryan Mendes nyota wa klabu ya Lille ya Ufaransa aliyewaua Kameruni wasishiriki michuano hii mwaka 2013.

Mitanange ya Makundi inaanza hapo kesho Jumamosi Januari 19 na kumalizika Januari 30 mwaka huu.

UN YATHIBITISHA KUSHINDWA KWA MAZUNGUMZO NA IRAN



Mkaguzi mkuu wa nishati ya nyuklia wa Umoja wa Mataifa amethibitisha leo kuwa mazungumzo nchini Iran yameshidwa kufikia makubaliano ya kuchunguza uwezekano wa kufanyika kwa utafiti wa silaha za atomiki katika miaka iliyopita. 
Herman Nackaerts aliwaambia waandishi wa habari katika uwanja wa ndege wa Vienna, kuwa walikubaliana na Iran kukutana tena Februari 12 mjini Tehran. Nackaerts alisema wakati wa ziara yake ya mwisho mjini Tehran mwezi Disemba mwaka jana kuwa alitarajia kufikia makubaliano wiki hii, baada ya juhudi za mwaka mzima ambazo hazikuzaa matunda. Alisema hata wakati wa mazungumzo yaliyomalizika, shirika la kimataifa la kudhibiti kuenea kwa silaha za nyuklia, IAEA, halikuruhusiwa kukitembelea kituo cha Parchin, mojawapo ya vituo ambavyo shirika hilo linataka kuvikagua. Iran inasema kwa kuwa hakuna shughuli yoyote ya kinyuklia iliyofanyika Parchin, shirika la IAEA halina haja ya kukikagua kituo hicho.

Thursday, January 17, 2013

ZAIDI YA MILLION 31.9 ZAGHARAMIA VIFAA LIGI YA MOHAMMED DEWJI, SINGIDA


Mwenyekiti wa CCM jimbo la Singida mjini, Hamisi Nguli (kushoto) akikabidhi vifaa vya michezo kwa kiongozi wa tawi la Mitunduruni.
Foleni ya viongozi wa matawi katika jimbo la Singida mjini wakikabidhiwa vifaa vya michezo kwa ajili ya timu zao kushiriki kombe la MO inayotarajiwa kuanza Januari 20 mwaka huu. (Picha zote na Nathaniel Limu).

Mbunge wa jimbo la Singida mjini,Mohammed Gullam Dewji,ametoa msaada wa vifaa mbalimbali vya michezo vyenye thamani ya zaidi ya shilingi 31.9 vitakavyotumika kwenye ligi ya kombe lake, inayotarajiwa kuanza kutimua vumbi januari 20 mwaka huu.
Vifaa hivyo ni pamoja na jezi pea 854,mipira 122, soksi pea 854 na cloves za magolikipa 61.Vifaa hivyo ni kwa ajili ya timu zitakazoshiriki ligi ngazi ya kitongoji katika jimbo la Singida mjini.Baada ya ligi hiyo,itafuatwa na ligi ngazi ya kata ambayo atakuwa na vifaa vyake pia.
Akizungumza kwenye hafla ya kukabidhi vifaa hivyo,mwenyekiti wa CCM jimbo la Singida mjini, Hamisi Nguli amepongeza mbunge Dewji kwa kuendelea kutoa misaada mikubwa mbalimbali katika jimbo lake kwa lengo la kuendeleza wapiga kura wake na wananchi kwa ujumla.
“Dewji toka awe mbunge wa jimbo la Singida mjini,siku zote yupo karibu zaidi na vijana. Amewasaidia mambo mengi makubwa ikiwemo kuwaendeleza kimichezo na pia ametoa pikipiki kwa ajili ya vijana wa bodaboda watakaojiunga katika vikundi”,alisema.
Awali msaidizi wa mbunge Dewji, Duda Mughenyi,amesema msaada huyo wa vifaa,ni mwendelezo wa Dewji kuhakikisha vijana wanatumia michezo kujiendeleza kimaisha.

WASANII WA FILAMU BONGO KUPELEKWA NIGERIA


 Mkurugenzi wa Mad Mad Entertainment, Yasmin Razak (katikati) akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana kuhusu kampuni yake kuingia mikataba na wasanii wa filamu wa Tanzania watakaokwenda Nigeria na Jmahuri  ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kwa ajili ya kutengeza filamu. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Superior, Issack Kasanga na Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania, Simon Mwakifamba. 
Msanii wa filamu, Steve Nyerere (kulia) akifafanua jambo wakati wa mkutano hupo.Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Superior, Issack Kasanga na Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania, Simon Mwakifamba.  

