Saturday, December 29, 2012

UBUNGO BUS TERMINAL KUHAMA JANUARY 15, 2013.


MCHAKATO wa kuhamisha Kituo cha Mabasi yaendayo mikoani na nje ya nchi (UBT), kwenda Mbezi Luis unatarajiwa kuanza Januari 15 mwaka ujao.
 
Akizungumzana wandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Jiji Mussa Zungiza, alisema lengo la kuhamisha kituo hicho ni kwa ajili ya kupisha Mradi wa Mabasi yaendayo Haraka (DART).
 
Kituo kikuu cha mabasi Dar es Salam
Alisema kuhamishwa kwa kituo hicho kutakuwa kwa awamu, kutakakokwenda sambamba na kukamilika kwa ujenzi wa kituo hicho cha Mbezi.
 
"Siyo kweli kama ifikapo Januari tunahamisha au tunasimamisha shughuli zote pale Ubungo la hasha, tutakacho fanya pale tutawakabidhi wajenzi wa mradi huo wa DART ambao nao watachagua maeneo maalumu ya kuanzia shughuli zao, huku maeneo mengine yakiendelea kutoa huduma bila ya kuleta athari katika utoaji huduma”alisema Zungiza.
 
Zungiza alisema hadi sasa pale Mbezi kinachofanyika usafishaji wa eneo hilo la stendi hiyo mpya. Alisema katika awamu hiyo ya kwanza watejenga miundombinu ikiwemo uzio, alama za kuelekeza magari, njia za kuingia na kutoka.
 
“Pengine tunatarajia ndani ya miezi mitano tunaamini awamu yakwanza itakuwa imekamilika”alisema.
 
Zungiza alisema uhamishaji kabisa wa kituo hicho cha Ubungo kutategemea kukamilika kwa ujenzi wa kituo hicho kipya cha Mbezi.

TRELA LA LORY LATEKETEA KWA MOTO JIJINI DAR ES SALAM

Trela la lori lililokuwa limebeba mafuta likiteketea kwa moto mchana huu eneo la Kibamba Darajani jijini Dar es Salaam.haijafahamika mara moja chanzo kutokea kwa moto huo. Na kushoto ni baadhi ya wananchi wa eneo hilo la Kibamba wakishudia Trela la Roli likiteketea kwa moto.



DKT KIKWETE AMPA POLE PADRI AMBROS MKENDA WAKATI AKIUGUZA MAJERAHA YA KUPIGWA RISASI VISIWANI ZANZABAR.

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akimjulia hali Padri Ambros Mkenda wa Kanisa Katoliki la Mpendae mjini Zanzibar anayeuguza majeraha katika taasisi ya mifupa ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (Moi) jijijini Dar es salaam leo Jumamosi Dsemba 29, 2012 kufuatia kupigwa risasi sehemu za mdomoni na watu wasiojulikana mapema wiki hii wakati akisubiri kufunguliwa geti la nyumbani kwake maeneo Kitomondo Mjini Zanzibar akiwa ndani ya gari aliyokuwa akiendesha akiwa pekee yake. 
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akimsikiliza Padri Ambros Mkenda wa Kanisa Katoliki la Mpendae mjini Zanzibar anayeuguza majeraha katika taasisi ya mifupa ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (Moi) jijijini Dar es salaam leo Jumamosi Dsemba 29, 2012 baada ya kupigwa risasi sehemu za mdomoni na watu wasiojulikana mapema wiki hii wakati akisubiri kufunguliwa geti la nyumbani kwake maeneo Kitomondo Mjini Zanzibar akiwa ndani ya gari aliyokuwa akiendesha akiwa pekee yake. Rais Kikwete amempa Padri Mkenda pole nyingi na kumuombea apate nafuu haraka.


ARUSHA KUWA MAKAO MAKUU YA CHAMA CHA NGUMI ZA KULIPWA AFRIKA YA MASHARIKI NA KATI (ECAPBA).