DAR ES SALAAM, Tanzania
KAMPUNI ya Mad Mad Entertainment iliyopo jijini London nchini Uingereza, imeanzisha program maalum ya kupeleka wasanii wa filamu za bongo nje ya nchi kwa lengo la kukuza sanaa hiyo hapa nchini.
 Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo Yasmin Razak alisema ameamua kufanya kazi na wasanii  hao ili kuleta mabadiliko na kuwakwamua kiuchumi wasanii wa filamu hapa nchini.


 “Kwa muda mrefu niliokaa London sioni kama sanaa hii ina maendeleo, nikafikiria kitu gani nifanye ili  kukuza tasnia hii, katika mkataba na kampuni msanii atakayetengeneza filamu na wasanii wa nje atalipwa kiasi cha sh 50 milioni pamoja na malipo mengine yatakayokuwepo kwenye mkataba, ikiwa ni pamoja na asilimia fulani kwa kila kazi itakayouzwa hapa nchini.

“Nimekuwa nikifanya kazi hiyo na wasanii wengi kutoka Nigeria wakiwemo kina Omotola, Two Face na wengineo na pia Ghana, Congo na hata Uingereza, hivyo nimeonelea kuwa itakuwa vema Tanzania nao kuingia katika mchakato huo,”alisema Razak.

Razak ambaye amewahi kufanya kazi ya filamu na Fally Ipupa,  alitaja vigezo vya msanii atakayechaguliwa ikiwa ni pamoja na umaarufu,  kuijua lugha ya kiingereza, uwezo wa kuigiza na kuuvaa uhusika wowote pamoja na mavazi.

Naye rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania, Simon Mwakifamba aliwataka wasanii hao kujipanga katika kuhakikisha wanaingia kwenye ushindani huo na kuwataka wale watakaochaguliwa kujituma na kuonyesha nidhamu ya uhakika.

“Hapa kuna kuinua vipaji, soko la kimataifa na mengineyo, hivyo ni vema kufanya kazi kikamilifu kwa wale watakaochaguliwa na si kujisahau, wanatakiwa wasanii watatu na tupo katika hatua za awali za mchujo,” alisema
Mwakifamba.

Naye muigizaji Issa Musa maarufu kama Cloud, alisema kuwa lugha itakuwa ni tatizo kubwa kwa wasanii walio wengi, hivyo kuitaka kampuni hiyo iangalienamna ya kuweza kuwasaidia wasanii hao.

SERIKALI YABARIKI FAINALI ZA TAIFA MISS UTALII TANZANIA 2012/13


Serikali ya Jamuhuri ya muungano wa Tanzania, kupitia Baraza la Sanaa la Taifa, limebariki kufanyika kwa Fainali za Taifa za Miss Utalii Tanzania 2012/13 baada ya kuridhishwa na maandalizi yaliyo fanywa na Miss Tourism Tanzania Organisation waandaaji wenye dhima ya kikomo ya kuandaa na kuendesha mashindano hayo kitaifa na kimataifa, pia kwa kuzingatia sheria za nchi, kanuni na Taratibu za mashindano.

Serikali pia imeridhishwa na jinsi Fainali za ngazi za mikoa na kanda zilivyofanyika kwa mafanikio,ambapo kila mkoa umepata washindi wenye sifa za kuwakilisha mkoa husika katika Fainali za Taifa mwaka huu,ambapo jumla ya warembo 60 waingia rasmi kambini kesho katika hoteli ya Ikondelelo Lodge Dar es Salaam, kuanza mbio za kuwania Taji
hilo la Taifa.

Washindi wa 1-5 wa Fainali za Taifa ,watawakilisha Tanzania katika mashindano mbalimbali ya Dunia yakiwemo ya International Miss Tourism World, Miss Tourism United Nation, Miss Heritage World, Miss Tourism University World, Miss Globe International n.k

Miss Utalii Tanzania ,hadi sasa tunashikilia Jumla ya mataji 5 ya Dunia na kimataifa, yakiwemo ya Miss Tourism World 2005-Africa,Miss Tourism World 2006-SADC,Miss Tourism World 2007-Africa, Miss Tourism Model Of The World 2008-Personality n.k

Fainali za Taifa mwaka huu zimepangwa kufanyika wiki ya kwanza ya Februari ,wilaya ya Temeke na mkoa wa Dar es Salaam ukiwa umepewa heshima ya kuwa wenyeji wa Fainali hizo.

Asante,
Erasto Gideon Chipungahelo
Rais

WASHINDI WA PROMOSHENI YA WESTERN UNION WAPATIKANA


 Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Posta Tanzania (TPB), Sabasaba Moshingi, akisoma namba ya mshindi wa zawadi ya sh. miloni mbili ya promosheni ya mwisho ya huduma ya Western Union, itolewayo na benki hiyo, wakati wa kuchezeshwa droo hiyo jijini Dar es Salaam leo. (Picha na Habari Mseto Blog)
 Mkurugenzi Mkuu wa Benki hiyo, Sabasaba Moshingi  akifafanua jambo wakati wa kuchezesha droo hiyo.
 Mkurugenzi Mkuu wa Benki hiyo, Sabasaba Moshingi (katikati) akimsikiliza kwa makini Meneja wa benki hiyo tawi la Kariakoo, Maduhu Bulebi Makoye wakati wa kuchezesha droo hiyo. Kushoto ni Meneja Mkuu Mauzo na Huduma kwa Wateja, Grace Nkuzi. 

Na Mwandishi Wetu
BENKI ya Posta Tanzania (TPB), imetangaza washindi watatu wa promosheni ya Shindano la  kutumia huduma ya Weastern Union, ambalo ni la pili, baada ya lile la mwaka jana.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa Benki hiyo, Sabasaba Moshingi amesema kuwa washindi hao watatu wamepatikana baada ya droo iliyochezeshwa mbele ya waandishi wa habari.

"Washindi hao wametoka katika matawi mbalimbali ya Benki ya Posta nchini ambapo zawadi ya kwanza na ya pili zimebaki jijini Dar es Salaam na ile ya tatu kwenda mkoani Arusha".

Moshingi aliwataja washindi hao kuwa ni pamoja na James Mkondya aliyejinyakulia sh milioni mbili, Ensel Issa, sh milioni mojawote hao wakazi wa jijini na Kaeni Kapangi aliyejinyakulia sh 700,000 mkazi wa Arusha.  

Aidha,  washindi  wengine kumi wamejipatia zawadi ya sh 100,000 kila mmoja.

Moshingi alitoa wito kwa Watanzania kujiunga na huduma za Benki hiyo kwani zimboreshwa na kuwafanya wateja wake kwenda na wakati katika shughuli zao zakujiletea maendeleo.

FILAMU YA REAL PROMISE KUTOKA HIVI KARIBUNI


Na Elizabeth John

KAMPUNI ya Faisal Production ikiwa miongoni mwa taasisi chache zenye lengo maalum la kuhakikisha fani ya filamu inastawi na kupata maendeleo nchini, imeandaa kazi mpya inayokwenda kwa jina la ‘Real Promise’.
 Rose Ndauka

Katika filamu hiyo ambayo tayari imeanza kuwa gumzo la jiji, waigizaji nyota kama Mohammed Mwikongi ‘Frank’, Rose Ndauka, Bambucha na Rania wameshiriki na kufanya makubwa ambayo yatamfanya mtazamaji kutopata muda wa kufanya shughuli nyingine.

Kwa mujibu wa msemaji wa kampuni hiyo, Mohammed Njiriku, filamu hiyo kwa sasa iko katika hatua ya uhariri, akisisitiza kutoa tungo bora kabisa sambamba na kuchezwa vizuri na wahusika.

Real Promise inazungumzia mikasa ya mapenzi na hatua mbalimbali za kukabiliana nayo ikizingatiwa kuwa mapenzi ni sehemu kubwa ya maisha ya kila siku ya binadamu.

Rose, ambaye ameng’ara katika filamu nyingi hapa nchini, amefanya makubwa katika kazi hiyo inayotarajiwa kutoka wakati wowote mwezi huu.