    Chama cha Ngumi za Kulipwa Cha Afrika ya Mashariki na Kati (ECAPBA) kimepata makao makuu Arusha, hii ni baada ya Mstahiki Meya wa jiji la Arusha  Mh. Gaudence Lyimo kuomba kihamie Arusha ili kiweze kukaa karibu na “Jumuiya ya Afrika ya Mashariki, EAC”Rais wa ECAPBA Onesmo Ngowi alimhakikishia mstahiki meya kuwa ECAPBA itahamishia makao yake makuu katika jiji la Arusha. Kwa sasa ECAPBA ina makao yake makuu katika Halmashauri ya Manispaa ya Moshi.
       Juhudi za Mstahiki Meya Gaudence Lyimo za kukuza michezo na kukuza utalii katika jiji la Arusha ni moja ya sababu zilizomfanya rais wa ECAPBA kuamua kuhamishia makao makuu katika jiji la Arusha.
       Uamuzi huo uliungwa mkono na mmoja wa wanachama wa  ECAPBA bw. Daudi Chikwanje ambaye ndiye Katibu Mkuu wa Chama Cha Ngumi za Kulipwa Cha Malawi!
         Nchi ya Malawi ni mwanachama wa ECAPBA pamoja na Kenya, Zambia, Ethiopia, Burundi, Sudan ya Kusini, DRC, Rwanda, Uganda na Sudan.
      ECAPBA inaratibu ubingwa unaojulikana kama ECAPBF ambao unawapa mabondia wa ukanda huu kuwa mabingwa imara wa ngumi Afrika

MATAYARISHO YA ZANZIBAR KUHAMA ANALOGIA KWENDA DIJITALI YAENDELEA


                Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema matangazo ya mfumo wa Analogia yatazimwa rasmi katika Mikoa yote ya Zanzibar ifikapo Februari 28 mwakani ili kupisha mfumo mpya wa matangazo kwa njia ya Dijitali.
                  Waziri wa habari, utamaduni, utalii, na Michezo Said Ali Mbarouk ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na Waandishi wa habari katika ukumbi wa Habari maelezo kikwajuni mjini Zanzibar kuhusiana na matayarisho ya kuhamia katika mfumo mpya wa matangazo ya Dijitali.
             Amesema Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na Kamisheni ya Utangazaji Zanzibar (ZBC) zimeshauriana na kukubaliana kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iingie katika mfumo mpya wa Dijitali kwa awamu ambapo kwa zoni ya ZanzĂ­bar imekubaliwa kuwa February 28 2013 ndio iwe mwisho rasmi wa matangazo ya Analogi.
        Waziri Mbarouk amesema Wizara yake haitozima mitambo ya matangazo ya Analogi ifikapo Disemba 31 bali itakachofanya ni kutangaza kwa pamoja matangazo ya Analogi na Digitali kwa mfumo unaojulikana kitaalamu kama SIMU L CAST hadi itakapofika muda rasmi wa kuhama mfumo wa Analogy.
      Akizungumzia matayarisho ambayo yamefanywa na Wizara yake katika kuukabili mfumo mpya wa Matangazo ya Dijitali Waziri Mbarouk amesema tayari wamejenga kituo cha usambazaji ishara(signals) katika eneo la Rahaleo kitakachokuwa na kazi ya kupokea na kusambaza ishara na mitambo ya uendeshaji.

Maelezo na Faki Mjaka-Maelezo Zanzibar

Friday, December 28, 2012

KAGAWA KUWEMO KIKOSI KESHO DHIDI YA WES BROM


Shinji Kagawa anatarajiwa kuwepo katika benchi la Manchester United Jumamosi katika mchezo dhidi ya West Brom.

Shinji Kagawa
Kiungo aliyejiunga na United akitokea Borussia Dortmund alikuwa nje ya uwanja tangu October 23 kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya mguu mbayo aliyatapata katika mchezo wa vilabu bingwa ulaya(champions league) dhidi ya Braga.

Hapo kabla alitarajiwa kuwepo nje ya uwanja kwa wiki nne lakini kutokana na maumivu yeke kuendelea, akalazimika kuendelea kuuguza mguu kwa siku zaidi na tangu wakati huyo hajashuka dimbani.