PNC KUFANYA MAGEUZI KATIKA MUZIKI WA KIZAZI KIPYA


Na Elizabeth John
BAADA ya kimya cha muda mrefu, msanii wa muziki kizazi kipya, Pancras Ndaki Charles ‘PNC’, ameibuka na kusema amerudi kufanya mageuzi makubwa katika muziki huo na kumtaka msanii mwenzake Naseeb Abdul ‘Diamond Platinum’ ajiandae kuvaa vumbi.
Pancras Ndaki Charles ‘PNC’

Akizungumza na Habari Mseto Blog, PNC, amesema kuwa ukimya wake haukuwa bure bali alikuwa anajipanga vema na ujio wake mpya umekuja huku Diamond akioneka kuliteka anga la muziki huo na kumtambia kuwa muda si mrefu atamfunika.

“Nilikaa kimya muda mrefu baada ya kutamba na ngoma yangu ya ‘Mbona’ niliyomshirikisha Mr Blue, na kipindi chote nilikuwa najaribu kuangalia jinsi nitakavyoliteka anga la muziki huu, na ujio wangu mpya umekuja wakati Diamond akiwa safi, hivyo asubiri kuvaa vumbi kwani nitampoteza vibaya,” alisema PNC.

PNC anayesimamiwa na meneja wake makini, Ostaz Juma, chini ya lebo ya Mtanashati Entertainment, alisema hivi karibuni anatarajia kuachia ngoma yake mpya ambayo hajataka kuitaja jina kutokana na maharamia waliopo katika tasnia hiyo.

Mmsanii huyo ambaye ndiye kiongonzi wa kundi la Mtanashati Entertainment, anawaomba wadau na mashabiki wa muziki huo kukaa mkao wa kula kwaajili ya kuzipokea kazi zao zinazokuja.

MAOFISA WA CHUO CHA TAIFA CHA ULINZI WATEMBELEA TBL


 Baadhi ya maofisa kutoka Chuo Cha Taifa cha Ulinzi (NDC) kutoka Dar es Salaam wakipata maelezo kutoka kwa Meneja wa Uzalishaji Bia wa Kiwanda cha Bia cha TBL Arusha, Ben Mwanri (wa pili kushoto), walipotembelea Kiwanda cha Bia cha Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) cha Arusha, wakati wa  ziara ya siku moja kujionea shughuli mbalimbali za kiwanda hicho mwishoni mwa wiki.
 Baadhi ya maofisa kutoka Chuo Cha Taifa cha Ulinzi (NDC) kutoka Dar es Salaam, wakiangalia eneo ambapo maji yaliyotumika kiwandani yanachujwa tayari kwa matumizi mengine, walipotembelea Kiwanda cha Bia cha Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) cha Arusha, wakati wa  ziara ya siku moja kujionea shughuli mbalimbali za kiwanda hicho mwishoni mwa wiki.

 Baadhi ya maofisa kutoka Chuo Cha Taifa cha Ulinzi (NDC), Usalama, wakitembelea mwishoni mwa wiki Kiwanda cha Bia cha Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), cha Arusha, walipofanya ziara ya siku moja kujionea shughuli mbalimbali za kiwanda hicho.
 Baadhi ya maofisa kutoka Chuo Cha Taifa cha Ulinzi (NDC), Usalama, wakitembelea mwishoni mwa wiki Kiwanda cha Bia cha Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), cha Arusha, walipofanya ziara ya siku moja kujionea shughuli mbalimbali za kiwanda hicho.
 Baadhi ya maofisa kutoka Chuo Cha Taifa cha Ulinzi (NDC) kutoka Dar es Salaam wakipata maelezo kutoka kwa Meneja wa Uzalishaji Bia wa Kiwanda cha Bia cha TBL Arusha, Ben Mwanri (wa pili kushoto), walipotembelea Kiwanda cha Bia cha Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) cha Arusha, wakati wa  ziara ya siku moja kujionea shughuli mbalimbali za kiwanda hicho mwishoni mwa wiki.
Kiongozi wa ujumbe wa maofisa wa Jeshi kutoka Chuo ChaTaifa cha  Ulinzi (NDC) Mafunzo ya Kijeshi na Usalama, S.M Minja  (kushoto) akimkabidhi zawadi  Meneja wa Uzalishaji Bia wa Kiwanda cha Bia cha TBL Arusha, Ben Mwanri, walipotembelea kiwanda hicho mwishoni mwa wiki.

Mshindi ‘Valentine Day’ kulamba Vitz

Meneja Mauzo na Masoko wa Push Media Mobile, Rodney Rugambo akisisitiza jambo wakati wa uzinduzi wa shindano la kampeni maalum ya kuadhimisha sikukuu ya wapendanao ‘ Valentine Day’ iliyoandaliwa kwa kushirikiana na Kampuni ya African Media group (AMG) kupitia kituo cha televisheni cha Channel Ten na Redio Magic FM. Kushoto ni AFISA Masoko na Mauzo wa AMG,  Prosper Vedasto 




Na Mwandishi Wetu
KAMPUNI ya Push Media Mobile inatarajiwa kutoa zawadi ya gari aina ya Vitz lenye thamani ya sh milioni 8 kwa mshindi wa kampeni maalum ya kuadhimisha sikukuu ya wapendanao ‘Valentine Day’ inayoadhimishwa Februari 14 kila mwaka.

Hayo yalisemwa jijini Dar es Salaam Meneja Mauzo na Masoko wa Push Media Mobile, Rodney Rugambo, katika uzinduzi wa kampeni hiyo pamoja na Kampuni ya African Media Group (AMG), kupitia kituo cha televisheni cha Channel Ten na Redio Magic FM.

Rugambo alisema kuwa, wameamua kutoa zawadi hiyo kubwa ili kuwafanya wapendanao wengi kushiriki na kupata nafasi ya kushinda.

Alisema kuwa, ili kuingia katika droo ya shindano hilo, unatakiwa kutuma neno ‘Penzi’ kwenda namba 15678 na kujibu maswali mbalimbali yahusiyo masuala ya mapenzi na siku ya Valentine.

“Hii ni promosheni ya kwanza kubwa hapa nchini na mshindi kujishindia gari, lengo kubwa ni kutoa ufahamu kuhusiana na sikukuu ya wapendanao na vile vile kuwazawadia wadau wetu kwa kushiriki katika shughuli zao za ujenzi wa taifa,” alisema Rugambo.

Alisema kuwa, mbali ya zawadi hizo, washiriki wa promosheni hiyo pia watapata nafasi ya kujishindia kompyuta (Laptop), aina ya HP yenye thamani ya sh milioni 1.5, simu aina ya Blackberry Curve yenye thamani ya sh 500,000 na ‘Home Theatre’ ya thamani ya sh 400,000.

Kwa mujibu wa Rugambo, lengo lao kubwa ni kuifanya sikukuu ya wapendanao kuwa kubwa kama nyingine, kwani mapenzi ni kitu muhimu katika maisha ya kila siku.

Alisema kuwa, mipango yao ni kuwekeza katika sikukuu hiyo, ambayo jamii imeanza kuitilia mkazo japo si siku ya mapumziko kama sikukuu nyingine, ambako mwaka huu, wameweka bajeti ya sh milioni 30 ili kufanikisha zaoezi hilo.

ALICHOKISEMA NAY WA MITEGO KUHUSU NYIMBO YAKE YA NASEMA NAO



Na Elizabeth John
MSANII wa muziki wa kizazi kipya nchini, Emmanuel Elibariki ‘Nay wa Mitego’ amesema wimbo wake wa ‘Nasema Nao’, ambao unafanya vizuri katika vituo mbalimbali vya redio na runinga, ni hisia zake binafsi na wala hana bifu na mtu.

Akizungumza jijini Dar es Salaam leo, Nay, alisema kuwa alifanikiwa kurekodi wimbo huo baada ya kufika studio na kukuta mapigo bila wimbo, na ndipo alipoamua kufanyia mazoezi kabla ya kuirekodi na kuisambaza.

 Emmanuel Elibariki ‘Nay wa Mitego’
Nay, alisema hakukusudia kumsema mtu, licha ya baadhi ya maneno ya wimbo huo kuwa na majina ya wasanii na viongozi, lakini lengo lake ni kufikisha ujumbe kwa jamii na si vinginevyo.

“Mimi ndiye msanii wa kwanza wa muziki wa kizazi kipya kutaja watu kwenye nyimbo nikiwa na lengo la kufikisha ujumbe ninaoukusudia kwa jamii, na humu simaanishi chochote kibaya,” alisema Nay Wa Mitego.

Mkali huyo wa Bongo Fleva, alisema katika hilo, hana ‘bifu’ na mtu yeyote na hatarajii kusikia akiingia katika malumbano na wasanii waliotajwa katika wimbo huo ambao unafanya vizuri katika redio mbalimbali nchini.