Wednesday, December 26, 2012

AWAMU YA PILI YA OPARESHENI OKOA BONDE LA KILOMBERO



        Desemba 23 na 24, mwaka huu  Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Joel Bendera, aliongoza awamu ya pili ya Opareshani Okoa bonde la Kilombero kwa kutumia helikopta ya Jeshi la Polisi kwa  muda wa siku mbili  ambapo ng’ombe zaidi ya 5,000 walikamatwa na kuondolewa ndani ya Hifadhi.                                                       
        Ng’ombe hao ni sehemu ya waliobakia wanaokadiriwa kufikia 7,000 baada ya kuondolewa zaidi ya ng’ombe 370,000 kati ya waliokuwemo kwa pande zote mbili za Bonde la Hifadhi na Pori Tengefu la Mto Kilombero wapatao 380,000 kati ya Ulanga na Kilombero. Maeneo ambayo ng’ombe hao wameondolewa walikofichwa na wafugaji ndani ya hifadhi ya Taifa na Pori Tengefu la Bonde la Mto Kilombero ambayo hayakuweza kufikiwa na Askari kwa njia ya miguu ama magari isipokuwa kwa kutumia Helkopta.                         
SEHEMU YA BONDE LA MTO KILOMBERO LIKIWA LIMEHARIBIWA LINAVYOONEKANA TOKA ANGANI  (picha na John Nditi).
         Hata hivyo Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Bendera ameongeza siku kumi hadi Januari 3, mwaka 2013 kwa askari wa Kikosi maalumu cha Opereshani hiyo wanaojumuishwa Polisi, Mgambo, Wanyamapori na Magereza kushirikiana na wananchi kumalizia kuiondoa mifugo hiyo.                                                                      
 Mifugo inayoondolewa ndani ya Hifadhi na Pori Tengefu katika Bonde la Mto Kilombero , wafugaji wenye mifugo mingi wamekuwa wakihamia wao wenyewe maeneo ya kupekea mifugo hiyo kwenye minada inayotambuliwa kisheria kwa kuandikiwa vibali maalumu na mamkala husika na si kwamba hawana sehemu ya kwenda.                                                                                                                                                  
         Hata hivyo baadhi ya wafugaji hao wamekuwa wakisafirisha ng’ombe wao walioondolewa ndani ya Hifadhi na Pori Tengefu kuipekea maeneo ya minada ya Makuyuni, Mkoani Arusha, Pugu ,Dodoma na mingine iliyipo Mkoani Morogoro ukiwemo wa Dakawa.                                                                              
         Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, zoezi hilo halihusiki kuwahamisha wafugaji bali ni kuondoa ng’ombe walioingizwa ndani ya Hifadhi ya Bonde la Mto Kilombero na Pori Tengefu , na kwamba baadhi ya wafufaji walikuwa ni wakazi wamepunguza mifugo yao na michache waliyobakiza wamepewa maeneo ya ardhi za vijiji kulingana na matumizi bora ya ardhi kwa kuwa Wilaya ya Ulanga na Kilombero asilimia kubwa ya Vijiji vimepimwa ili kutenga maeneo ya mifugo kilingana na idadi yao inayohitajika.                       
           Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na uongozi wa Serikali ya mbili za Ulanga na Kilombero, Bonde la mto Kilombero limekumbwa na uharibifu mkubwa wa mazingira utokanao na uvamizi wa makazi, kilimo na mifugo ndani ya hifadhi na Pori Tengefu.                                                                                                        
          Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Pori Tengefu la Kilombero lipo katika Wilaya mbili hizo zinazogawanywa na Mto Kilombero , ambapo kwa miaka ya hivi karibuni kumekuwepo na ogezeko la makabila ya jamii za wafugaji wakiwemo Wamasai, Wabarbeig na Wasukuma, ambao wamehamia kutoka maeneo ya Mbeya, Shinyanga, Tabora , Arusha na Manyara.                                                                                                      
        Hivyo kutokana na kuingizwa kwa wingi kwa ng’ombe ndani ya Hifadhi hiyo , tangu mwaka 2006, uharibifu ni mkubwa na kwamba kisheria za mazingira na maliasili ambazo zimetungwa na kupitishwa na Bunge maeneo hayo nanapaswa kulindwa na watu kutoruhusiwa kuendesha shughuli za kilimo na ufugaji.       
          Operasheni hiyo ni utekelezaji wa agizo la Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanznaia ambaye sasa ni Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar , Dk Ally Mohamed Shein aliiyoitoa Aprili mwaka 2006 kuwa wafugaji na wakulima waliovamia mabonde na maeneo ya vyanzo vya maji ya Usangu na Kilombero waondoke mara moja.                                                                                                                      
          Agizo hilo lilitekelezwa katika bonde la Usangu kwa mafanikio, utekelezaji wa agizo hilo katika bonde la Kilombero halikufanikiwa na kusababaisha uharibifu kuongezeka kwa kiwango kikubwa .                          
BAADHI YA SEHEMU ZENYE MAJI BONDE LA MTO KILOMBERO  (picha na John Nditi).
         Pia opareshani hiyo pia ni utekelezaji mwingine wa maagizo na tamko la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , Dk Jakaya Mrisho Kikwete alilolitoa Novemba 25, 2008 la kuondoa mifugo katika Bonde la Kilombero .                                                                                                                                                  