Baadhi ya wasanii waliotajwa katika wimbo huo ni pamoja na Selemani Msindi ‘Afande Sele’,  Hamad Ally ‘Madee’, Chid Benzi na viongozi wengine wa kisiasa.

MZEE MALECELA, WAZIRI MKUU MSTAAFU SUMAYE NA JAJI MKUU MSTAAFU SAMATTA WATOA MAONI KATIBA MPYA LEO


Waziri Mkuu Mstaafu Fredrick Sumaye akiongea na Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba aliokutana nao leo kutoa maoni yake kuhusu Katiba Mpya. Kulia ni Makamu Mwenyekiti wa Tume Jaji Mkuu Mstaafu Augustino Ramadhani na Mjumbe wa Tume Waziri Mkuu Mstaafu Dkt. Salim Ahmed Salim (katikati).
Jaji Mkuu Mstaafu Barnabas Samatta akiongea na Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba aliokutana nao leo kutoa maoni yake kuhusu Katiba Mpya. Kulia ni Mwenyekiti wa Tume Jaji Joseph Warioba.
Waziri Mkuu Mstaafu Mzee John Malecela akipata maelezo kuhusu Kitengo cha Utafiti cha Tume ya Mabadiliko ya Katiba kutoka kwa Mjumbe wa Sekretarieti ya Tume Bw. Mohammed Hamad leo mara baada ya kutoa maoni yake kuhusu katiba Mpya. Kushoto ni Mwenyekiti wa Tume Jaji Joseph Warioba. 
Waziri Mkuu Mstaafu Mzee John Malecela akiongea na Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba aliokutana nao leo kutoa maoni yake kuhusu Katiba Mpya. Kulia ni Makamu Mwenyekiti Jaji Mkuu Mstaafu Augustino Ramadhani na Mjumbe wa Tume Prof. Mwesiga Baregu.
Waziri Mkuu Mstaafu Mzee John Malecela akitoka nje ya ukumbi wa mikutano wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba leo mara baada ya kutoa maoni yake kuhusu katiba Mpya. Kushoto ni Makamu Mwenyekiti Jaji Mkuu Mstaafu Augustino Ramadhani na kulia ni Mjumbe wa Tume Waziri Mkuu Mstaafu Dkt. Salim Ahmed Salim.

Tuesday, January 15, 2013

"NO INTENTION FOR THE ABOLISH OF WITHDRAWINGBENEFITS"


The Minister for Labour and Employment, Gaudensia Kabaka has assured mine workers that the government has no intention to abolish withdrawal benefits in February, this year.

Opening a two-day social security funds stakeholders’ meeting in Mwanza City , Ms Kabaka strongly dismissed rumours that withdrawal benefits would be abolished in February, this year.

“This workshop is held to clear the air on withdrawal benefits, Tanzanians must understand that the government does not intend to abolish withdrawal benefits,” said Ms Kabaka.

She, however, said the government was collecting views from stakeholders to enable social security funds become effective, beneficial and friendlier to all workers.

Minister Kabaka said that the government had already instructed the Social Security Regulatory Authority (SSRA) to withdraw its public notice on withdrawal benefit.

According to her, the government believes that it is important to remove from the law the section that denies members right to withdrawal benefits.

Since the rumours of abolishing withdrawal benefits hit mining sector a few months ago, over 400 workers from Lake Zone major gold mines had tabled resignation letters.

Thomas Sabaya, an official from Tanzania Mining and Construction Workers Union (Tamico) in Geita Gold mine, said over 300 workers had written to have their jobs terminated by the end of 2012.

By MOSES MATTHEW, Tanzania Daily News
The Minister for Labour and Employment, Gaudensia Kabaka has assured mine workers that the government has no intention to abolish withdrawal benefits in February, this year.

Opening a two-day social security funds stakeholders’ meeting in Mwanza City , Ms Kabaka strongly dismissed rumours that withdrawal benefits would be abolished in February, this year.
 
“This workshop is held to clear the air on withdrawal benefits, Tanzanians must understand that the government does not intend to abolish withdrawal benefits,” said Ms Kabaka.
 
She, however, said the government was collecting views from stakeholders to enable social security funds become effective, beneficial and friendlier to all workers.
 
Minister Kabaka said that the government had already instructed the Social Security Regulatory Authority (SSRA) to withdraw its public notice on withdrawal benefit.
 
According to her, the government believes that it is important to remove from the law the section that denies members right to withdrawal benefits.
 
Since the rumours of abolishing withdrawal benefits hit mining sector a few months ago, over 400 workers from Lake Zone major gold mines had tabled resignation letters.
 
Thomas Sabaya, an official from Tanzania Mining and Construction Workers Union (Tamico) in Geita Gold mine, said over 300 workers had written to have their jobs terminated by the end of 2012.
 
By MOSES MATTHEW, Tanzania Daily News

MAKAMU WA RAIS WA TANZANIA ASEMA VIFO VYA MAMA NA WATOTO BADO NI CHANGAMOTO KWA AFRIKA


Makamu wa Rais Dr.Mohamed Gharib Bilal amesema Bara la Afrika bado linachangamoto kubwa katika kuweka sera na mipango itakayosaidia kupunguza vifo vya kina mama hususani katika kipindi cha ujauzito,wakati wa kujifungua na kuzuia vifo vya watoto walio chini ya umri wa 
miaka mitano

Makamu wa Rais ameyasema hayo Jijini Arusha wakati akifungua rasmi mkutano wa pili wa kimataifa unaowakutanisha wataalamu wa masuala ya afya kutoka nchi mbalimbali duniani wakiangazia namna ya kupunguza vifo kwa akinamama wajawazito,wanaojifungua na watoto walio na umri chini ya miaka mitano

Dr.Bilala mesema japokuwa nchi ya Tanzania kwa upande wake imekuwa ikijitahidi kupunguza idadi ya vifo vya watoto lakini takwimu zinaonesha idadi ya vifo vya kinamama bado ipo juu na hivyo ni lazima kuwepo na uwajibikaji katika kuokoa maisha ya akinamama na watoto

Kwa upande wake waziri wa Afya wa Tanzania Dr.Hussein Ally Mwimyi amesema tangu mwanzoni mwa miaka ya 1970 Tanzania imekuwa ikiendesha miradi mbalimbali inayohusu uboreshaji wa afya ya mama na mtoto hali iliyopelekea kwa hivi sasa huduma hizo kutolewa sii tu katika mahospitali bali pia katika vituo mbalimbali vya afya

Awali waratibu wa mkutano huo shirika la Management and development for health (MDH) kupitia kwa mkurugezi wake Dr.Chalamilla Guerino, ameeleza kuwa mkutano huo unatarajiwa kuleta majibu yatakayosaidia kuboresha kuduma na kuhakikisha mama hapotezi maisha wakati wa kuleta uhai.

Monday, January 14, 2013

MIRUNGI "GOMBA" YAKAMATWA ARUSHA


Jeshi la Polisi mkoani Arusha  limewakamata watu wanne wakiwa na madawa ya kulevya aina ya mirungi. Watu hao walikuwa na jumla ya viroba 202 vya dawa hizo  ambazo zilikuwa kwenye gari aina ya Mitsubishi Canter lenye namba za usajili T 306 BUN.
 
Akizungumza na waaandishi wa habari nje ya jengo la Makao Makuu ya Jeshi hilo Mkoani hapa, Kamanda wa Polisi Mkoani humo Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Liberatus Sabas aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Joel Alfayo Lukumay (37), Rahim Azizi Gilla (35), Ibrahimu Solomon Katambwei (40) na Musa Lazaro Mollel (38) wote ni wakazi wa Mkoa wa Arusha.

Alisema tukio hilo lilitokea leo saa 1:00 asubuhi katika eneo la Engikareti lililopo wilayani Longido mkoani hapa. Aliongeza kwa kusema kwamba, mafanikio hayo yametokana na taarifa toka kwa raia wema ambao waliwasiliana na jeshi hilo, ambapo mara baada ya kupata taarifa hiyo waliweka mtego katika eneo hilo na kufanikiwa kulikamata gari hilo ambalo lilikuwa linatokea nchi jirani ya Kenya.

Kamanda Sabas aliwashukuru wananchi wa Mkoa wa Arusha kwa ushirikiano wao  mkubwa unaofanywa kwa jeshi hilo na kuwaomba waendelee kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu kwani kama wananchi wakiamua uhalifu unaweza ukapungua kwa kiasi kikubwa.