FATHER AMBROS APIGWA RISASI - ZANZIBAR


        Watu wasiojulikana jana wamempiga risasi Father, Ambros Mkenda wa Kanisa Katoliki la Mpendae Mjini Zanzibar nje ya nyumba yake majira ya saa 12 jioni wakati akitokea kanisani.                                                                                                                                                    
Father Ambros Mkenda
      Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mjini Magharibi Aziz Juma Mohammed amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambalo alisema Father amepigwa risasi na ameumizwa sehemu ya kichwa na amekuwa akitoka damu nyingi kichwani na tayari anapatiwa matibabu katika hospitali kuu ya Mnazi Mmoja.                                                                                                              
           Amesema jeshi la polisi linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo ili kubaini wahusika walifanya uhalifu huo kwa madhumuni gani kabla ya kuchukuliwa hatua za kisheria.                                        
     Kamanda Aziz akisimulia tukio hilo alisema walipata taarifa majira ya saa 2 na kwenda katika eneo la tukio ambapo Father alikuwa akitokea kanisani na kutaka kuelekea nyumbani kwake wakati akiwa ndani ya gari ndipo aliposhambuliwa na watu wasiojulikana na kuanguka.                                                            
       Aidha Kamanda Azizi amesema Father Ambros yeye ni mhasibu pale kanisani na hivyo mara nyingi watu wananaamini kwamba katika siku za krismass mara nyingi sadaka hukusanywa fedha nyingi na hivyo wanamini kwamba alikuwa fedha mikononi na ndipo inawezekana waliamua kumpiga risasi wakitaka kuchukua fedha hizo.                                                                 
     Hata hivyo amesema uchunguzi wa awali ndio utakaoeleza ni suala gani lililopelekea kupigwa risasi lakini wanaendelea na uchunguzi huo ambapo uchunguzi ndio utakaojulikana sababu kamili ya tukio hilo.                                                                                                                                 
     Akizungumzia tukio hilo, Askofu Michael Hafidh wa Kanisa la Anglikan la Mkunazini amesema wamesikitishwa na wamepokea kwa mshituko mkubwa tukio hilo hasa kwa kuzingatia matukio kama hayo hayajawahi kutokea ya kuwahujumu viongozi wa dini.                     
CHANZO: ZANZIBAR YETU

Monday, December 24, 2012

RAIS WA TANZANIA ATOA MILIONI 30 KWA MRADI WA KULEA NA KUHIFADHI MBWA MWITU HIFADHI YA TAIFA YA SERENGETI MKOANI MARA

Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania akikata utepe
Rais Jakaya Mrisho Kikwete na viongozi wa Tanapa Jumapili Desemba 22, 2012 atoa mchango wa milioni 30 ili kuzindua boma maalumu la kulea na kuhifadhi mbwa mwitu kuashiria rasmi kuachiwa huru kundi la pili la wanyama hao (15) waliokuwa wamehifadhiwa kwa miezi kadhaa kwenye boma maalumu la mradi huo, lililojengwa katika eneo la Nyamuma, Magharibi mwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, mkoani Mara.

MECHI YA TANZANIA STARS VS CHIPOLOPOLO YAINGIZA MIL 109/-

  Pambano la kirafiki la kimataifa kati ya Tanzania (Taifa Stars) na Zambia (Chipolopolo) lililochezwa juzi (Desemba 22 mwaka huu) limeingiza sh. 109,197,000. Fedha hizo zimepatikana kutokana na watazamaji 17,383 waliokata tiketi kushuhudia mechi kwa kiingilio cha sh. 5,000, sh. 7,000, sh. 10,000, sh. 20,000 na sh. 30,000.                                                                                             
    Mgawanyo wa mapato hayo ulikuwa kama ifuatavyo; asilimia 18 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ni sh. 16,657,169.49, maandalizi ya mchezo sh. 55,339,510, tiketi sh. 5,803,900, ulinzi na usafi kwa Uwanja wa Taifa sh. 2,350,000, Wachina (technical support) sh. 2,000,000, umeme sh. 300,000 na maandalizi ya uwanja (pitch marking) sh. 400,000.                                                                                                                                
    Nyingine ni bonasi kwa Taifa Stars sh. 13,826,313, asilimia 20 ya gharama za mchezo sh. 2,504,022, asilimia 10 ya uwanja sh. 1,252,011, asilimia 5 ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) sh. 626,005 na asilimia 65 ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) sh. 8,138,070.   
    Mapato ya mechi nyingine za Taifa Stars ilizocheza nyumbani mwaka huu yalikuwa Taifa Stars vs Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo-DRC (Leopards) iliyofanyika Februari 23 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam sh. 32,229,000. Taifa Stars vs Msumbiji (Mambas) iliyochezwa Februari 29 mwaka huu sh. 64,714,000.                                                                                                    

    Taifa Stars vs Malawi (The Flames) iliyochezwa Mei 26 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam iliingiza sh. 40,980,000. Taifa Stars vs Gambia (The Scorpions) iliyochezwa Juni 10 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam zilipatikana sh. 124,038,000 na Taifa Stars vs Kenya (Harambee Stars) iliyofanyika Novemba 14 mwaka huu Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza iliingiza sh. milioni 45.