Baadhi ya waaandishi na askari waliokuwa kwenye eneo hilo walishuhudia viroba hivyo vikiwa na majina ya watu pamoja na uzito wa kila mzigo huku wengine wakidai kwamba inawezekana gari hilo huwa linabeba mizigo ya watu mbalimbali ambao wanakuja kugawana mara baada ya kuingia Arusha Mjini.

Kutokana na tukio hilo Jeshi la Polisi Mkoani hapa linaendelea kuwahoji watuhumiwa hao na pindi upelelezi utakapokamilika watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili. Aidha taarifa za ndani ya jeshi hilo zinasema kwamba gari hilo lilishawahi kukamatwa tarehe 16 mwezi Machi mwaka jana ambalo lilikutwa na madawa ya aina hiyo na kesi yake ilikwishafikishwa mahakamani na bado shauri hilo bado linaendelea.

WAHINDU WAOGA KATIKA MTO GANGES


Wahindu katika mto Ganges
Mamilioni ya waumini wa madhehebu ya Hindu nchini India wamejitosa katika mto wao mtakatifu, Ganges, kitendo ambacho wanaamini kinawaosha dhambi zote. 
Siku ya leo inachukuliwa kama siku yenye heri kubwa zaidi katika  maadhimisho ya siku 55 yajulikanayo kama Kumbh Mela, ambacho umuhimu wake unatokana na masuala ya kinajimu. Afisa mkuu wa maadhimisho hayo Mani Prasad Mishra amesema kwamba tayari watu milioni tatu wamekwishaingia ndani ya mto Ganges kuanzia asubuhi, na kwamba wanategemea kuwa ifikapo jioni watu milioni kumi na moja watakuwa wamejiosha na maji ya mto huo yenye baridi kali. Wakereketwa wa dini ya Hindu wanaamini kwamba kuoga ndani ya mto Ganges kunaondoa dhambi zao, na kuwaepusha na mzunguko wa kifo na kuzaliwa kwa mara ya pili.

TENGA KUTOGOMBEA TENA URAIS TFF


     Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga amesema hatagombea tena wadhifa huo katika uchaguzi uliopangwa kufanyika Februari 24 mwaka huu.
Leodegar Tenga

Akizungumza na Waandishi wa Habari kwenye ofisi za TFF leo, Rais Tenga amesema wakati anaingia kwenye uongozi mwaka 2004 ajenda ilikuwa na kuijenga TFF kama taasisi kwa kuweka mifumo ya uendeshaji ikiwemo kutengeneza katiba na kanuni, jambo ambalo limefanyika.

“Wajumbe wamekuwa wakiniuliza Rais vipi? Mimi hapana. Nilishafika pale pa kufika. Tulipoanza wakati ule ilikuwa ni kujenga taasisi. Na kazi hiyo tumeifanya. Tulipoingia mwaka 2004 hiyo ndiyo ilikuwa ajenda,” amesema Rais Tenga.

Amesema walitengeneza Katiba, vyombo huru vya kufanya uamuzi, kuongeza wigo wa wapiga kura ambapo hivi sasa kwenye mpira wa miguu hakuwezi kutokea migogoro, hata ikitokea kuna mfumo wa kuidhibiti.

Rais Tenga ameishukuru Sekretarieti ya TFF, Kamati ya Uchaguzi ya TFF, kamati za uchaguzi za wanachama wa TFF na vyama wanachama wa TFF kwa hatua iliyofikiwa katika uchaguzi ambapo mikoa yote imekamilisha uchaguzi na kubaki vyama shiriki pekee.

Ametoa mwito kwa wadau kujitokeza kugombea uongozi TFF, kwani baada ya kujenga taasisi ajenda iliyobaki ni mpira wa miguu wenyewe ikiwemo nini kifanyika ili mpira uchezwe katika maeneo mbalimbali.

“Tumeshatengeza mfumo, sasa ni kuangalia jinsi ya kuendeleza mpira. Changamoto ni tufanye nini ili mpira uendelee. Tunataka watu wengine wabebe hiyo ajenda ili tuangalie tunakwendaje mbele,” amesema.

Pia amesema ushirikiano ambao amepata kwa wapenzi na wadau wa mpira wa miguu ni wa ajabu. Vilevile ameishukuru vyombo vya habari, Serikali, klabu, wadhamini na wafadhili kwa mchango wao katika uendeshaji wa mpira wa miguu nchini.